Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibiti
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuwa mchangiaji wa kwanza katika bajeti hii muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kabla sijaanza kuchangia bajeti hii nichukue nafasi kuwapa pole Wananchi wangu wa Jimbo la Kibiti na wale wajomba zangu wa Rufiji kwa kadhia ya mafuriko ambayo imetukuta. Pia naomba niwaambie tu wananchi hawa wawe na subira kwani inna-llaha kana `aliiman hakiima (hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na yeye ndio mwenye hekima). Kwa hiyo, niwaombe wananchi wawe na subira, Serikali ipo kazini na inaendelea kuwashughulikia wananchi hawa ambao wamepatwa na mafuriko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaendelea kuifanya ndani ya nchi hii. Vilevile, kwa kazi ambayo anaendelea kuifanya katika sekta hii. Mheshimiwa Rais amefanya mabadiliko makubwa sana, tunaona uwekezaji wa hali ya juu sana ambao umeendelea na unaendelea kufanyika. Mfano mzuri upo kwa ndugu yangu, Mheshimiwa Kassinge kule Kilwa. Hivi sasa ninavyozungumza inaenda kujengwa bandari nzuri sana ya uvuvi ambayo inakwenda kuwa bandari ya kihistoria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila katika Quran pale, kuna aya inasema kwamba; “Innallah yarzuqu man yashaau bighairi hisaab” (Mwenyezi Mungu anamruzuku mambo binadamu bila hesabu yoyote). Mambo haya ameruzukiwa mdogo wangu Mheshimiwa Abdallah Hamis Ulega. Mheshimiwa Ulega ni mbunifu, mchapakazi na anataka matokeo. Haya ni mambo ambayo Mwenyezi mungu amemruzuku. Ndugu yangu hongera sana na naimani sana kwamba wewe ni institutional memory katika sekta hii na unakwenda kufanya mabadiliko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaendelea kuifanya na kumsaidia ndugu yangu Mheshimiwa Abdallah Hamis Ulega. Mheshimiwa Ulega naomba tu nikwambie unatuheshimisha Kaka zako wa Pwani, fanya kazi sisi tuko very much proud of you. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo mawili tu ya kuchangia katika bajeti hii. Jambo la kwanza linahusiana na masuala mazima ya uwezeshwaji wa vijana katika suala zima la mambo ya kiuchumi hasa katika kuweza kupewa boti. Ndugu yangu, Mheshimiwa Ulega kazi kubwa unaifanya na mimi sina shida wataalamu wako wanakusaidia ipasavyo. Katika mambo ya kutoa boti kwa vijana, Mheshimiwa Ulega mimi nikuombe tu, pale kwa kaka yako Kibiti kuna Kata ya Salale, Kiongoroni, Mbuchi, Msala. Maeneo haya pamoja na Kata ya Mtunda kule chini, haya ni maeneo ya delta na wewe unajua sisi tumeathirika kikubwa sana na mambo haya ya mafuriko. Vijana wale hivi sasa mazingira ya kimaisha siyo rafiki. Maeneo yetu ya kilimo wewe mwenyewe unayajua. Kwa hiyo, mimi nikuombe sana tengeneza mpango uliokuwa na uhalisia huku ukiwa unajua kabisa kwamba, kuna wajomba na kaka zako katika Jimbo la Kibiti na pale Rufiji ambao tumeathirika kwa kiasi kikubwa sana na mambo haya ya mafuriko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, wakati anakuja ku-wind up hapa utoe tamko maana kuna wababaishaji wanapita pita kule Rufiji na Kibiti, wananza kuwaambia watu sijui wekeni vikundi, changieni hela zinakuja boti, Mheshimiwa Waziri hiki kitu hakikubaliki. Nikuombe sana waambie wananchi wajue kwamba, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan yuko kazini lengo lake ni kuwawezesha wananchi kiuchumi hasa hawa vijana. Kama kuna agent mmewaweka huko chini basi mtuambie sisi Wabunge. Mimi ninavyojua sisi tuna vikundi viko tayari. Mheshimiwa Waziri mimi nilishakukabidhi na vijana hawa wanasubiri tu kauli yako useme Kibiti kuna mgao gani? Rufiji kuna mgao gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anisamehe sana nikiwa naitajataja Rufiji wala usishangae, maana sisi Kibiti tumejaziwa ndani ya Rufiji. Rufiji ndiyo baba yetu. Kwa hiyo, sasa nikiizungumzia tu Kibiti peke yangu wale wajomba zangu wa pale Rufiji nikirudi inaweza ikaja ikawa mtihani. Mimi kuweza kutafuta kamba lazima niende Muhoro halafu ndiyo nirudi Kibiti. Kwa hiyo, hili nilikuwa nakuomba sana uweze kulitolea tamko ili sasa tuweze kuona ni jinsi gani vijana hawa wanakwenda kunufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo nililokuwa nataka nilichangie ni eneo zima linalohusiana na sekta nzima ya mambo ya mifugo. Mheshimiwa Waziri wewe unajua sisi ni wahanga namba moja, maeneo haya ya Pwani ya Kusini yote ukianzia Mkuranga ukienda Kibiti, Rufiji, Kilwa, Lindi na kwa Wamakonde kule wewe unafahamu. Sisi ni waathirika wa hali ya juu sana katika suala zima la mambo ya mifugo. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri wakati muafaka sasa umefika wa kuweza kuharakisha sera mpya ya mambo ya mifugo, ili sasa tuweze kuona ni jinsi gani tunakwenda kuwa na mifugo ambayo inakwenda kuwa ni mifugo ya biashara. Ni jinsi gani tunakwenda kutenga maeneo ambayo yanakuwa maeneo sahihi kwa ajili ya mifugo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anajua katika maeneo ya kwetu kule unaamka asubuhi unakutana na ng’ombe 150 na ametoka kuzungumza hapa Mheshimiwa Getere jana, kama sijakosea juzi. Alizungumza hapa kwamba, kule kwake kuna watu wanachomwa mikuki. Mimi nataka niseme tu hao wenzetu wafugaji wote ni Watanzania lakini wenzetu ni wakali sana. Sisi Watu wa Pwani ni waraimu sana, Mheshimiwa Ulega wewe unajua ndugu zetu wako ndani wana ulemavu wa hali ya juu, wengine wamepoteza maisha kutokana na mambo haya kati ya wakulima pamoja na wafugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri na najua nimetoka kusema hapa; “Innallah yarzuqu man yashao bighairi hisab” (Mwenyezi Mungu anamruzuku mwanadamu mambo bila hesabu). Najua katika mambo ambayo Mwenyezi Mungu amekuruzuku wewe ni game changer, unakwenda kufanya mabadiliko katika Wizara hii. Lete ile sera sasa tuweze kuhakikisha tunakwenda kutunga sheria. Haiwezekani tukawa na mifugo holela holela tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nina wakulima pale nyumbani kwangu katika Kata ya Maparoni, hivi ninavyozungumza kuna mifugo ya ng’ombe takribani 1,250. Ile Maparoni ni ndogo na vile ni visiwa na ninyi mnajua taratibu za visiwa jinsi zilivyo, mifugo hairuhusiwi kwenda kule. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri pamoja na wataalamu wako harakisheni leteni sera mpya ili sasa iweze kutusaidia tuweze kuwa na mifugo yenye tija kama vile Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anavyokusudia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho kwa sisi wanasiasa. Mheshimiwa Waziri, natamani sana kuona eneo hili ambalo Mheshimiwa Rais amewekeza fedha nyingi sana na anaendelea kuwekeza, basi sasa liweze kuchangia ipasavyo katika GDP (pato letu la Taifa). Umetoka kuzungumza katika hotuba yako kuna 1.8% lakini katika miaka miwili au mitatu iliyopita tulikuwa tumekwenda juu zaidi. Kwa hiyo, hapa tafsiri yake ni nini? Tunakimbia mbele katika speed ya kurudi nyuma. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri na wewe mdogo wangu mimi nakujua shughuli yenyewe unaiweza pamoja na wataalamu wako. Kwa hiyo, nikuombe sana kaa kitako na wataalamu wako tunataka kuona sasa hii sekta nzima ya mambo ya mifugo inakwenda kuchangia katika Pato la Taifa na tukifanya hivyo tutakuwa tumemuenzi Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa fedha nyingi na jitihada ambazo anaziingiza katika sekta hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nikushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)