Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa. Naomba na mimi pia nichukue fursa hii kutoa mchango wangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri lakini pia na kwa hotuba yake nzuri inayoonesha dira ya muelekeo mpya na mzuri wa Sekta yetu hii ya Mifugo na Uvuvi. Pia, nishukuru kwa upande wa Jimboni kwangu tuna shida kubwa ya watumishi wa Sekta hii ya Mifugo na Uvuvi. Tulipata watumishi 14 kwa ujumla wake lakini bado tunayo changamoto ya watumishi wengi wapatao 93, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri uendelee kututazama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepata pia vitendea kazi zikiwemo pikipiki nane lakini bado tuna upungufu wa pikipiki 17 kwa hiyo bado tunaendelea kukulilia utusaidie. Pia, huko nyuma tulikuwa tunapata hizi dawa za kuogeshea mifugo, kwa hiyo niendelee kuomba sasa hii huduma iendelee kupatikana kwa sababu mwaka huu hatujapata ile yenye ruzuku. Tunaomba Mheshimiwa Waziri uendelee kutuona katika Wilaya yetu tuendelee kupata dawa za kuogeshea mifugo katika majosho yetu kwa sababu mfugo unapokosa afya hata tija yake inakosekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikukumbushe ile ahadi ya majosho 10 ambayo Waziri alituahidi siku ile alivyofika kule kwenye Kijiji cha Mwinkulu, alipokuja kwenye ile timu ya Mawaziri Nane pamoja na hiko Kijiji chenyewe cha Mwinkulu. Alituahidi kwamba angetupatia majosho 10 lakini ile kazi bado haijafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mkubwa ningetaka kujikita kwenye maeneo makubwa kama mawili, matatu hapa. Eneo la kwanza ni kuhusu maeneo ya malisho. Nashukuru sana Wizara imejitahidi kutupa mbegu, imejitahidi sana kupeleka mbegu za malisho na kuleta mbegu mpya kwa ajili ya malisho ya mifugo. Hii ni hatua kubwa lakini bado kuna changamoto kubwa ya maeneo yenyewe ya malisho. Hapa nataka niishauri Serikali, Wizara ianzishe mashamba kwa ajili ya malisho ya mifugo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nirejee mchango wa Mheshimiwa Kunambi. Amechangia vizuri sana kwenye eneo la kuwekeza kwenye maeneo ya malisho. Malisho ya mifugo kwa sasa ni biashara, wafugaji wanahitaji malisho, wanahitaji majani lakini majani hayapatikani. Watu wengi wanaamini kwamba malisho ni ya Mungu, majani ni ya Mungu lakini majani yenyewe hayaonekani. Ndiyo maana unaona kila mahali sasa hivi kuna migogoro, utakuta migogoro ya wafugaji na wadau wengine wanaohitaji ardhi. Kwa hiyo kumekuwa na shida kubwa kwa sababu hatujawekeza ipasavyo kwenye eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza ukaangalia tu kwa tathmini ndogo au kitakwimu. Mkulima au mfugaji akitaka kupanda eka moja ya majani, yeye kazi yake kubwa pale ni kuwa na mbegu, kulima na kupanda. Mavuno yake mpaka mwisho atajikuta robota moja la majani ni shilingi 3,000. Sasa kwa mazingira kama hayo akitoa robota 300 tu anapata shilingi 900,000 lakini ukilima heka moja ya mahindi ukapata gunia 10, gunia moja ni shilingi 40,000, unapata shilingi 400,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, unaona kwamba ukilima majani faida yake ni mara mbili zaidi na yanahitajika yana wateja. Kwa hiyo natoa wito hapa kwa Serikali na sisi ambao ni wazalishaji wa majani tuwekeze kwenye eneo la mashamba ya malisho ya mifugo na hasa hapa Mheshimiwa Waziri kwa kuwa umeleta mbegu nyingi basi nikuombe uwekeze kwenye eneo la mashamba sasa. Tushushe chini kwenye wilaya zetu, kwenye ma-ranch ili wananchi wanaofuga waweze kupata hii huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, Kamati pia imeeleza kuhusu kuanzisha mamlaka kamili ya mifugo pamoja na mamlaka kamili ya...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Ighondo...
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, uvuvi kama unavyoona TRA...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ighondo, ahsante
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, TARURA, RUWASA na kadhalika na huku pia tuweke hili ili kuwe na tija kwenye ufuatiliaji na usimamizi wa Sekta hii ya mifugo. Nakushukuru kwa nafasi na naomba kuwasilisha, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)