Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na mimi nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunipa afya njema na kusimama hapa leo kuchangia katika Wizara yetu hii ya Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuipongeza Wizara, Kaka yangu Mheshimiwa Ulega na Naibu Waziri wake na wataalamu wote wa Wizara, kwa kwa kweli mnafanya kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia alitupatia matumaini sana wavuvi pale alipofanya tukio la kihistoria, tukio ambalo halijawahi kutokea tangu tupate uhuru. Alikabidhi boti zaidi ya 160 na vizimba zaidi ya 120 katika Ziwa Victoria. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa juhudi hizi, tunampongeza sana Mheshimiwa Samia na tunaona kazi yake njema inavyofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wavuvi tulitarajia baada ya matumaini kutoka kwa Mheshimiwa Rais kwa kuwekeza katika Ziwa Victoria tulitamani kuona uwekezaji ule unahamia katika Ziwa Tanganyika, hayo ndiyo yalikuwa matumaini yetu Mheshimiwa Waziri, lakini kwa masikitiko makubwa sana, tunaona juhudi katika Ziwa Tanganyika bado haziridhishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, ukienda kwa wavuvi changamoto yao kubwa ni tozo, tozo, tozo, tozo. Mheshimiwa Rais, ukimsikiliza dhamira yake kubwa ni kuhakikisha uwekezaji unafanyika, kutengeneza mazingira wezeshi na mazingira rafiki kwa wawekezaji wetu katika sekta mbalimbali. Leo katika Sekta ya Uvuvi uwekezaji wake umekuwa ni mgumu, ni mgumu na ni mgumu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu mbili. Sababu ya kwanza, leo hii nikitaka kuwekeza katika Sekta ya Uvuvi, kwanza kabla sijafanya chochote nitaenda TASAC. Nikiwa TASAC kule watachukua pesa yao, nikitoka hapo lazima mimi kama mnunuzi wa boti nitakata leseni yangu mimi kama mnunuzi wa boti. Nikitoka hapo nitakata leseni nyingine kwa ajili ya boti lakini boti hiyo moja haiwezi kwenda kuvua ikiwa peke yake, lazima inahitaji supporting boat ndogo ndogo na zile boti ndogo ndogo pia na zenyewe zote zikiwa tatu, zikiwa nne, zikiwa mbili zote nitazikatia leseni, hii siyo sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yaani katika kazi moja unakuwa na leseni zaidi ya tano, hii haiwezekani Mheshimiwa Waziri, hii siyo sawa. Leo hii mimi nikitaka kuwekeza kwenye Sekta hii lazima nitakuwa na dola 55 kwa ajili ya boti lakini nitalipa dola 50 kwa ajili yangu mimi mnunuzi wa boti, hata kama siendi kuvua lakini pia mvuvi lazima awe na leseni, hii siyo sawa Mheshimiwa Waziri. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, ukae na timu yako kama ilivyo kwa wamiliki wa magari, akishakuwa na leseni ya chombo hatuoni umuhimu wa kuwa na leseni ya mmiliki na kama ni hivyo inahitajika sana basi zijumlishwe kwa pamoja. Hii kwetu wavuvi ni kero na inatukwamisha sana, sana, sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri, ninapotaka kwenda kuvua wewe unafahamu, wewe umesema wewe ni mvuvi unafahamu ile boti moja haiwezi kwenda kuvua ikiwa pekeyake lazima kuwe na boti hizi saidizi, kuna haja gani hizi boti saidizi kuwa na leseni zake kwa kazi ile ile moja? Haiwezekani Mheshimiwa Naibu Waziri. Ninaomba utakapokuja kufanya majumuisho utueleze; ni kwa nini wamiliki wa magari wana leseni moja, wamiliki wa boti tuna leseni zaidi ya nne? Hilo ni jambo moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo ningependa kulizungumza, tumeona maziwa mbalimbali yanaelezwa. Nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri na Wizara yako; hivi mnafahamu kama kuna uwepo wa Ziwa Rukwa? Hatuoni Ziwa Rukwa likizungumziwa popote lakini Ziwa Rukwa lile lipo linafanya kazi lakini hatuoni uwekezaji wa Serikali katika Ziwa Rukwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatusikii habari za vizimba Ziwa Rukwa, hatusikii habari za mialo Ziwa Rukwa, nini changamoto hasa Mheshimiwa Waziri? Kama hatufahamu kwamba kuna uwepo wa Ziwa Rukwa basi tuwaeleze wananchi kwamba Wizara haifahamu uwepo wa Ziwa Rukwa tujue. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, inasikitisha sana kuona Ziwa lipo lakini hakuna uwekezaji wowote uliofanyika katika Ziwa Rukwa. Mheshimiwa Naibu Waziri kama itakupendeza tunaomba tupate mialo katika Kata ya Nankanga kama itakupendeza. Pia, katika Ziwa Rukwa pale Muze tunaomba tupate mialo pale. Tunatamani kuona wavuvi pia wa Ziwa Rukwa na wenyewe wanaangaliwa kama wavuvi wengine wa maziwa mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia tumeona hapa wavuvi wa Kigoma, Rukwa na Katavi tumepokea hizo vizimba 29. Kwa takwimu na uhalisia wa mikoa hii mitatu kwa idadi ya wavuvi waliopo bado tunaona vizimba hivi 29 havitoshi Mheshimiwa. Hata kama unasema kwamba hao ndiyo waliojitokeza, imani yetu ni kwamba wananchi bado hawana elimu ya kutosha kuhusu upatikanaji wa hivyo vizimba. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, tuongeze elimu. Pia, tuongeze ushirikishwaji wa wananchi ili waelewe vizimba hivi vinapatikana kwa namna gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu wananchi wanapiga simu, wanashangaa kuona Serikali inasema walioomba ni wachache vizimba vipo lakini wao wenye uhitaji bado wanaona hawawezi kuvipata. Kwa hiyo nikuombe Mheshimiwa Waziri pamoja na timu nzima ya Wizara tutoke ofisini twende kwa wananchi wavuvi tuwafikie waelewe, waelimishwe namna gani vizimba hivi vinapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, unapomwambia mwananchi wa kawaida aanze kuandika maandiko, wengi huwa wanahisi ni jambo kubwa sana. Kwa hiyo turahisishe mambo, kama itawezekana watumie hata fomu. Kwani kuna haja gani ya kuwa na maandiko kama kweli ni mvuvi na anajulikana na uwezekano wa kutumia fomu uwepo? Turahisishe kazi, wavuvi hawa waombe vizimba kwa kutumia fomu, siyo lazima wawe na maandiko. Tunapoanza kusema maandiko ndiyo tunaongeza chain ya rushwa.... (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa...
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, tunaongeza chain ya usumbufu... (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda wako umekwisha, ahsante.
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na nakushukuru kwa nafasi. (Makofi)