Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Emmanuel Lekishon Shangai

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, moja kati ya majukumu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kupanga na kusimamia matumizi ya ardhi kwa ajili ya mifugo na uvuvi. Tukijaribu kuangalia kwa sasa hivi hatujaona kama Wizara imeweza kusimamia jukumu hili; kwa sababu wafugaji wa Tanzania, kama alivyosema hapa ndugu yangu Mheshimiwa Kunambi, wamekuwa kama watu ambao hawana mwenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, wafugaji wa Tanzania kama tunavyowazungumzia na kwenye hotuba yake amesema kwamba mifugo yetu imeongezeka; kwamba sasa hivi tuna ng’ombe milioni 37.6, mbuzi 27.6 million na kondoo milioni 9.4. Sasa hii mifugo yote inatakiwa kuwanufaisha wafugaji hao wa Tanzania. Kwa hiyo hao wafugaji ili waweze kunufaika ni lazima wawe na maeneo kwa ajili ya kulishia mifugo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri mwenyewe ajue kwamba katika maeneo yote ambayo Wizara ya Mifugo ilipima kwa ajili ya wafugaji wa Wilaya ya Ngorongoro, Monduli, Kiteto, Simanjiro na Longido. Maeneo yote yaliyopimwa na kuwekwa kwenye Gazeti la Serikali, kama ni maeneo ya malisho, yote yamechukuliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii. Kwa nini wao kama Wizara ya Mifugo wanayaruhusu haya? Leo ametuletea hoja ya kutaka kuanzisha mamlaka kamili kwa ajili ya mazao na miundombinu ya mifugo ambayo wote tungependa yatokee. Sasa hii mifugo ambayo hatuna maeneo ya malisho tutawalishia wapi kama hatuwezi kusimamia maeneo yao ya malisho? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kumshauri Mheshimiwa Waziri, ili Watanzania na wafugaji wa Tanzania waweze kunufaika na mifugo yao na ili uchumi wa Tanzania uweze kupanda kutokana na mifugo hiyo ni lazima tuwe na maeneo ya uhakika ya malisho na kuondoa migogoro kati ya wafugaji na wakulima nchini Tanzania. Kwa sababu tusipofanya hivyo hao wafugaji wanakuwa wanatembea kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiongelea kwa mfano Wilaya yangu ya Ngorongoro, eneo la Kijiji cha Engaresero, eneo ambalo lilipimwa ni la Reparkashi. Eneo hilo limechukuliwa na Wizara ya Maliasili, ambalo ni eneo la mifugo, ni eneo ambalo lipo kwenye GN ya Serikali kwenye Gazeti la Serikali, lilitangazwa kama eneo la malisho. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri kuangalia maeneo ya malisho; kwa sababu wafugaji kama hawana malisho maana yake ng’ombe wao watakufa na uchumi wa Tanzania utashuka kwa sababu hatutanufaika na mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, miongoni mwa majukumu mengine ya Wizara ni kuzuia magonjwa mbalimbali ya mifugo. Kwa sasa hivi kuna magonjwa mengi sana, ili sasa tuweze kuzuia ni lazima Wizara ihakikishe kwamba kila kijiji nchini Tanzania kina majosho ya kutosha kwa ajili ya kuogesha mifugo, kama tunataka kuzuia na kutibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kwamba Wizara ije na mkakati na kwenye hili baadaye nitamshikia shilingi; aje na mkakati atuambie sisi wafugaji kwamba Wizara imejipanga vipi na chanjo kwa ajili ya magonjwa mbalimbali Tanzania. Kwa sababu tuna magonjwa mengi sana ambapo tungechanja tungeweza kuzuia magonjwa mengi; lakini kila wakati ukienda kwenye maabara yetu tunasema bado tupo kwenye uchunguzi. Wapo kwenye uchunguzi mpaka lini? Unajua wafugaji wanapoteza mifugo mingapi kwa ajili ya PPR? Au unajua kwamba wafugaji wanapoteza mbuzi na kondoo wangapi kutokana na ugonjwa wa coenurosis, ugonjwa ambao unatokana na kirusi anayeitwa taenia multiceps? Ng’ombe, mbuzi wanapotezwa kwa sababu hatuwezi kuzuia. Tukiweza kuzuia tungeweza kuzuia hawa ng’ombe wasife wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka Mheshimiwa aje atuambie kwamba amejipanga vipi kwa ajili ya chanjo ya ECFF kwa wafugaji? Amejipanga vipi kwa ajili ya PPR? amejipanga vipi kwa ajili ya CCPP? Pamoja na chanjo ya ugonjwa holimilo kwa Wamasai wanasema hivyo. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri; yeye kama Waziri wa Mifugo tunataka kuona mbwebwe zake kwa wafugaji wa nchi hii. Tumpongeze sana na niunge mkono hoja. Nashukuru sana. (Makofi)