Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nachingwea
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Tarehe 17 Septemba, 2023 Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alifanya ziara kwenye Jimbo langu la Nachingwea na katika changamoto ambazo alikutana nazo tulimlalamikia juu ya mgogoro wa wafugaji na wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mwezi mmoja ilikuja timu maalum ambayo imetusaidia kuondoa tatizo hilo, mgogoro huo wa wakulima na wafugaji. Nitumie nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Nachingwea kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi hiyo kubwa na nzuri ambayo ametufanyia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi pamoja na Naibu Waziri na timu yake kwa ujumla wake, wanafanya kazi kubwa na nzuri kweli kweli. Wakati wa mzozo huu, Mheshimiwa Waziri pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani walifanya ziara Nachingwea na kuchukua hatua ambazo walau ziliweza kutatua mgogoro huo kwa awali na baada ya hapo Mheshimiwa Rais alivyokuja akaendelea kuumaliza kabisa huo mzozo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mzozo huo wa wafugaji na wakulima pamoja nimeshukuru hapa kwa kazi kubwa na nzuri ambayo imefanywa na Serikali, bado imeacha makovu mengi kwenye jamii. Hapa wakati Mbunge mwenzetu anachangia alikuwa anashauri namna ambavyo wakulima wanaweza kupanda majani kwenye mashamba yao ili iwe kama sehemu ya wao pia kuwa na mahusiano mazuri na wafugaji kwa maana ya wafugaji watakuja kulisha kwenye majani ambayo tayari yamepandwa na wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii kwa kweli kama angekuwa anazungumzia kwenye maeneo yetu, sisi tunaojua hiyo adha iliyotokea kwa sababu ya migogoro hii ya wafugaji na wakulima wala isingekuwa na afya na wala hakuna mtu ambaye angeweza kusikia kauli ya namna hii. Ni hivi, hawa wafugaji wanavyokuwa wanavamia kwenye maeneo haya kwanza ni maeneo ambayo siyo rasmi kwa ufugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni maeneo ya kilimo, ni maeneo ambayo hayajatengwa kabisa na ufugaji. Sasa wakija wanaacha kabisa kulisha kwenye nyasi wanakwenda kulisha kwenye mazao kwa maana ya mahindi, mbaazi na mazao mengine. Wanayo wenyewe kauli yao wanasema wakilisha haya mazao, hawa ng’ombe wanatoa maziwa mengi na wananenepa kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya madhila tunayajua na tunashuhudia sisi ambao tunatoka kwenye maeneo hayo. Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri hapa, tuendelee kuchukua hatua. Hii kupongeza ninapopongeza kusiwe kwa muda, muendelee kuchukua hatua ili mgogoro ule usirudie tena, ili wale wafugaji wasirudie tena kwenye maeneo ambayo hayajatengwa kwa ajili ya ufugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye utatuzi wa mgogoro huu mimi kama Mbunge naishauri sana Wizara kuendelea kuzingatia usawa baina ya wafugaji na wakulima. Kwenye utatuzi wa migogoro hii wapo wakulima ambao wamepata madhila mbalimbali; wapo wengine wameuwawa na wapo wengine wamepata vilema vya kudumu. Hakuna hatua iliyochukuliwa na hakuna mtuhumiwa hata mmoja ambaye kwa sasa yupo mahabusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa na hii nitatolea mfano, wapo wapiga kura wangu tisa ambao sasa zaidi ya mwaka mmoja na nusu wapo ndani na kesi yao haieleweki. Hawa wamekamatwa kwa kesi ambayo haina mlalamikaji. Mimi niiombe sana Serikali kuchukua hatua juu ya vijana hawa ambao sasa zaidi ya mwaka na nusu wapo ndani ili kuleta usawa na amani kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii haikubaliki leo, hii wala haikubaliki kesho; na maeneo haya hata kufanya siasa ni ngumu kweli kweli kwa sababu wanahisi kwamba hawa wakulima wameonewa. Wapo wakulima ambao wameuawa hakuna mtuhumiwa, lakini huku upande mwingine tumeona hatua zimechukuliwa bila hata kushuhudia huyo aliyeuawa ni nani na alizikwa wapi. Hii haikubaliki, hii sasa tunaonesha ni double standard; na kwa kweli tukifanya hivyo hatuwezi kuendelea mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sana Serikali kupita Mheshimiwa Waziri hapa kuchukua hatua. Kama tunataka maridhiano ni pamoja na kuweka usawa kwenye jamii. Hawa vijana ambao hawana sababu mpaka sasa wapo ndani waone namna ya kuleta maridhiano. Kama upande wa wafugaji hakuna watu ambao wapo ndani na yapo madhila na matukio mbalimbali yalitokea, basi ni vizuri pia ku-balance hii hali; hawa vijana watoke nje nao ili waje waungane na jamii zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, inasikitisha sana na inatia uchungu, vijana hawa wengine ni wadogo wameacha wazazi wanateseka, wameacha wake wanateseka, wameacha watoto ambao kwa sasa hawawezi kusomeshwa. Niiombe sana Serikali…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Amandus. Jiandae Mheshimiwa Janejelly Ntate.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.