Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia mpango wa maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2024/2025. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii ya uhai na pia nampongeza Rais wetu kipenzi Mheshimiwa Mama Samia Suluhu kwa kazi zake kubwa ambazo anaziendeleza na tunaziona na pia nimpongeza Waziri wetu Mwigulu na Waziri wa Mpango, mmeandaa kitu kizuri tumekiona, Mwenyezi Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mchango wangu ni mdogo sana. Mchango wangu wa kwanza nataka nizungumzie Kada ya Ununuzi na Ugavi, sana sana Serikalini. Kada hii ya ununuzi na ugavi tunaona imeongezewa kazi, kuna kazi ambayo ilikuwa inafanyika kwenye kada ya uhasibu na ilikuwa inapatikana kwenye Finance Act, kuna masuala ya vifaa (assets) kazi hii ikiwa inafanywa na uhasibu lakini sasa hivi kuna mabadiliko ya sheria kazi hii imerudi inatakiwa ifanyike kwenye kada ya ununuzi na ugavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali. Kwanza naomba tuiandae kada hii kwa kazi rasmi ambayo inaingia kwenye kada yao. Tutaiandaaje kada hii? Kwenye Serikali yetu ninaona kada mbalimbali ambazo zipo, kwa mfano, kada ya uhasibu. Kuna Mhasibu Mkuu wa Serikali, kuna Mganga Mkuu wa Serikali, kuna Mfamasia Mkuu na kada nyingi zina Mkuu, mkuu mkuu wa Serikali lakini hii kada ya ununuzi ni kama vile imetengwa fulani kama vile siyo kada rasmi au siyo kada ambayo inafanya mambo ya muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke ndugu zangu, pesa kubwa ya Serikali, hela nyingi zaidi ya 80% inaingia kwenye ununuzi. Sasa kwa kuwa pesa nyingi ya Serikali inatumika kwenye ununuzi hii kada ninaomba tuiboreshe apatikane Afisa Ununuzi Mkuu wa Serikali. Kada inapokuwa haina mkuu kule juu inakuwa inalega lega, kwa sababu kuna mambo mengi yanashindwa kwenda sawa, kada hii inatumia pesa nyingi sana za nchi hii. Ninaomba sana kada hii iandaliwe, iwekewe Mnunuzi Mkuu wa Serikali, waweke malengo vizuri na kuwawekea kupokea kwenye kazi hii ya vifaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe pia kunapokuwa na Mkurugenzi wa Ununuzi awe na wasaidizi wake wawili. Mmoja awe anaenda kwenye ununuzi, mmoja awe anaenda kwenye vifaa kwa sababu, kada hii imeongezewa vitu ambavyo vilikuwa vipo kwenye uhasibu. Kada hii ya ununuzi naomba ku-declare interest, mimi mwenyewe ni mnunuzi, ninaifahamu. Kada hii huwa inapigwa vita na kupewa mizigo ambayo wakati mwingine siyo ya kwake. Mara nyingi malalamiko yakitokea kwenye ununuzi wa Serikali kwenye miradi mbalimbali ya Serikali wanatupiwa mizigo kada ya ununuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaambie leo, mara nyingi kesi mbalimbali zinazotokea, barabara mbovu, majengo mabovu, ununuzi wakati mwingine labda vitu vimefanyika visivyo, wakati mwingine siyo wanunuzi wanaofanya hayo mambo. Mnunuzi anafanya sehemu yake anayotakiwa afanye lakini yeye ni mtaalam wa ununuzi. Tukumbuke kwamba kwenye barabara kuna wataalam ma-engineer, kwenye majengo kuna wataalamu ma-engineer, wale ndiyo wanakuwa wasimamizi wakuu wa yale mambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana, mara nyingi sana wanapata lawama lakini baadae wanapokuja kufuatilia utakuta kada hii hawana kosa jamani, kuna watu pale nyuma yake ndiyo wanakuwa na makosa hayo. Kwa hiyo niombe kada hii tuimarishe, tuwatafutie semina vizuri, wapokee kazi ambayo imeingia iliyokuwa upande wa pili na tuwaimarishe jamani, kwa kweli tuwaimarishe, wanatumia pesa nyingi ya nchi yetu, wanatakiwa wapewe kazi na muongozo ulio imara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wetu wa Maendeleo ya Taifa 2024/2025 tunaona kwamba kuna vipengele hapa, kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani, kukuza biashara na uwekezaji, kuchochea maendeleo ya watu, kuendeleza rasilimali watu na vitu kama hivyo. Kipengele hiki cha nne kuchochea maendeleo ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wangu wa Lindi asilimia kubwa kuna kazi mbili zinazofanyika, wananchi wengi ni wakulima, wananchi waliobaki asilimia kubwa ni wavuvi. Nikija kwenye suala la wakulima hiki kipengele cha nne kinachosema kuchochea maendeleo ya watu, kule Mkoa wa Lindi mpaka majirani zake mwaka huu itakuwa ni shida sana. Kuna huyu mnyama tulishapiga kelele mara nyingi sana kwenye Bunge lako, huyu mnyama anaitwa tembo, kiukweli wananchi wa kule wanakufa, wanauawa na huyu mnyama, wakienda mashambani kulima mazao yanaliwa, watoto wengi wanashindwa kwenda shule, hata hao waliolima ni wachache, wengi wameshindwa kulima, hata hao waliobarikiwa wakaweza kulima mazao yote yanaliwa na tembo. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa
MWENYEKITI: Mheshimiwa Chinguile, taarifa.
TAARIFA
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge anazungumza vizuri, hata kule kwenye Jimbo la Nachingwea mwananchi ameuawa mara ya mwisho tarehe 17 Juni, mwaka huu kwa hiyo hali siyo nzuri sana. Naomba kuunga mkono anachokizungumza.
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Chinguile, Mheshimiwa Pathan.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa. Sasa hali iliyoko ni njaa…
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha ahsante.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja sijaongea kabisa. Hali ni mbaya na sheria zilizopo sasa hivi Maliasili kifutajasho heka moja mtu unamlipa laki moja, halafu pamoja na kwamba kifutajasho wanalipwa laki moja bado hata vifutajasho vya mwaka jana wananchi hawajapata. Hali ni mbaya sana, tuwakumbuke wananchi wetu, hali siyo nzuri jamani. Huyu mnyama tumewashauri kutengeneza solar electric fence hata kwenye sehemu chache, tunaomba Serikali itusaidie. (Makofi)