Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

hon Hassan Seleman Mtenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Bajeti hii ya Mpango. Vilevile nimpongeze Waziri wa Fedha na Waziri wa Mipango kwa kutuletea bajeti moja ambayo inaweza ikakidhi mahitaji ya wananchi. Vilevile nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu hii nataka niseme kidogo, tunakwenda kwenye uchaguzi mwakani na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni Rais pekee atakayetoa matokeo makubwa ya kura ndani ya chama cha CCM. Kwa hiyo, tuwambie tu wale jamaa ambao wanapigapiga kelele kule nje kwamba Mheshimiwa Rais hana mpinzani ndani ya nchi hii. Kwa kazi ambazo amezifanya na anatufanyia inabidi na ni lazima tumpe salute yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia uchumi, lakini tunapozungumzia uchumi inawezekana ikawa kwenye mipango yetu tunakuwa na mipango mizuri sana, lakini kwenye utekelezaji kunakuwa na tatizo. Leo ukiangalia Kusini mwa Tanzania, tunazungumzia kule Mtwara na Lindi, sisi tuna Mto Ruvuma. Tunazungumza kilimo ndiyo uti wa mgongo, kilimo ndiyo Wizara ambayo inapata bajeti kubwa kwa sababu Rais ameamua sasa kuwabeba wakulima ndani ya nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwamba kwenye mpango sijaona jinsi gani hii mito ambayo ni kubwa, Mto Ruvuma sasa hivi maji yote yanaingia baharini lakini tukiwa na scheme za umwagiliaji mimi nadhani hata vijana wetu ambao wako kule idle hawana kazi za kufanya tukawatengenezea mazingira, tayari tutakuwa na nguvu kazi ambazo zinaweza kujiajiri. Kwa hiyo niombe Mheshimiwa Dkt. Mwigulu hili nalo mlizingatie na mliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza kuhusu suala la sukari na kwenye kipengele hiki nataka nizungumze kwa uchungu sana. Mimi nilishawahi kutoa document na kumpa mkubwa mmoja, nikamweleza jinsi gani tunavyodhulumiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni hizi na viwanda vyetu hivi vinavyotengeneza sukari, leo wanatoa sukari na delivery note lori zaidi ya nne, tano na kwa siku wanatoa lori zaidi ya 30 kwenda kwa mawakala. Zinavyofika kule kwa mawakala zinaingia godown. Wakala anauza sukari kupitia godown kwa delivery note na ina kwenda moja kwa moja kwenye duka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hebu tuangalie hapa ndipo tunapopoteza fedha za kutosha lakini klule kwenye kiwanda kuna watu wa TRA wako mule ndani. Leo nimshauri tu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, katika viwanda vyetu ambavyo vinazalisha sukari inawezekana siyo lazima sisi Wabunge tupige kelele hapa lakini inawezekana TRA wakajua kuanzia Januari mpaka Desemba gari ngapi za sukari zimetoka kwenye kiwanda “A” na zimekwenda wapi? Leo mkitoka moja kwa moja mkaenda Dar es Salaam mkasema wakala ni fulani amepokea gari 100, hebu tuangalie kodi yetu sasa ya gari 100 ambayo amechukua Mtibwa iko wapi? Hapo ndipo tunapoibiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaibiwa fedha nyingi sana. Sasa hao wakubwa, ukiuliza unatafuta mapambano. Leo ukiangali huku Dodoma Hotel kuna watu wenye viwanda huko wako huku wanawashawishishawishi Wabunge hapa. Baadhi ya Wabunge wanawaita wanawashawishi lakini nashukuru sana kwamba, Wabunge sasa hivi wamekuwa ni Wabunge wa kuwatetea wananchi na Serikali yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza dhana ya uchumi, sisi Mtwara mmetujengea airport kubwa sana. Tunamshukuru Rais kwa kutoa fedha nyingi sana kwa ajili ya airport, lakini Mtwara hatuna ndege na kama Mtwara hatuna ndege, juzi yametokea mafuriko tumeomba ndege Air Tanzania wametupatia ndani ya mwezi mmoja, inasikitisha. Ndege hizi mnazoziona za ATCL ni fedha za korosho. Kwa nini wana Mtwara wasifaidike? Mimi nimwombe Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana katika mfuko wetu ambao tuliuweka wa fedha za korosho zikachukuliwa na Serikali kwenda kununua zile ndege sisi tunasema ni jambo zuri sana, lakini kwenye keki ya Taifa inatakiwa kila Mtanzania apate. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tiketi ya kutoka Dar es Salaam kwenda Mtwara ni zaidi ya shilingi 600,000 siyo go and return, unakwenda mara moja shilingi 600,000 Precision. Sasa mimi nataka niseme, tufike mahali kama tuna mipango ya nchi basi tusiangalie kwenye eneo moja na haya nimekuwa nazungumza sana. Sisi Mtwara tuna shida ya umeme lakini tumshukuru sana Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, alivyoingia amepambana kweli kweli mpaka sasa hivi tumetoka kwenye ile shida ya umeme. Bado umeme ule hauna guarantee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna gesi, gesi ile imetoka Mtwara imekuja Dar es Salaam Kinyerezi inatengeneza umeme ambao umeingizwa kwenye Gridi ya Taifa. Kwa masikitiko makubwa sana tunatakiwa na sisi Wana-Mtwara tuingizwe kwenye Gridi ya Taifa tufaidike na ile gesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana tukazungumza na mipango hapa lakini hakuna mpango ambao tusiojadili fedha. Siku zote nilikuwa nazungumza kwenye Bunge hili nikawa nawashauri Mawaziri wenye dhamana kwamba, twendeni sasa tukajenge Daraja la Mozambique – Mtwara ambalo litachukua distance ya kilometa 100, tunaingia sasa Mozambique. Hili halihitaji Profesa wala mtu mwenye degree.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Dangote anauza cement Mbeya, Katavi, anashindwaje kwenda kuuza cement Msimbo na Playa? Kwa hiyo, kama tutafika tukafungua mpaka wa Mtwara, tukazungumza na watu wa Mozambique na kwa bahati nzuri wenzetu wa Mozambique wameanza kutengeneza barabara ya lami kilometa 15 kutoka Msimbo na Playa wanakuja Mto Ruvuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nataka nishauri, Waziri Fedha, Waziri wa Mambo ya Nje na Waziri wa Ujenzi kaeni mzungumze haya. Mimi namshukuru Waziri aliyepita aliweka token ya kutafutia fedha. Hata hivyo, token imewekwa toka mwaka 2022/2023 hakuna kinachoendelea. Sasa tusizungumze mipango bila kuwa na mipango ya kutafuta fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nataka nizungumze tena, tunapozungumza suala la sukari kwa kweli linasikitisha sana. Sisi tuna viwanda hapa lakini katika Nchi za Kiafrika, wananchi wanaonunua sukari kwa bei kubwa katika eneo lao ni Watanzania. Sisi tunapakana na Mozambique, tunapata sukari ya magendo ya Mozambique kwa shilingi 2,200. Sasa sikatai kama tunataka tuvi-handle viwanda vya kwetu lakini je, hivi viwanda vya kwetu Tanzania pamoja na kuwa vinalipa kodi vina masilahi gani kwa Watanzania? Vilevile, tuwanaangalie wananchi wetu kwa sababu leo ukisema sukari imepanda bei, kesho utasema unga umepanda bei. Maudhi ya vitu hivi kupanda bei yanakuja kwa Serikali yetu ya Chama Cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nikuombe nimshukuru Mheshimiwa Bashe, hiyo sheria inayotaka kuletwa sisi tunaisubiri tuipitishe ili tuendele sasa na mambo mengine ili wananchi wetu wapate unafuu wa sukari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ya kwangu yalikuwa ni hayo naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)