Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru sana kwa kuniruhusu na mimi nichangie bajeti hii ya Serikali ya mwaka 2024/2025. Nianze kwanza kuwapogeza Ndugu yangu Mwigulu na Naibu Waziri wake, pia Profesa Mkumbo na Naibu Waziri wake, wamefanya kazi nzuri sana kuandaa bajeti hii. Matokeo yake bajeti hii imelenga katika kuendeleza miradi ya kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tuna mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo ndiyo uti wa mgongo wa umeme wa REA Vijijini, kama bwawa hili halijakamilika basi umeme vijijini itakuwa hadithi, hautawaka, utakuwa unawaka na kukatika. Vilevile, bajeti hii imelenga kumalizia mradi wa SGR Lot 3, 4 na 5. Reli hii ikikamilka itafanya kazi ya kuongeza mapato na tuna mapango wa kupeleka mpaka Musongati kule Burundi ambako ingebeba mizigo mikubwa na kuingiza hela kwenye Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Msalato cha Kimataifa ili ndege za kimataifa ziweze kutua hapa na Serikali ipate fedha. Pia ujenzi wa barabara na madaraja makubwa hasa lile la Kigongo – Busisi litasisimua uchumi katika maeneo hayo ya Kanda ya Ziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumeongeza bajeti kwenye bajeti hii. Tumeongeza matumizi ya bajeti ya TARURA kutoka shilingi milioni 710 mpaka shilingi milioni 825, hili si jambo dogo tuipongeze sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hatua hii ya bajeti Waziri Mwigulu ameeleza dhamira ya Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan kukuza huduma za afya, maji, elimu na anaongelea nishati safi kwa akina mama hasa vijijini, jambo ambalo litaleta faida kubwa sana ya kiafya na nafuu kwa akina mama. Vilevile, kule kwangu Tabora tuna kazi mbili kubwa sana ya kukata miti, eneo la Mkoa wa Tabora tunakaribia kuwa jangwa kwa sababu tunalima sana tumbaku na hatuwezi kuacha kulima tumbaku, inaleta fedha Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakata miti kukaushia tumbaku na kwa ajili ya kupikia kuni na mkaa. Wazo hili la Mama Samia Suluhu Hassan la kuleta nishati safi ya kutumia gesi na nishati mbadala itaokoa miti ambayo itasaidia sana hapo baadaye ili wajukuu zetu waikute Tabora yenye miti badala ya jangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango mizuri hii ya kuleta maendeleo na kukuza uchumi ina changamoto kwetu. Tumefurahia mambo mazuri lakini hela za mama katika Jimbo langu la Tabora Kaskazini na maeneo mengine imezima zile changamoto kubwa zilizokuwepo. Naishauri Serikali ingezifanyia kazi changamoto hizi ambazo zipo, kwa mfano, uwekezaji mkubwa sana katika sekta ya elimu, madarasa na shule nyingi zimejengwa za sekondari na msingi, limetokea tatizo kubwa sana la upungufu wa nyumba za walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vyetu kwa mfano Wilaya ya Uyui na vijijini kote hatuna nyumba za kulala wageni za kukodisha, kila mtu na nyumba yake kwa hiyo walimu hawa, fikiria amechukuliwa amepangwa shuleni kijijini anapelekwa na gari la Halmashauri mpaka pale kijijini shuleni anateremshwa basi, mwalimu atalala wapi? Hali ni mbaya sana, watu hapa mjini walimu wanasema hawana nyumba lakini kuna nyumba za kupanga, kule kijijini hakuna nyumba ya kupanga hata moja. Walimu hawa wanalala nyumba moja iliyopo pale shuleni watu saba, nane, kumi na wana familia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano katika Halmashauri yangu, mahitaji ya nyumba za shule za msingi za walimu ni 1,720 zipo 261 pungufu ni nyumba 1,459. Watoto wetu, wanafunzi wetu na walimu waliopangwa vijijini wanalala wapi? Sisi tumejengewa shule nyingi, Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana kuleta fedha za madarasa, shule mpya na kadhalika, walimu nyumba hakuna, kwa hiyo bajeti hii itibu suala la nyumba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naliona napata taabu sana ninapoenda kutembea, mimi naenda vijijini sana. Ukiuliza mwalimu unakaa wapi anakuambia nyumba hii, mwalimu unakaa wapi, sina nyumba; unakaa wapi, nakaa na jirani. Hiki ni kitu kibaya sana naomba bajeti hii ifikirie sana suala la nyumba za walimu kule vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala lingine la watoto wa mitaani. Serikali tumetunga sheria ya mimba za utotoni lakini tumelenga sehemu ya watoto wanaosoma shule. Hilo ni kundi moja. Wapo watoto wengi mimi nilikwenda Mwanza juzi hapa wanasema wamekusanya watoto wanawarudisha majumbani kwao, mimi naona uchungu sana. Badala ya kutatua tatizo watoto hawa wanapata mimba mitaani halafu wanaenda kuzaa wanarudi mitaani. Watoto wa shule wanapata mimba shuleni halafu wanarudi shuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina data gani za watoto waliopata mimba za utotoni wapo mitaani, nini kinafanyika? Tulikaa Bungeni hapa tukapitisha sheria kwamba watoto wa shule wakipata mimba, kwanza aliyemtia mimba miaka 30 lakini akimbaka ni maisha. Akipata mimba ajifungue mtoto arudi shuleni, lakini watoto wa mitaani wanapata mimba wanarudi mitaani. Tunazo Wizara mbili, Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu na Wizara ya Wanawake, Jinsia na Wenye Mahitaji Maalum. Wizara hizi zina sheria za kibaguzi kwa watoto wa mitaani, watoto wa mitaani nani baba yao anawatunza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaona uchungu kwa watoto wa shule tu? Hawa watoto dawa siyo kuwakamata na kuwapeleka majumbani kwao, watarudi tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana bajeti hii iongezwe kwenye Wizara hizi mbili zipewe majukumu ya kuwachukua watoto wa mitaani na kupata utatuzi wake, siyo kuwatia kwenye malori na kuwarudisha majumbani kwao walikotoka. Wajawazito, wagonjwa wanaumwa, hili ni tatizo kubwa sana kitaifa pia hii ni nguvu kazi kubwa, mimi naomba Serikali hii inisikie na Mheshimiwa Mwigulu jaribuni kusaidia watoto hawa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Naibu Waziri.

TAARIFA

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuheshimu na kumpongeza mchangiaji Mheshimiwa Mbunge anachangia vizuri, lakini nataka kuweka kumbukumbu sahihi kwamba Wizara ya Kazi, Vijana na Ajira na Wizara ya Maendeleo ya Jamii kwamba zinabagua mtoto wa mtaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza katika sheria na sera zetu tulizonazo tunayo Sera ya Masuala ya Haki za Watoto na tunayo Sheria ya Mtoto tumetunga katika nchi hii. Sambamba na hilo pia tuna Katiba ya nchi ambayo inazuia kuhusiana na masuala ya ubaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahsusi kwa uzito Serikali iliamua kuandaa na kuwa na Wizara maalumu zitakazoshughulika na masuala ya watoto, ikiwemo Wizara ya Afya na hii ya Maendeleo ya Jamii. Katika kufanya hivyo zipo taratibu na sheria mbalimbali zinazoongoza namna gani ya kushughulika na masuala ya watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hata hao watoto wa mtaani, mitaa haina watoto kwanza nataka tu kuweka tu kumbukumbu vizuri. Kwa hiyo, watoto wanazaliwa, isipokuwa kuna masuala ya makuzi na malezi ambayo inakuwa ni wajibu wa msingi kwa mujibu wa sheria ya mtoto kwamba, wazazi na walezi tunao wajibu kuweza kuhakikisha kwamba tunashughulikia masuala hayo. Kwa hiyo, kwa kushirikiana na Serikali tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali kwanza kuweka bajeti kwa ajili ya masuala ya watoto na kuangalia masuala ya ustawi wao, makuzi yao na malezi yao kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Serikali tumeendelea kutekeleza hayo tofauti na jinsi alivyosema Mheshimiwa, nataka kurekebisha hapo tu, ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante na kabla sijamuuliza Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Naibu Waziri unachotaka kusema ni kwamba Serikali ina mechanism ya ku-capture makundi yote ya watoto waliopo kwenye mifumo rasmi ya malezi na wale ambao hawapo kwenye mifumo rasmi ya malezi, ndicho unataka kusema?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo.

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Almas Maige unapokea taarifa ya Mheshimiwa Naibu Waziri?

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nilindie muda wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu Naibu Waziri amesema mengi lakini Serikali haina data ya watoto waliozaa watoto wenzao (mimba za utotoni) huko vijijini, mitaani na mijini. Watoto wakazaa watoto wenzao ila tunajua watoto wa shule waliozaa watoto wenzao tunajua.

Mheshimiwa Mwenyekiti basi naomba niseme hilo suala la watoto la ubaguzi sheria ya ubaguzi nimelitoa, lakini naona kama sheria zilizopo haziwasaidii watoto ambao wamefurika katika mitaa yetu na wanalala huko na kupata mimba za utotoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirudi Naibu Waziri ametumia muda wangu mrefu, naomba sasa nishukuru kwamba Serikali…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Almas Maige nakuongezea dakika moja uhitimishe.

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru ahsnate sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nyingi alizozifanya katika Jimbo langu. Kwa miaka mitatu hii ametuletea karibu shilingi 55,600,000,000 na hii imetupatia Hospitali ya Wilaya, sekondari mbili, shule ya msingi na Kituo cha VETA na mengine mengi. Pia barabara tumetengeneza na elimu tunasoma kama vile ada. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, mwaka huu Serikali katika bajeti yake imepanga kujenga shule yenye ahadi ya Marais watatu pale Benjamin Mkapa, Kijiji cha Migugumalo, nashukuru sana Serikali. Pia, lipo tatizo dogo sana kwenye Wizara ya Nishati umeme unakatika kila mara kwenye Makao Makuu ya Wilaya ya Uyui, ambapo sasa kuna mabenki na vituo vya mafuta lakini wafanyakazi na watumishi hawafanyi kazi vizuri. Tatizo kubwa tuliambiwa ni urefu wa njia inayotoka Tabora mpaka Chaya hapa Manyoni, ikitokea shoti yoyote huku mpaka Isikizye kule Makao Makuu ya Wilaya. Tulisema dawa ni kuunga circuit breakers ama kujenga kituo cha kupoozea umeme. Naomba bajeti hii ifikirie suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniongezea muda. Naunga mkono hoja. (Makofi)