Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Fedha pamoja na Mpango wa Taifa na mimi nigusie pale alipomalizia Kamani hapa kwenye dollarization.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ningeshauri najua Wizara ya Fedha imefanya kazi nzuri sana na inaendelea kupambana sana na inflation na inaonekana lakini ijitahidi zaidi ipambane na black market. Huku benki tunasema ni 2,690, elfu mbili mia sita na ngapi, wanakuambia hakuna chukua 500, 300 huko nje ni 2,800 mpaka 2,850 ili tu-stabilize zaidi, tunao uwezo huo kwa sababu ni kitu kidogo tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niombe kuwe na special consideration kwa watu ambao bidhaa zao zote wanazo-deal nazo zinatoka nje. Mathalani watu wanaochukua tenda Serikalini halafu wana-order vitu nje, halafu vinachukua muda kufika, vilevile Serikali inachukua tena muda kuwalipa, sasa waki-deal na hela ya ndani tu bado wataenda kupata shida. Kwa hiyo hayo maeneo mawili matatu yakiwekewa mkazo hapo kwenye dola tutakuwa tumekaa vizuri lakini nakubaliana kabisa na lile wazo la Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze sana Wizara zote mbili kwa ujumla kwa eneo la wakandarasi. Nimeona ule ukurasa wa 54 wameonesha nia ya kuhakikisha wakandarasi wazawa ambao wanapata sub contract, inapotoka interest na wale wazawa nao wanapata ile interest, hilo ni jambo zuri sana. Ameongeza stake ya wakandarasi wazawa kwenye kazi ni jambo zuri sana tumelipigia kelele mara nyingi niwapongeze sana, niombe tu sasa tuangalie pia namna ya kuweka interest hata kidogo kwa wakandarasi wazawa kwa malipo yanayochelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba maeneo mengi yamekaa vizuri yako maeneo ambayo ninashauri Serikali i-consider kuyarekebisha. Eneo la kwanza ni ile faini ya kutokutoa risiti ambayo iko ukurasa wa 100 pale ambayo ni ile Sheria Namba 86(1). Unajua jinsi unavyoweka ile kodi ya juu au faini ya juu unatoa mwanya wa wale wanapiga ile kodi ku-negotiate ili walipe ile ya chini halafu wapate hapo cha juu. Kwa hiyo, mwisho mzigo utaenda kumdondokea mfanyabiasara wa kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuliangalie milioni 15 ni nyingi sana kuna maduka ambayo yanatumia EFD na milioni 15 ni almost mtaji wake hata kama turn over ni kubwa, sasa ukimwambia faini ni milioni 15, TRA wana mtindo wa kwenda kwenye ile ya juu ili mrudi mezani muongee na mkiongea pale unaona kabisa wana chochote ili warudi kwenye ile ya chini naomba tuliangalie sana hilo na ninaongea kama mtu ninayetoka kwenye jamii ya wafanyabiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ninapowashauri Serikali waiangalie ni eneo la ile tozo kwa magari yanayotumia gesi. Haya magari bado ni machache, motive yetu ni kutia nguvu au kuwasaidia magari yawe mengi, haya magari wanafanya modification kule nyuma unakuta wameweka mtungi wa gesi hakuna hata sehemu ya kuweka begi, sasa ikiwekea tozo ya shilingi 382 kwa kilo tayari unaanza ku-discourage, kwa sababu menzake yeye ana nafasi huko nyuma na huu mzigo ukimwangukia hawataona ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa sababu Rais anataka clean energy kwenye kupika definitely tunaenda kwenye clean energy kwenye magari pia. Ni afadhali ihamishiwe kwa sababu kwa sasa hivi miaka mitano ijayo magari ya umeme yatakuwa mengi, ni heri tuihamishie kwenye magari ambayo tunayaagiza ya umeme na hybrid ili tuweze kulinda hawa wa gesi kwanza, watakapokuwa wengi hiki chanzo kitakuwa na tija, lakini kwa hawa wachache ambao wako Dar tu ukawarundikia shilingi 382 naona ni nyingi sana, tuangalie hata 150 ili na wao waweze kupambana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nirudi eneo la road fund, barabara ni siasa, barabara ni maisha, barabara ni maendeleo. Tumekuwa tunawalalamikia sisi hapa wote Wabunge Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi kwamba barabara hazijengwi na nini lakii tunajua kile kikapu chetu kikoje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaushauri kwamba ni vizuri tuangalie namna ya kuimarisha mfuko ule, ndiyo sehemu ya kwanza ya kuanza, kwanza tuanze tuhakikishe ile hela yote inayokatwa kwenye maeneo yote iende yote kama ilivyo isiguswe. Wanasema sijui ni ring fencing kuna kiingereza chake, sasa ni vizuri yaende kwa sababu barabara kwa kweli itatusaidia sana kuharakisha maendeleo na tu aim juu zaidi siyo two trillion ambayo wamependekeza twende mpaka 2.5.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia zipo barabara za muhimu na zina maslahi kwa uchumi na zitapata watu. Tuende kwenye PPP na zile road toll kwa mfano ile barabara ya kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro ya njia sita tukaweka road toll hatujamzuia mtu kutumia hii ya kawaida kama ana haraka lakini maana yake tunamsaidia yule mwenye haraka kama kenya walivyoweka ile barabara ya haraka kutoka Mlolongo kwenda mpaka Westland, inakusanya hela na ile hela inaendelea kuingia kwenye Mfuko wa Barabara. Kwa hiyo ningeomba sana toll roads na PPP inaweza kusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la kuangalia kwa hara, hela inayokatwa kwa ajili ya REA tumeshapiga hatua kiasi gani kwenye REA? Si karibu tunamaliza vijiji vyote? Hatuwezi kuipunguza pale kwenye REA tukaongezea hapo kile kipande kilekile bila kuongeza kwa wananchi kikaenda kusaidia kwenye mafuta? Kwa hiyo nadhani kitasaidia kwenye barabara Road Fund ikawa ina hela hii itatusaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo ambalo ninapenda niishauri Wizara ya Ardhi na hii ishirikiane na Wizara ya Fedha. Watanzania wote hata mwenye kupata kipato cha shilingi laki moja wanajenga nyumba cash na kama wanajenga nyumba cash na nyumba ni security akiingia kazini akipata mwanya wa rushwa atakula, mwanya wa kuiba atakula kwa sababu security ya kwanza ni kupata nyumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tusirejeshe ile housing bank? Mtu akiingia kazini asaini mkataba kama ana kiwanja apate mkopo wa miaka 20, 30 wa kujenga nyumba apate amani na aheshimu kazi yake kwa sababu akiacha hiyo kazi tayari nyumba itauzwa, tuingize pale ili hiyo hela inayobaki mkononi kwa mtu kama tuna housing bank itumike kwenye maeneo mengine, ifanye uchumi wetu uchangamke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kujenga nyumba cash kwa kweli ni gharama sana na hela nyingi inaenda karibu vitu vyote ambavyo vinatoka nje. Kwa hiyo, nilikuwa nashauri sana tufikirie namna ya kuwa na Tanzania housing bank hasa kwa wale ambao wana maeneo yaliyopimwa na wana hati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iachane na biashara haiwezi, iachane kabisa na biashara, iendelee kutoa huduma. Kuna kiwanda kimejengwa pale Moshi cha Karanga Leather imeingizwa bilioni zaidi ya 100 na ni hela hiyo hiyo ya wastaafu NSSF sijui PPF Serikali ilikuwa inaleta viatu hapa pea moja moja imeshashindwa hata ile pea moja moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hauwezi kuwekeza Kiwanda cha Ngozi cha namna ile uendeshe kwa mtu ambaye anateuliwa hajawahi kuona Ngozi inatengenezwaje zile mashine ni za kisasa kabisa. Tuuze share 51% tubaki na 49%, kama ilivyo TBL kama ilivyo TPC na mashirika mengine walete hela wafanye kazi na tena iwe ni export kwa sababu kiatu kitakachotengenezwa pale kwa sababu mashine zile ni za leo za Italy za dunia ya leo kile kiatu hakiwezi kuwa bei rahisi sawa na mtumba unaotoka pale Kiboriloni road.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutengeneze au kama tukiamua kama hatutaki kukitoa tena kwa watu ili kilete hela za kigeni basi tuanze kupitisha sheria ya kwamba majeshi yote ya ndani yatumie viatu kutoka pale ambao sasa tunavunja tena ile nia halisi ya kuwa na soko la ushindani na hii ni kwa viwanda vyote Serikali haiwezi kusimamia kiwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kile kiwanda ukiuliza matatizo waliyonayo sasa hivi wanataka bilioni 10 working capital kwa nini? Mshahara wao hautokani na kazi wanayoifanya, hela ya NSSF imekaa pale, Magereza wamekaa pale, tuwape watu wenye uwezo watengeneze viatu kama inavyotengenezwa pale EPZ export sisi tupate hela na tuweze kutoa soko la ngozi na ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni hata kile kiwanda cha sukari cha Mkulazi hatuwezi mimi najua, kile kiwanda cha TPC kilikuwa cha kwetu tukatengeneza wenyewe mwisho wa siku tukaanza kubadilisha kila kitu, tukashindwa! Tumerudisha mpaka sasa hivi kinatoa gawio kwa Serikali. Kwa hiyo, nashauri hata kile cha Mkulazi tutafute wadau tuwauzie share, tubaki na share zetu za maana, ajira itokee na ufanisi uwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo la SGR, sijasikia kabisa SGR inakuja lini Kaskazini. Sasa purchasing power ya Kaskazini ni kubwa. Purchasing power ya Kaskazini hata hizo za luxury ni kubwa sana. Tuleteeni SGR, ianzie Dar es Salaam – Tanga – Kilimanjaro iende Arusha – Manyara mpaka Musoma iende itokee huko. Kule kuna purchasing power kubwa. Nina uhakika tutaweza kufanya marejesho kwa haraka zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo ambalo linahusu utumishi na nilishaliwasilisha mara kadhaa. Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana kwa kuboresha huduma za afya. Pale Moshi tuna KCMC ambayo ndiyo hospitali ya kanda, super specialist. Sasa hivi tuna deal na kansa, tutaenda kwenye kitengo cha moyo wameshakipatia fedha na tunaenda kwenye kufungua ubongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa shida tunayopata, salary scale yake haifanani na Bugando na haifanani na Muhimbili. Maana yake ni nini? Mfanyakazi kuliko abaki pale, super specialist, anaona mazingira mazuri zaidi aende Bugando au aende wapi. Hilo ni suala la kurekebisha tu ili hizi huduma zitolewe kote kwa usawa na sisi tuendelee kuwahudumia wananchi wetu vizuri. Tayari uwekezaji ni mkubwa, naomba sana Serikali ifikirie namna ya kuweka salary scale ambayo inafanana kwa hizi super specialist hospitals.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ni vizuri Wizara hii ya Mipango ifanye kazi kwa uchungu kama mtu binafsi, kama mchaga au kama mpare kwa maana ya kwamba, haiwekzekani kuna mradi Serikali imepeleka shilingi bilioni saba ujenzi wa stendi ya Mfumuni. Halmashauri imeshindwa ku-negotiate. Shilingi bilioni saba imekaa pale chini na kile ni chanzo cha mapato kwa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashindwa kuwafata CRJE. Hawa watu wakubwa walioko hapa, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Mheshimiwa Professor Kitila wakienda CRJE ambao mnawalipa kwa miradi mingine mkawaambia, bwana tuna interest na hili eneo kwa sababu hela imekaa chini muda mrefu tunaihitaji ili iongeze mapato Moshi na iingie Serikalini warudi site wamalizie ile stendi imebaki kiasi kidogo sana. Tunatenga fedha, lakini tunashindwa kupata wakandarasi kurudi.
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante muda wako umeisha.
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi kabisa naomba niunge mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)