Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kusimama tena mara nyingine ndani ya Bunge, kuchangia Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. Wiki mbili au tatu zilizopita tulipata ridhaa ya kumwona Mheshimiwa Waziri Mkuu akikabidhi boti ya doria baharini kwa ajili ya kulinda usalama na maslahi ya wavuvi maeneo ya baharini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kupitia boti hii nachukua nafasi ya kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutafuta fedha kwa ajili ya kuendelea kuwalinda na kuimarisha ulinzi kwenye maeneo ya baharini hasa kwa wavuvi wetu ambao wamekuwa wakihangaika kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwendelezo huo, nachukua nafasi kukuomba sana Mheshimiwa Waziri na nimekuwa nikisema sana ndani ya Bunge, kwa kuwa tayari angalau tumelifanya hili baharini, tufikishie salamu kwa Mheshimiwa Rais na wewe Mheshimiwa Waziri ulione hili namna ambavyo wavuvi wa Mkoa wa Mara ambavyo wamekuwa wakiteseka na kudhulumiwa haki zao maeneo ya ziwani na wanapigwa na wenzetu, kimsingi usalama wao haupo vizuri sana. (Makofi)

Mheshimwia Naibu Spika, kwa kuwa limeanza maeneo ya baharini Mheshimiwa Waziri libebe hili pia lifanyike maeneo ya maziwa ili kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama kwa wavuvi wetu. Ninafikiri utakumbuka siyo mara ya kwanza kulizungumzia hili, ni changamoto kubwa sana kwa wavuvi maeneo ya Ziwa, niliwahi kukuambia kuna wengine wamefilisika wameacha kazi hizi za uvuvi kwa sababu usalama wao ndani ya Ziwa hauko stable, kwa hiyo, nachukua fursa hii kukuomba sana Mheshimiwa Waziri kama tulivyofanya maeneo ya bahari tuone namna tunavyoweza kulifanya kwa Mkoa wa Mara na Kanda ya Ziwa kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo kwa sababu dakika ni chache, nitajikita sana kwenye Jimbo langu. Jambo la kwanza ni Chuo cha Gabimori. Mheshimiwa Waziri hiki chuo kwa bahati nzuri nimeona kwenye hotuba yako nimesoma yote sijaona ukikizungumzia mahali popote. Wewe ni shahidi chuo hiki tumekuwa tukikiomba zaidi ya miaka 10, wananchi matumaini yao ni makubwa sana hasa vijana ambao wanahitimu kidato cha nne, matarajio yao ni kwamba chuo hiki kiweze kuimarika waweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tazama kwa miaka 10 tunakiimba chuo hiki na hakifanyi kazi, ninakuomba utakaposimama leo jioni, kwa kuwa kwenye hotuba yao hujakizungumza, basi ukitolee majibu ili wananchi kule ndani ya Jimbo la Rorya na Mkoa wa Mara kwa ujumla wake waweze kujua nini hatma ya chuo hiki ambacho tumekiomba zaidi ya miaka 10. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni soko. Mheshimiwa Waziri nimekuwa nikikuomba sana masoko ya samaki na masoko ya dagaa. Mheshimiwa Waziri umesema sekta hizi ni sekta za uzalishaji lakini kimsingi Mheshimiwa Waziri nimekuwa nikikuambia sana, tuzungumze wewe pamoja na Mawaziri wa TAMISEMI tuone namna ya kuisaidia Wilaya ya Rorya kwa kutengeneza masoko mawili makubwa, Soko la Samaki na Soko la Dagaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunavua lakini hatuna soko la uhakika la kuuza bidhaa zetu. Kama unavyojua, uchumi wa Jimbo la Rorya ukiacha kilimo, shughuli kubwa inayofuata ni uvuvi lakini hatuna soko la uhakika. Mvuvi anavua Rorya anapeleka kuuza bidhaa zake Mwanza, anapeleka kuuza bidhaa zake Kenya. Mheshimiwa Waziri lione hili. Tunataka na sisi tupate masoko nasi watu wa Kenya na hao tunaowafuata Mwanza waje kununua mahitaji yetu ndani ya Jimbo letu la Rorya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni vizimba. Ninachukua nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais na wewe mwenyewe kwa vizimba ulivyokabidhi Mwanza, mimi ndani ya Jimbo langu la Rorya wavuvi wangu wamepata vizimba vitatu pamoja na boti tatu, tupelekee salamu, tunashukuru sana kwa kazi hii nzuri na uendelee kumwomba tena Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa sisi shughuli yetu ya uchumi ni uvuvi, tunaomba tupate vizimba vingine na nimekuletea vikundi 15 Mheshimiwa Waziri, ninaomba hivi vikundi 15 uwape vizimba wafanye shughuli ya uvuvi iliyo salama ili angalau na wao waweze kujikwamua kenye uchumi wao. (Makofi)

Mhhesimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la majosho. Mheshimiwa Waziri kama unakumbuka toka ukiwa Naibu Waziri nimekuwa nikikufuata sana kuomba majosho na ulinikabidhi kwa mtu mmoja pale Wizarani, ninafikiri anaitwa Ndugu Rutega, toka mwaka 2022 ninakuomba majosho, ninakuomba sasa na hii iwe awamu ya mwisho, josho moja ni shilingi milioni 20 mpaka shilingi milioni 25, siwezi nikawa ninakufuata kila siku kwa miaka mitano kuomba shilingi milioni 25 peke yake kujenga hata josho moja. Mheshimiwa Waziri ninakuomba sana, kwenye bajeti yako na utakaposimama hapa jioni uwaambie wananchi wa Rorya toka mwaka 2021 ukiwa Naibu Waziri, leo wewe ni Waziri, tunapata lini majosho kwa ajili ya kuboresha na kusaidia wafugaji wetu wanaofanya shughuli hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo limekuwa likiendelea ni namna ambavyo, kama ukifuatilia sasa hivi Mheshimiwa Waziri, soko la dagaa kwa sasa hivi, dagaa zimepanda bei, wanaoumia sana ni hawa wananchi wa kawaida kabisa ambao wengine tunatoka nao vijijini, kwa namna ambavyo wanapata yale mahitaji. Mwingine hana uwezo wa kununua nyama, kwa hiyo, chakula chake cha kila siku kwa mwananchi wa kawaida ni dagaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukifuatilia Kanda ya Ziwa Mheshimiwa Waziri, bei ya dagaa sasa imepanda, kidumu alichokuwa ananunua shilingi 5,000 sasa hivi ni shilingi 10,000 mpaka shilingi 15,000, maana yake bei imepanda. Wale wananchi wa kawaida wanashindwa kumudu gharama za maisha. Mheshimiwa Waziri nini kimetokea? Ni kwa sababu tumeruhusu wenzetu kutoka nchi jirani kwa maana ya Congo na Uganda kuja kuingia mpaka kwenye Visiwa huko wanakofanya wavuvi kwenda kununua wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwanzoni walikuwa wananunua wazawa, wanaleta sokoni, hawa watu wageni walikuwa wananunua kupitia masoko ya kawaida, lakini leo wanafuata kulekule ziwani wananunua na wakinunua wananunua kwa bei kubwa. Wakinunua kwa bei kubwa maana yake mlanguzi anaponunua kule anapoleta kwenye masoko ya kawaida, leo ukienda CCM Kirumba Mwanza na maeneo mengine, bei imepanda zaidi ya mara mbili, imepandishwa na nini, kwa sababu ya bei hizi za wenzetu wanaofuata kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukitengeneza utaratibu kama alivyotengeneza Waziri wa Kilimo hapa, kwamba wale wageni wasiende kule inakovunwa penyewe kwa maana ya visiwani, wasubiri kwenye masoko wanunue kule bidhaa ili angalau bei iwe linganifu lakini tutawalinda pia wanunuzi wa ndani pamoja na walaji ambao ni wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)