Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuwa kitinda mimba katika siku ya leo, katika kuchangia bajeti hii ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa shukrani na kuwapongeza Mawaziri wa Mipango na Fedha, vijana hawa wa Singida wenye akili nyingi kwa jinsi ambavyo wanaifanya kazi kwa weledi mkubwa na kwa uaminifu mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua kushikilia pochi ya nchi lazima uwe mwaminifu na mtu ambaye unachapa kazi na ndiyo maana unatosha sana Mheshimiwa Waziri na tunakupongeza na tunakuamini Mkoa wa Singida jembe letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninataka nichangie kwenye barabara, ninajua barabara wameongea watu wengi sana lakini barabara za katikati ya nchi, Mkoa wa Singida na Dodoma ni barabara za kimkakati. Kwa sababu unapotaka kwenda popote kwenye nchi hii, kutoka Kaskazini kwenda Kusini, Kusini kwenda Magharibi, Mashariki, popote, lazima utapita katikati ya nchi. Kwa hiyo, tunaposema barabara hizi zitengenezwe kwa kiwango cha lami, maana yake zinatumika na nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu akiwa pembeni kule anaweza akawa anamaliza mambo yake kule, lakini ukitaka kwenda Mwanza utakatiza Singida, ukitaka kutoka Mbeya uende Arusha utakatiza Singida. Sasa unatoka huku na lami unafika hapo katikati unaingia kwenye vumbi. Hata kama ulikuwa na gari yako ya maana umetoka nayo huku ukifika pale inaingia kwenye vumbi. Kwa hiyo, ninataka niwaombe Waziri wa Mipango na Fedha, wala msije mkadhani mtaonekana kwamba mmependelea Mkoa wa Singida. Hizo ni barabara ambazo nchi nzima wanazitumia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara inayotoka Iguguno ikaenda Simiyu, barabara kama hiyo inaleta pamba kutokea huko Mkoa wa Mara, inapita Singida inakwenda inapeleka Dar es Salaam, inatoa materials Dar es Salaam inapeleka huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana hata barabara ya katikati ya nchi, ya Mwanza mpaka Dar es Salaam imelemewa inaharibika kila wakati kwa sababu imekuwa congested. Magari yote yanafuata pale lakini hizi barabara tukishaziwekea lami ina maana mtawanyiko. Mtu anayekwenda Musoma hatahangaika kwenda Shinyanga akakatize mpaka Mwanza, akifika Singida anapita Simiyu anakwenda anamaliza. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anayetaka kwenda upande huu anapita, kuna barabara nyingi.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hizi barabara za katikati tunaomba ziwekwe lami. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni barabara za kimkakati ambazo zinatumika na nchi nzima. (Makofi)
MWENYEKITI: Taarifa; samahani Mheshimiwa Isack. Taarifa Mheshimiwa Massay.
TAARIFA
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Mheshimiwa Francis Isack anachangia vizuri sana na kwa sababu ni jirani yangu, ninataka nimkumbushe na hii barabara inayotoka kwake pale kuja Mtinko na kwenda mpaka Hydom na hiyo ndiyo barabara inayoenda Simiyu na hata hii aikumbuke kwa sababu wapigakura wake na ndiyo barabara kubwa tunayoipitia, ahsante. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Isack unaipokea Taarifa?
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea. Nimesema barabara za katikati ya nchi, hata Dodoma nimeitaja, ni barabara za kimkakati. Kwa sababu huwezi kuruka, yaani wewe kama unataka kwenda huko huruki hapa, lazima utapita kwenye vumbi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge wote, wote lazima mzitetee barabara za katikati ya nchi. Ni eneo liko located strategically yaani hapa sisi tuna bahati kuwa hapo kwa sababu lazima upite. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri mwenyewe wa Ujenzi anapotaka kwenda jimboni haruki, akitoka Dar es Salaam lazima apite kwenye vumbi hilo. Kwa hiyo, mimi ninataka tu niseme, hizi barabara za katikati ya nchi ambazo ziko chini ya TANROADS, zinatakiwa ziwekewe lami ili tuiunge nchi nzima kwa lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haipendezi kuwa umevaa suti, chini unavaa kaptula yaani unatoka na barabara ya lami unafika hapo unakutana na vumbi. Halafu unaharibuharibu gari yako baadaye ndiyo unakuta lami tena mbele. Hii inatuharibia muunganiko wa kinchi. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Waziri wa Fedha toa fedha, Waziri wa Mipango weka mipango ili hizi barabara za katikati nchi iweze kupitika yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nihame hapo niende kwenye suala la maji. Katika nchi yoyote duniani ambayo itahesabika inawatunza watu wake vizuri ni ile inayowapa maji kwa sababu maji ni uhai, maji safi ni kila kitu. Hata kiwanda hakiendeshwi bila maji, gari huendeshi bila maji. Ikiwa tu haina maji injini ina-knock. Sasa, sembuse itakuwa watu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Mipango, Profesa, ulipokuwa Katibu Mkuu wa Wizara wa Maji pamoja na Waziri wako wa wakati huo, mlikuwa mna mpango mzuri sana wa kutoa maji Ziwa Victoria kuyaleta mpaka Dodoma. Sasa, leo umeingizwa jikoni kwenye mipango ya nchi, hiyo ilikuwa ni mipango yako ya Wizara ya Maji na Waziri wako, lakini sasa umeingizwa kwenye Wizara ambayo unapanga mipango ya nchi. Ninakuomba uufufue huu mpango ndugu yangu, utakuwa umetibu kidonda cha nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji kutoka Ziwa Victoria ni chanzo cha maisha ya milele. Sisi tutakufa tutakiacha. Maji, lile ziwa Mungu amelipa uwezo. Mto Nile unamwaga maji kwa wingi, kila siku tangu dunia iumbwe lakini lile ziwa halijawahi kupungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ule mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kuja Dodoma ulikuwa unapitia pale Sibiti unakuja mpaka Dodoma. Tena vizuri zaidi ule mradi kule kote utatumia pampu lakini ukishafika Mkoa wa Singida ukaingilia Sibiti, unakwenda Kijiji kinaitwa Kisana kiko pale jimbo la Mheshimiwa Dkt. Mwigulu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokea pale Kisana-Singida mpaka Dodoma maji yanakuja kwa gravity. Kwa hiyo, yatakuwa hayana tena hata gharama kubwa. Sasa mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri wa Mipango na Fedha, vijana wetu; hebu ufufue huo mpango halafu mpasie jirani yako hapo amwage fedha ili Watanzania wapone maji yafike Dodoma. Sasa wakati yanakuja Dodoma yatapita kwenye jimbo langu na mimi nitaogelea maji, tena haya yatatumika hata kwenye umwagiliaji. Kwa hiyo, nikuombe sana hili suala la mpango wa maji usije ukaliacha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, nije kwenye suala la bomba la gesi, nilishawahi kuchangia hapa. Hili bomba liko Dar es Salaam, bomba hili tunalihitaji liende mpaka Mwanza, liende Arusha, liende Mbeya ili tutumie gesi hii kwenye nyumba zetu kama tunavyotumia maji. Mungu ametujalia kuwa na gesi. Tumeshaitoa chini tumeifikisha Dar es Salaam, sijaiona kwenye mpango, huu mradi wa bomba. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri wa Mipango pamoja na Fedha, hebu wekeni hii mipango na fedha zitoke bomba hili litembee nchi nzima. Kama tulivyoweka Mkongo wa Taifa, leo tunatesa na internet mpaka vijijini watu wanaangalia internet. Ni kwa sababu mkongo umesambaa nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili bomba lisambae nchi nzima Tanzania ili tutumie hii gesi vizuri. Tena kuna wazo hili la kupeleka gesi kule Kenya, achaneni kabisa na hili wazo. Wale jamaa watachukua hii gesi wataanza kutuuzia by-products za gesi. Ile gesi by-products zake ni nyingi; chupa za plastiki, vizibo kwenye containers za maziwa na nini. Hebu hii gesi isambae hapa hapa nchini. Sisi bado tuna uwezo wa kuitumia hii gesi ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba sana; hata hizi Mheshimiwa Waziri wa Fedha, mimi ningeomba kabisa hizi kodi za vifaa hivi vya kubadilisha magari ili yatumie gesi, hivi mngevifikiria kuvifutia kodi kabisa ili magari mengi yabadilishwe yaweze kutumia gesi. Hata hii tozo hii, hiki chanzo mngekiweka kama cha akiba. Yaani mngefanya uchochezi kwanza mfute kodi za hivi vifaa, magari mengi yabadilishwe kuwa ya gesi, mwakani hivi, ninajua bado utakuwa Waziri wa Fedha Mama anakupenda na unafanya kazi vizuri ili sasa uje utumie hiki chanzo kitakapokuwa kina magari mengi zaidi lakini kwa sasa utakiwahisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wataacha kubadilisha magari. Wataona mmh, kumbe huku nako tozo imeshaingia. Acha tu sasa hivi, wewe acha hii tozo iweke akiba, futa kodi kwenye hivi vifaa ili vituo vya kujazia gesi viwe vingi.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa kidogo, Taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa.
TAARIFA
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kutoa taarifa. Kama nchi tunahitaji sana kodi ndiyo maana rafiki yangu analalamika kwake hakuna maji na kwangu na mimi ninahitaji hiyo tozo nipate kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi ni kwamba, unajua ile bei ya gesi imeshuka sana? Kwa hiyo, kiwango kinachoongezeka hakiwezi kuathiri chochote. Kwa hiyo, tusiliweke kama jambo kubwa. Nchi inahitaji kodi na tunahitaji kufanya maendeleo, ahsante sana.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Francis Isack, unapokea taarifa ya Mheshimiwa Kiswaga?
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii taarifa ya Mheshimiwa mimi siipokei kwa sababu, magari ya gesi bado ni machache sana. Tunataka magari mengi yabadilishwe, halafu hiki chanzo tuje tukitumie vizuri wakati magari mengi na kituo chenyewe cha kujaza gesi Dodoma bado hakuna. Bado kiko Dar, leo tunakimbilia kuweka tozo, magari mangapi hayo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ndiyo maana ninasema hivi, kodi zifutwe za vifaa vya kubadilisha ili magari mengi yabadilishwe halafu kituo kianzishwe hapa Dodoma na mikoa mingine, magari yawe mengi halafu hiki chanzo tutakitumbukiza tu. Sasa hivi haraka haraka watu wataacha kuagiza hata hayo magari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimalizie harakaharaka tu kwa sababu mimi ni kitinda mimba.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa ninaomba uhitimishe, muda wako umeisha.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nihitimishe tu kwa kusema, Waheshimiwa Wabunge, ule Muswada wa kuja, ile Finance Bill kuhusu kupitisha suala la sukari, NFRA kununua ni jambo zuri sana na niliwahi kuchangia hapa. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa, Mheshimiwa muda wako umeisha kabisa tafadhali.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba jambo hilo tulipitishe ili tuwasaidie wananchi wa Tanzania. Hili ndiyo zao lao la maskini ambalo kila maskini lazima anywe chai na uji wenye sukari. Kwa hiyo, niwaombe sana hili tulipitishe kwa nguvu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)