Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi ya kuchangia kwa dakika hizo ulizonipatia.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na suala la upumzishaji wa Ziwa au ufungaji wa Ziwa Tanganyika. Ziwa Tanganyika kwenye mikoa hii mitatu, Mkoa wa Rukwa, Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Kigoma ndiyo shamba letu, ndiyo duka letu, ndiyo maisha yetu. Kwa kuwa shughuli hii ni shughuli halali, mwaka jana tulimshauri Waziri hapa, tulimshauri kwamba jambo hili halikuwa shirikishi. Tunashukuru amechukua hatua ya kwanza kwa kutushirikisha sisi Wabunge, tulikaa naye, pamoja na kushirikisha Wabunge, tulitaka awashirikishe wavuvi, jambo hilo halijafanyika kikamilifu. Tunajua umefanya kwa baadhi ya maeneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema nini? Kwa nini tunataka kufunga Ziwa leo? Mheshimiwa Waziri tumefikaje hapa? Kwa sababu Serikali ilikuwepo miaka yote, ni kweli kwamba Ziwa Tanganyika huwa linajifunga lenyewe na majibu mliyotupatia wakati umekutana na sisi Wabunge ulituambia samaki wamepungua, swali ni kwamba kwa nini wamepungua? Kwa sababu miongoni mwa majukumu yako kama Wizara ni kuendeleza uvuvi pamoja na ufugaji. Sasa, samaki wamepungu na Wizara ipo! Ninaomba nishauri mambo machache. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mkataba huo umeusoma hapa, kwa namna ulivyousoma unaanza kutekelezwa kesho tarehe 15, ndiyo mnaanza kutekeleza hilo jambo, wakati mnakwenda kutekeleza, mbadala wa hicho kipindi ambacho wanafunga Ziwa, umezungumza hapa mmetoa vizimba 29 ambavyo bado havijaanza kufanya kazi, huo ndiyo mbadala kwa kipindi ambacho mmefunga Ziwa, sasa hao samaki wana-mature baada ya muda gani? Ninataka kuzungumza nini Mheshimiwa Waziri? Yawezekana hiki unachokifanya leo ilitakiwa kianze kufanyika mwaka jana kwa ajili ya maandalizi kama mbadala kabla hatujafunga Ziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri jambo la kwanza ni lazima tutafute suluhisho la uvuvi halamu ndiyo chanzo cha samaki kupungua, kufunga Ziwa kwa miezi mitatu siyo suluhisho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba Ofisi ya Rais mnaohusika na mazingira, ni vizuri pamoja na kwamba mkataba huu tumesaini zaidi ya nchi moja, hili jambo linahusu Watanzania, kama linawahusu Watanzania lazima tuwashirikishe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka leo nazungumza hao wavuvi bado wanakata leseni, hawakati leseni kwa ajili ya kuuza maandazi, wanakata leseni kwa ajili ya uvuvi. Sasa, kama tunaenda kufunga na hao watu wanakata leseni, naomba Waziri ukija hapa utuambie mmetenga kiasi gani kwa ajili ya kuwapa hawa wavuvi ambao wamekata leseni na hii ni shughuli halali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, naomba ukija hapa utueleze mmetenga kiasi gani kwa Watanzania ambao maisha yetu ndiyo uvuvi kwa kipindi cha mpito? Kwa sababu kuzaliwa karibu na Ziwa Tanganyika siyo laana ni baraka! Msitufanye tuanze kulaumu kuzaliwa karibu na Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri alionekana akimpeleka Rais kuzindua vizimba Ziwa Victoria ni jambo jema sana, lakini kama Ziwa linalofungwa leo ni Ziwa Tanganyika why alianza kupeleka Ziwa Victoria? Huoni kama unakwenda kuwachanganya hawa Watanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya mambo hayastahili hata kidogo. Ukiangalia hapa, tunasema hivyo vizimba, utekelezaji wa maduhuli katika malengo mliyokuwa mmejiwekea ni 42% tu mpaka sasa hivi lakini fedha za maendeleo ni 41%. Hii ni sekta ya uzalishaji tunayoitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo uvuvi ni utajiri, ufugaji ni utajiri. Msifanye hao watu waanze kuona kama hili jambo siyo halali kwao, lazima tuanze kufikiri upya. Jambo la vizimba ninarudia tena, Ziwa Tanganyika lipewe kipaumbele. Mtaenda kufunga kwa sababu ya wingi wa maamuzi ambao tutafanya kwa watu lakini mimi ninasema, hata kama kulikuwa na nia njema, tutafute suluhisho la uvuvi haramu siyo kufunga Ziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, narudia kushauri, kama Kata ina vijiji vinne, tusiende kufunga Kata nzima. Mnaweza mkafunga vijiji viwili, vijiji viwili mkaacha. Mshehimiwa Waziri ukija hapa utueleze, kwa kipindi hiki ambacho mnaenda kufunga, wale watu ambao wanafanya uvuvi wa ndoano kwa ajili ya kitoweo utaratibu gani utatumika wakati haya maisha mengine yanaendelea? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo machache ya kushauri. Jambo la kwanza, mnapowaambia wakope hivi vizimba, kuna kuandika maandiko, mmetoa elimu kiasi gani kwa hawa wavuvi? Kuandika hayo maandiko ni gharama. Huyu mvuvi wa kawaida anaweza wapi kutoa shilingi laki nne, shilingi laki tatu, shilingi laki mbili? Haiwezekani! Tumeamua kwamba huu ndiyo mbadala, nendeni mkatengeneze mazingira rafiki kwa hao wavuvi. Kwa sababu ukiangalia, ni kwa nini wako 29? Kwa mujibu wa taarifa yako Mheshimiwa Naibu Waziri ukiwa Sumbawanga ulisema utatoa vizimba 800 lakini leo unazungumzia 29, halafu tunakwenda kufunga Ziwa kesho! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi hata kama nia ni njema kweli, kama hivyo vizimba vimetolewa jana au juzi, Ziwa linafungwa kesho, hao Samaki wata-mature lini? Tunakwenda kutengeneza nadharia, jambo ambalo haliwezekani kutekelezeka. Hatutaki kuzalisha vibaka mtaani, hii ni kazi halali ya Watanzania. Sisi ambao tunaamini Ziwa Tanganyika ndiyo shamba letu na ni duka letu, tumeandaa utaratibu gani kwenye kipindi hiki cha mpito? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na nia njema ninarudia, tusije na majibu mepesi kwenye mambo magumu. Uvuvi haramu upo, hakuna mtu anakataa. Samaki wamepungua ni kweli, nani ametufikisha hapa? Serikali ilikuwa likizo? Ilikuwepo. Kwa nini leo tuwape adhabu hawa Watanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachosema, approach ambayo inatumika sasa hivi ndiyo ambayo sikubaliani nayo, yawezekana nia ni njema tupate samaki wengi lakini kupata samaki wengi siyo kufunga Ziwa kwa miezi mitatu. Tuandae operation maalumu ya kupambana na uvuvi haramu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye utitiri wa kodi, utitiri wa kodi, leo kile chombo ambacho mvuvi anatumia mnasema akilipie leseni. Mmiliki dola 55 chombo chenyewe wanakilipia dola 50, halafu na wavuvi wanaokwenda kuvua na wao wanalipia leseni. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Aida muda wako umekwisha.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hili suala la tozo libaki kwa mtu mmoja ambaye ni mmiliki, chombo hakiwezi kujiendesha.

NAIBU SPIKA: Mengine mwandikie Waziri kwa maandishi.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)