Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mimi pia niungane na mwezangu kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tukiangalia bajeti ya mifugo na uvuvi katika mwaka tunaoumaliza ilikuwa ni bilioni mbili tisini na mbili point tano, lakini leo wanaomba Bajeti ya bilioni 460.3, sawa na ongezeko la 63.5%. Hii ni kwamba Mheshimiwa Rais ana nia thabiti ya kutaka kuendeleza uvuvi na mifugo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Ulega na Naibu Waziri wake. Hakika wana nia thabiti ya kuendeleza uvuvi na mifugo na wakiwa na mtendaji wao ambaye ameongoza jahazi la watendaji, Profesa Riziki, hakika wamekuwa wasikivu kwa Kamati. Huwa napenda kauli yake Mheshimiwa Waziri, Kamati ikimwambia anasema hayo ni maelekezo na anakwenda kuyafanyika kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitajikita kwenye kuimarisha ranchi za Taifa, maana wameiweka ni kati ya kipaumbele kwenye vipaumbele vyao 10. Ranchi zetu za Taifa hizi zingeendelezwa huu mchango wa asilimia saba wa mifugo ungeweza kuongezeka zaidi ya hapo. Niwashauri, ranchi zetu nyingi zilikuwa zimetelekezwa na zimeshakuwa ni mapori. Sasa waende wakatengeneze miundombinu kama tunataka Watanzania wa kawaida ndio wawe wawekezaji kwenye hizo ranchi, kwa sababu wanaomba wanawapa. Wanaweza wakampa mtu hekta tano lakini hekta 20 ndizo zipo sawasawa. Pengine ni miti mikubwa ambayo yeye kwa uwezo wake hawezi kuwekeza. Kama watawekeza miundombinu iliyo sahihi then ndipo wakawakodisha hawa Watanzania, uzalishaji utaongezeka na manufaa ya hizi ranchi zitaongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, kwenye ranchi zetu hizi watumishi wengi ni vibarua na ni wa mikataba. Sidhani kama mtumishi kibarua anaweza akaleta tija kwa kujiamini kama hakuajiriwa kwa kazi ya kudumu. Hili nalo waende wakaliangalie.
Mheshimiwa Naibu Spika, uhondo wa ngoma ni sharti uingie ucheze. Leo watumishi wetu wa hizi ranchi hawana hata kitalu cha mfano ili kutuonesha ufugaji bora. Akiwa nacho hicho kitalu ni dhambi na akiwa nacho hicho kitalu ameshaonekana amevunja taratibu na Kanuni. Niwaombe waende wakaliangalie hili. Hawa watumishi wetu wa kwenye ranchi hizi wawe na vitalu vidogo vya mifano, wafuge kwa mifano ili na wengine tunaofuga nasi twende tukajifunze kutokea kwao. Hili pia liende na kwa Wizara ya Kilimo, hao Maafisa Ugani wetu wawe na mashamba ambayo ni ya mfano. Hii itatufanya kila mmoja kutaka kuingia kwenye tasnia hii ili kuwekeza, kwa sababu watakuwa wanacho cha kutuonesha; lakini sasa wanatuonesha vya kwenye karatasi tu. Atakuja ataniambia namna ya kuchanja mifugo, kulisha lakini yeye hana hata kitalu cha kunionesha au hata mifugo yake ameilishaje na inafananaje. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, kama alivyozoea, kwamba ushauri ni maelekezo, akalichakate hili na alifanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kuhusiana na hivi vitalu ni muda wanaopewa wawekezaji; hebu tujaribu kuona muda. Kuna wengine wakipewa mwaka mmoja atakuwa bado anapambana na visiki, mwaka mmoja bado anapambana na kuweka miundombinu, hawezi akapata faida na hivyo nasi hatuwezi kupata tunacholenga. Tuangalie muda wanaowapa uwe kama muda tunaopewa kwenye hati za umilikaji wa ardhi; uwe ni muda mrefu, mtu awekeze kwa muda mrefu ili Serikali ipate pato na yeye aweze kupata faida kama mwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye uvuvi sasa, uvuvi wa kwenye bahari. Leo hii kilimo walituambia hawawezi wakaleta mbolea, hawawezi wakaleta zana za kilimo ndani ya Dar es Salaam, lakini tuna bahari kuu. Katika hili waangaliwe akinamama na vijana wa Mkoa wa Dar es Salaam ili waingie kwa nguvu zaidi kwenye kilimo cha mwani, kufuga majongoo bahari kwenye Bahari yetu ya Hindi ili tuweze kuinua uchumi wao na waweze kupata kipato cha kila siku. Jana tumeona…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Janejelly.
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Naibu Spika, Ooh! Ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)