Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
House of Representatives
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii, lakini nikupongeze kwa namna ambavyo unaendelea kutuongoza na kumsaidia Mheshimiwa Spika tangu asubuhi unaendelea kuongoza vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, ambaye ametupatia uhai na uzima hadi sasa hivi tupo tunaendelea na majukumu yetu. Sambamba na hilo nimpongeze na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa na nzuri anayoendelea kuifanya ya kulitumikia Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mama yetu anaendelea kuwa msikivu sana. Amekuwa msikivu kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi mbalimbali. Bajeti hii ambayo tunaijadili hapa na mpango ambao tunaujadili leo ni matokeo ya maoni ya Wabunge waliochangia kwenye bajeti mbalimbali za kisekta, kwa kweli ni jambo la kumpongeza sana mama yetu amekuwa msikivu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kulikuwa na changamoto nyingi kuhusiana na wafanyakazi mbalimbali ambao walikuwa wanazungumzia suala la kikokotoo, mama amesikia kilio kile na sasa anakwenda kutatua changamoto ambayo ilikuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mama amekuwa muungwana sana, mama yetu amekuwa mwadilifu sana. Ni mzalendo sana kwa Taifa hili na ndiyo maana anaendelea kutuletea mipango mizuri na bajeti nzuri, leo hii endapo bajeti hii itapita tunaamini kwamba changamoto nyingi za watanzania zinaenda kutatuliwa kupitia bajeti hii ambayo tuna matumaini nayo makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ni Rais ambaye ana misimamo isiyoyumba na isiyoyumbishwa, kutokana na misimamo hiyo ndiyo maana leo mradi wa SGR unandelea kwa kasi kubwa, ndiyo maana leo hii mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere umefikia zaidi ya 97%, ndiyo maana leo hii mradi mkubwa unaendelea kuwekezwa kwenye bandari yetu ya Dar es Salaam na bandari mbalimbali, ndiyo maana kuna mabadiliko na mapinduzi makubwa sana ya sekta ya elimu, afya na miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kwamba mama yetu analitendea haki Taifa hili sana na anawatendea haki watanzania, tuendelee kumuunga mkono, kumuombea kwa Mwenyezi Mungu Allah ampe afya na umri mrefu lakini busara na hekima ziendelee kumtawala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumebarikiwa sana Tanzania na rasilimali nyingi sana. Moja, miongoni mwa rasilimali ambazo tumebarikiwa nazo ni bahari. Bado mchango wa bahari kwa maana ya sekta ya uvuvi ni mdogo sana kwa Taifa letu. Bado hatujaweza kuwekeza kwenye bahari kasa kwenye uvuvi wa Bahari Kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ni ya tatu kwa ya nne kumekuwa kuna mpango wa ununuzi wa meli nne kubwa ambazo zitakwenda kuvua kwenye bahari ya kina kirefu (Bahari Kuu), lakini mpango ule hadi leo bado haujatekelezeka. Kwa hiyo, ninaiomba sana Serikali kwa sababu meli hizi nne zilikuwa zina mgao kwamba mbili zitanufaisha Zanzibar na mbili zinakuja hapa Tanzania Bara, lakini sisi kama Zanzibar tulikuwa tunazisubiri kwa hamu kubwa meli hizi kwa sababu kule tunakwenda na uchumi wa bluu. Meli hizi zitakuja kutusaidia sana kuongeza Pato la Taifa letu pia litakuja kusaidia sana kwenye kutatua changamoto za ajira hasa kwa vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasubiri sana na tunamuomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie mradi huu na mpango huu umefikia wapi? Kwa sababu mara nyingi tumekuwa tunaulizia lakini bado majawabu yanakuwa tunasubiria kwamba, mpango wanasema umekamilika lakini hadi leo hii bado jambo hili halijatekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala la manunuzi. Hizi fedha nyingi ambazo tunazipitisha ama tunazijadili leo, bajeti hii, asilimia kubwa inakwenda kwenye manunuzi. Suala la ku-comply na sheria mbalimbali za manunuzi ni jambo moja lakini jambo kubwa ambalo ninataka kulizungumzia ni suala zima la value for money kwenye manunuzi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunatekeleza miradi mikubwa, ni kweli miradi ya miundombinu inajengwa lakini nisisitize na niiombe sana Serikali kwenda kusimamia manunuzi haya yazingatie zaidi value for money na kuweza kuokoa fedha za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo lazima tuweke mifumo ya uwajibikaji ambayo iko wazi ili kuona kwamba manunuzi haya yanafanyika kwa utaratibu mzuri na yanazingatia thamani halisi ya fedha ya Umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nimalizie kwa kusema kwamba, kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi imehimiza suala la ushirikiano wa Serikali zetu mbili, hasa zile Wizara ambazo si za Muungano. Ninaipongeza sana Serikali ya Awamu hii ya Sita, imeendelea kushirikiana sana na Serikali ya Awamu ya Nane ya Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi, hasa Wizara zile ambazo si za Muungano lakini bado kuna taasisi ambazo ushirikiano wao haujawa imara, hususan kwenye maeneo ambayo Tanzania inawakilishwa kwenye mambo mbalimbali ambayo yako nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe sana Serikali isiishie huku juu kwa Mawaziri kwenye ushirikiano, hadi taasisi zetu ambazo tunazisimamia wahimizane kwenye kushirikiana taasisi ambazo siyo za Muungano zilizoko huku Bara na kule Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na niiunge mkono hoja hii, ahsante. (Makofi)