Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Ali Hassan Omar King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Jang'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nashukuru sana kwa kupata hii nafasi. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametupa uhai na siku ya leo hapa tupo tunajadili maendeleo ya Watanzania wenzetu kwa niaba yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, natoa shukrani kwa Serikali. Nafikiri tulipokuwa katika Wizara mojamoja tuliishauri Serikali vitu vingi na Serikali imekubali na imepokea vitu vingi ambavyo sisi tunaviona. Kwa hiyo, tunaishukuru sana Serikali yetu hii sikivu. Tunampongeza na tunamshukuru sana Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutusikiliza Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulivyokuwa tunachangia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, tukasema kwamba hii Wizara imetengwa lakini sasa kwa kubadilika muundo kwamba tayari tunaona makundi maalum na masuala ya jinsia yanaenda kushughulikiwa na yatapata solution. Tulisema sana kuhusiana na maadili. Kwa hiyo, mama ameweka Naibu Makatibu Wakuu wawili. Kwa hiyo, hapa tunaishukuru Serikali hii inatusikiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tulikuwa tunalia na pensheni za kiwango cha chini, kwamba ziko chini sana lakini Serikali imetusikiliza. Japo kwamba hawakusema watafanya nini au itakuwa ngapi lakini naamini kwamba Serikali inaweza ikafanya vizuri kwa kitu ambacho kinaweza kikaja kikawafanyia watu vizuri. Pia, tulisema kuhusiana na fedha za wamachinga; sasa hivi zimeshatoka ila tulikuwa tunaomba ziongezwe kwa sababu hili kundi ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo haya yanaonesha kwamba Mama Samia Suluhu Hassan ndiye mtu maarufu sana ndani ya CCM na nje ya CCM. Ndugu zangu niwaambie ndani ya CCM hatuwezi kuwa na mtu kama Mama Samia Suluhu Hassan na ndani ya CCM tunapimana kwa utekelezaji wa Ilani. Sasa ukijitokeza wewe mwana CCM ukasema labda kwamba unataka kupambana ina maana kwamba utekelezaji wa Ilani haujafana. Tumeona ametekeleza Ilani kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo twende tukatazame katika masuala ya skuli, masoko ya maendeleo, maji, umeme vijijini, barabara na katika maeneo ambayo yameigusa jamii. Wapinzani tuliokuwa nao katika Bunge la 11 walikuwa na msemo wao, “Ni kweli CCM inafanya maendeleo lakini wanafanya maendeleo ya vitu”. Sasa hivi CCM inafanya inafanya maendeleo ya vitu na bado tunafanya na maendeleo ya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi mishahara imeongezwa. Tunashukuru kwamba watu wamepanda vyeo na ajira zimetoka katika maeneo chungu nzima kama tulivyokuwa tunazipata takwimu. Kwa hiyo, hiyo inaonesha wazi kwamba ndani na nje ya CCM hakutakuwa na mtu mzuri wa kugombea Urais isipokuwa ni Mama Samia Suluhu Hassan na hapa naungana na Dkt. Nchimbi anayesema kwamba, “Mama mitano tena.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kuwa mwalimu. Unapotoa suala, halafu unaweka na suggested solution halafu unaweka na marking scheme. Sasa unampima mtu yale masuala yako ulitaka ajibu sababu tano yeye anakupa sababu kumi na wewe ulitaka tano. Hapo maana yake kwamba huyu mwanafunzi right unayomtilia hutii kwa kinukta kimoja kimoja unapiga ile right moja kubwa kwa sababu amejibu zaidi ya majibu yaliyotakiwa Hivi ndivyo alivyofanya Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati katika paragraph ya 5.1 iliishauri Serikali kuwa na nidhamu ya upelekaji wa fedha ambazo ring fence. Mheshimiwa Tarimo amezungumza hapa, hizi ring fence kama hatujazipeleka kwa nidhamu nzuri ina maana kwamba moja kwa moja tunakwenda kufeli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mfuko wa barabara ambao ni road fund. Makusanyo yalikuwa shilingi bilioni 906 lakini fedha zilizopelekwa ni shilingi bilioni 382, sawa na 40%. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu umekuja na mabadiliko ya sheria. Nimeona humu katika finance bill kwamba unataka kuweka contingency fund kwa ajili ya barabara wakati hizi fedha zipo na tunaweka makadirio madogo kuliko makusanyo. Kwa mfano Bajeti ya Mwaka 2021/2022 tuliweka bajeti ya shilingi bilioni 908 lakini tukapata takriban shilingi trilioni moja; hiki kiwango kilipelekwa. Mwaka 2022/2023 tuliweka bajeti ya shilingi bilioni 857 lakini tukakusanya shilingi trilioni moja, tukapeleka shilingi bilioni 800.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ina maana kwamba hizi fedha zinaenda wapi na wakati hapa tulipata matatizo na changamoto za barabara na wakati mfuko wa barabara fedha ya makusanyo makubwa ipo; hizi fedha zilienda wapi? Yale malalamiko na vilio tuliyokuwa tunalia kwa kukatika madaraja na barabara fedha si zilikuwepo? Kwa nini zisiende na hizi ring fence? Hili nilikuwa naomba kwamba Serikali tuwe na nidhamu. Hii imesemwa katika page ya 51 na Kamati, mpaka 57 wametaja mifuko yote. Kwa hiyo, hapa nilikuwa naomba tuwe na nidhamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine nazungumzia katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii. Juzi Mheshimiwa Dkt. Mwigulu alivyosoma hotuba yake hapa alisema kwamba katika Deni la Taifa kilichoongezeka miongoni mwao ni shilingi trilioni mbili ambazo ni hatifungani za Serikali ambazo walikubaliana na mifuko ya hifadhi lakini tumesahau kuli-calculate hili Deni la Taifa la Ndani, kwa sababu nyuma ya mwaka 2000 huko, kwa miaka 20 nyuma, Serikali ikidaiwa na mifuko shilingi trilioni 5.9 na hawajaanza kuzilipa; walianza kuzilipa baada ya miaka 20. Tunaonaje zingelikuwa zimewekezwa na zikawa zinapata faida, zingekuwa ngapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa nini hatuwalipi na riba hizi fedha na kwa nini kwenye Deni la Taifa hatu-account hiki kitu? Kwa sababu hizi fedha ni za wananchi katika mifuko. Kwa hiyo, hili deni kama tutalitazama Deni la Taifa basi hebu tujaribu kuingiza na hiki na ndiyo maana tunaweza tukapata tabu kikokotoo kiwe kipi kwa sababu zile fedha zilizowekezwa kule nyuma hazikulipwa ndani ya miaka hiyo 20. Zingekuwepo kwamba zimewekwa na Serikali inatambua deni basi angalau lingekuwa limekaa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine tunazungumza kikokotoo; kusema ukweli Watanzania wengi hawajui kipi kipo katika kikokotoo. Watu walikuwa wakipokea 25%. Zaidi ya 81% ya wafanyakazi ilikuwa wanapata kikokotoo cha 25%, kikaja 33%. Kilipokuja 33% tunaishukuru Serikali kuja kupeleka kwenye 40% na wengine wakaenda kule kwenye 25%. Kinachotakiwa hebu haya mashirika yetu yatoe elimu; watakapotoa elimu watu watafahamu. Serikali inafanya jitihada na kwa upande wake imetusikiliza lakini watoe elimu. Naamini ni elimu ndiyo kilichokosekana. Kwa hiyo, hiki kama kitatolewa elimu kinaweza kikakaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali sasa imeamua katika monetary policy wamesema watatumia interest rate base monetary policy. Sasa wasiwasi wangu kwa mujibu wa formula na mataifa mengine wanavyotumia ni lazima kutakuwa kuna changing of interest rate katika kipindi kifupi kifupi. Serikali mara nyingi inakaa na madeni ya wakandarasi au ya watu ambao wamefanya zabuni zao kule Serikalini. Wale wameenda kukopa benki kwa kupitia fedha ambazo wameshatoa huduma Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa je, itakapokuwa kwamba ile interest ina change huyu atakapoanza kwenda kukopa hakutakuja kuwa na hasara na hawezi kuja kupata maumivu? Serikali ikae ijaribu kuangalia au kama kuzielekeza hizi benki tuanze sasa mambo ya hedging, vinginevyo bila ya hivyo tunaweza tukaja tukaathiri uchumi wa wafanyabiashara wetu ambao fedha zao ziko Serikalini. Sasa hili napenda Serikali ijaribu kuliangalia na itakapoliangalia ije na majibu mazuri, ituambie nini kinaweza kikafanyika. Kuna athari nyingi sana, lakini moja kwa hawa watu ambao wametoa huduma Serikalini halafu wakawa wanadai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongeze tena kutoa shukurani kwa Serikali; Serikali ya Chama cha Mapinduzi inafanya vizuri na inajali watu. Hapa nitoe msemo mmoja; wasitokee wengine wakawa kurumbizi. Kurumbizi akitoka kwenye kichaka anaanza kusema kichaka hiki kichaka gani; kichaka hiki kichaka mavi. Usiku ukifika anarudi tena palepale anaanza kunyenyekea; Kichaka hiki kizuri; kichaka hiki kinanukia. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha, ahsante sana.

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, CCM kichaka kinachonukia anayeona kichaka mavi siyo CCM, nashukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)