Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon Lucy John Sabu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kuipongeza Wizara, inayoongozwa na Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Abdallah Ulega, Naibu wake Mheshimiwa Alexander Mnyeti, pamoja na watendaji wote wa Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, amekuwa msikivu sana kwenye Kamati. Wakati wote tulipokuwa tukimshauri amekuwa akitupa ushirikiano. Pia niwapongeze na watendaji wote wa Wizara wakiongozwa na Profesa Shemdoe. Kiupekee kabisa niungane na wote waliochukua nafasi kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri na kubwa anayoifanya katika Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa tunampongeza kwa tukio alilolifanya tarehe 30 Mwezi Januari, 2024 katika Mkoa wa Mwanza, la kuwakabidhi wavuvi boti 160 na vizimba 222. Kiukweli kabisa tunampongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wamenufaika zaidi ya watu 16,000 na hasa wanawake na vijana. Tumeona katika bajeti ijayo zitaongezeka boti 497. Hii ni mara tatu zaidi ya ambazo zimetolewa awali. Kiukweli tunaipongeza sana Wizara kwa maono haya makubwa na mazuri kwa ajili ya wavuvi wanaozungukwa na Ziwa Victoria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kiupekee kabisa nichukue nafasi hii kuipongeza Wizara kwa mambo mbalimbali ambayo wanayafanya, hasa katika eneo la mbegu za malisho. Kama Kamati tumepata fursa ya kutembelea katika eneo la Pwani na Kibaha. Tumejionea namna ambavyo Wizara inatekeleza mradi huu. Kiukweli tunawapa hongera sana. Tusisitize tu, kwamba mbegu hizi za malisho ziwafikie wafugaji wote katika maeneo yote ambayo wanajihusisha na ufugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapongeza programu ya unenepeshaji wa ng’ombe kupitia NARCO ambapo mradi huu umewagusa vijana wa BBT na wanawake. Tunashukuru Wizara kwa maono haya mazuri ambayo yatasaidia kuwa na wafugaji vijana katika mradi huu wa unenepeshaji wa ng’ombe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuipongeza Wizara kwa Mradi wa Kopa Ng’ombe Lipa Maziwa. Nafahamu kwamba mradi huu unatekelezwa katika Mkoa wa Kigoma mahususi kwa ajili ya vijana na wanawake. Nichukue nafasi hii kuipongeza Wizara kwa ajili ya mradi huu. Kama ambavyo tuliahidi katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, kwamba, tutatengeneza ajira kwa vijana na wanawake; sasa nisisitize kwamba mradi huu uendelee kuwa endelevu. Ikimpendeza Mheshimiwa Waziri atafute fedha ili aweze kupeleka katika halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Simiyu tuna maeneo makubwa na mazuri kwa ajili ya mradi huu. Nimwombe Mheshimiwa Waziri atuletee mradi huu ili uwanufaishe vijana wa Mkoa wa Simiyu kuweza kufuga kisasa, lakini kuweza kufanya ufugaji wa ng’ombe hususani katika upande wa maziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuipongeza Wizara kwa namna ambavyo imeendelea kutenga maeneo kwa ajili ya wafugaji. Niendelee kusisitiza; na Mheshimiwa Waziri amesema katika hotuba yake kwamba ana mpango wa kuleta guest house kwa ajili ya wafugaji. Nimwombe, kama ilivyo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, kwamba tuliahidi kupima maeneo ya wafugaji na kuwamilikisha wafugaji maeneo kama ilivyo katika ilani ya uchaguzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nisisitize, kwamba ili kuondoa changamoto ya migogoro ya wafugaji na wakulima, Mheshimiwa Waziri atafute namna ya kutengeneza jambo hili ili kuweza kutenga maeneo kwa ajili ya wafugaji na kuondoa migogoro ambayo imekuwepo. Hii itatuwezesha kuwasaidia wafugaji kupata maeneo mazuri na kuwatengenezea miundombinu bora itakayowawezesha kuondokana na changamoto za migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona katika hotuba ya bajeti pia kwamba Wizara itaendeleza chanjo na uchanjaji wa mifugo. Niwapongeze mawaziri wa mifugo katika eneo hili. Pia, niendelee kusisitiza kwamba, chanjo za mifugo ni muhimu hivyo ziweze kuwafikia wananchi kwa wakati katika maeneo yote ambayo yanajihusisha na ufugaji wa ng’ombe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili litatusaidia kuweza kuhakikisha kwamba mifugo inakuwa katika viwango ambavyo ni vizuri ili wale wafugaji ambao wanasafirisha mifugo yao kwa ajili ya kutafuta masoko ya nje waweze kusafirisha na kufikisha mifugo ambayo ipo katika namna nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kukushukuru kwa fursa hii. Naunga mkono hoja iliyopo mezani. (Makofi)