Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia katika Bajeti Kuu ya Serikali. Kwanza kabisa napenda kuanza kwa kuishukuru sana Serikali yetu, Serikali ya Awamu ya Sita, iliyo chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anayafanyia kazi maoni yetu sisi, kama Wabunge. Hiyo inatupa ari ya kuendelea kuishauri Serikali ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu, wakati tunajadili Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022 nilisimama hapa Bungeni nikaishauri Serikali ianze kutoza kodi ya huduma za kidigitali, yaani Digital Service Tax na Serikali iliichukua agenda hiyo. Sisi hapa Bungeni tulilipitisha jambo hilo na kati ya mwezi Julai, 2023 mpaka Aprili, 2024 Tanzania tumeweza kukusanya kodi kiasi cha shilingi bilioni 12.6 kodi ambayo awali ilikuwa haikusanywi. Kwa hiyo, naendelea kuipongeza sana Serikali kwa namna ambavyo tumeona hata katika bajeti hii ambayo tunaijadili hivi sasa inakwenda kujielekeza zaidi katika namna ya kuboresha malipo na uchumi wa kidijitali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huo napenda nianze kwa kuishauri Serikali, kama kweli nia ni hiyo na tayari tumeshaanza kuona matunda, naiomba sana Serikali kupitia Wizara ya Fedha/Benki Kuu, iweze kuruhusu malipo ya paypal. Maana haiingii akilini kwa nini, malipo ya paypal yamezuiliwa nchini kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bajeti Kuu hii ya Serikali ya mwaka 2024/2025 na kwa kuzingatia muda, mimi napenda nijikite katika maeneo machache yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea kukuza uchumi wa Taifa letu ni lazima tuone ni namna gani tutatanua wigo wa walipa kodi. Nimeshasema mara kadhaa hapa ndani ni lazima Serikali ije na jitihadi za makusudi kabisa za kurasimisha sekta isiyo rasmi. Katika kila shilingi kumi ambayo inazunguka katika uchumi wetu shilingi sita mpaka saba ipo katika sekta isiyo rasmi. Wakati umefika sasa kama ambavyo tunaisikia Serikali, kama ambavyo tunasikia Wizara ya Mipango na Uwekezaji, Wizara ya Fedha waweke mazingira wezeshi kwa ajili ya wawekezaji wa nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati umefika sasa Serikali iweke jitihada za makusudi kabisa kuweka mazingira wezeshi, kwa ajili ya biashara ndogo kuweza kufanyika hapa nchini. Bila ya kufanya hivyo tutaendelea kuzunguka bila kupata jawabu kamili kwa sababu, ni lazima turasimishe sekta isiyo rasmi, lakini ili kufanya hivyo ni lazima tuwavutie wale ambao wako kwenye sekta isiyo rasmi, waone umuhimu wa kurasimisha biashara zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi hapa nawasilisha ombi maalum kwenda kwenye Shirika letu hili la BRELA. BRELA ianzishe dirisha maalum, kwa ajili ya kusajili biashara zisizo rasmi bila ya gharama. Iwe kama ni moja ya kichocheo, kwa ajili ya hizi biashara ziweze kurasimishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kwamba, ni lazima tuje na mfumo ambao utaweza kupima utekelezaji wa hii mipango na bajeti yetu. Ni lazima tuwe na mfumo ambao utaimarisha nidhamu ya utekelezaji kama ambavyo awali tulikuwa tuna Big Result Now, si lazima tuchukue hiyohiyo, lakini tunaweza tukajifunza kutoka pale tukachukua baadhi ya mambo yaliyoko pale tukaborsha mfumo, ili tuwe na mfumo ambao utaimarisha nidhamu ya utekelezaji katika bajeti zetu pamoja na mipango yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kurejea, wakati tunajadili Mapendekezo ya Mpango wa Taifa kwa mwaka 2024/2025 nilisimama hapa Bungeni nikaiomba sana Serikali tunapokuwa tunatawanya fursa za uwekezaji na maendeleo katika Taifa letu la Tanzania tuhakikishe maeneo yote tunayafikia, tukiwemo sisi wa mikoa ya pembezoni. Niliongelea kwa upekee Mkoa wangu wa Kagera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa kuwasilisha ombi maalum, ombi la kipekee. Sisi pale Bukoba Mjini tuna machinjio ambayo imechoka, tuna machinjio ambayo haiendani na usalama wa chakula, kwa maana ya food safety, hili jambo limeongelewa kwa muda mrefu. Kwa hiyo, mimi ninamuomba sana Mheshimiwa Waziri atafute fedha, na hawezi kukosa kupata fedha, ili tujengewe machinjio ya kisasa pale kwetu Bukoba Mjini kwa sababu, miundombinu ya machinjio ya Bukoba Mjini imechoka, imechakaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina uhakika Mheshimiwa Waziri wa Afya, dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu akifika kwenye machinjio ya Buoba sio ajabu akasema isiendelee kutumika kutokana na hali iliyonayo. Kwa upekee na umuhimu huo na unyeti wake naomba sana na sisi tukumbukwe, kama ambavyo maeneo mengine yamekumbukwa na kujengewa machinjio ya kisasa. Sisi Bukoba Mjini pamoja na Mkoa wa Kagera sio kisiwa, sisi ni sehemu ya Tanzania kwa hiyo, tunaomba sana Serikali itutendee haki. Tunaomba sana na sisi Serikali itukumbuke, tunaomba sana Serikali itekeleze maombi yetu, tunaomba machinjio ya kisasa pale Bukoba Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapoelekea kuhitimisha pia, napenda kuishukuru sana Serikali. Moja ya agenda ambazo nimekuwa nikizisemea hapa Bungeni ni zao la vanila. Naishukuru sana Serikali kwa sababu, mwaka huu, mwezi huu, tarehe 18, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeita wakulima na wadau wote wa zao la vanila hapa Dodoma, kwa ajili ya kujadili upatikanaji wa soko na changamoto zake, lakini natumia fursa hii nikirejea pale kwenye umuhimu wa nidhamu ya utekelezaji. Basi naomba sana maazimio ya kikao hicho yatekelezwe, ili na sisi Mkoa wa Kagera, wakulima wetu wa vanila waweze kuneemeka na zao hili la vanila. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhitimisha. Wengi tumeguswa na kifo cha mtoto Asimwe, mtoto mdogo mwenye miaka miwili mwenye ualbino. Tumesikia kauli ya Serikali kupitia kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba, Serikali inakwenda kufanya nini. Natumia fursa hii, naiomba sana Serikali kwamba, sasa wakati umefika tupate Sheria mahsusi ambayo inahusiana na ukatili wa kijinsia kwa maana ya Gender Base Violence Act.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili Tanzania ilisharidhia kupitia SADC, ninakumbuka hata ukirejea Hansard utaiona. Wakati tunajadili Sheria za Uchaguzi na Sheria za Vyama vya Siasa Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama aliahidi hapa ndani ya Bunge kwamba, Sheria ya Ukatili wa Kijinsia italetwa Bungeni. Ni kwa kuwa na Sheria mahsusi namna hii hata yale ambayo yamepangwa kutekelezwa kupitia MTAKUWWA yataweza kufanyika. Kwa hiyo, ninaomba sana Serikali ilete sheria mahususi ambayo itaweza kupinga na kupambana na vitendo vyote vya ukatili kwa wanawake, wanaume, watoto na hata wenzetu wenye mahitaji maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuhitimisha naipongeza sana Serikali kwa kuondoa import duties kwenye uzalishaji wa taulo za kike kwa maana ya pedi, lakini naiomba sana Serikali kwamba, hii haitoshi, watoto wa vijijini wanateseka sana. Kwa hiyo, naomba watafute namna ya kupunguza gharama, kwa ajili ya taulo za kike, hususan kwa watoto wa vijijini. Mwaka jana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba alituambia kwamba, wataweka kwenye Mpango wa TASAF kwa wale wanafunzi ambao wako kwenye kaya za TASAF.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nashukuru sana kwa nafasi hii na ninasisitiza kwamba sisi Wananchi wa Bukoba Mjini tunahitaji machinjio ya kisasa kwa sababu sisi siyo kisiwa na sisi tunataka tujione kwamba na sisi ni sehemu ya Tanzania. Kwa hiyo, niombe sana Bukoba Mjini tupate machinjio ya kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nashukuru sana na naunga Mkono hoja.