Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bahi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nchi yetu kwa sasa tuna viwanda karibu 10 vya kuchakata nyama kwa ajili ya kuuza nje ya nchi. Katika viwanda hivi 10 viwanda tisa vyote ni binafsi na kiwanda kimoja tu ni cha Serikali (machinjio ya Serikali) na machinjio hayo yapo hapa Dodoma, Machinjio ya Kizota. Katika viwanda hivi vingine vinavyobaki tisa vingine ni kama nilivyosema vya watu binafsi vingine vya EPZA.
Mheshimiwa Naibu Spika, huu ni mwaka wa tatu mfululizo nimekuwa nachangia kuomba Machinjio ya Kizota ipate fedha, nimeomba kwa miaka mitatu mfululizo na wala sio fedha nyingi ni shilingi bilioni mbili tu. Mheshimiwa Ulega ni rafiki yangu, amekuwa Naibu Waziri nikiomba bilioni mbili kwa ajili ya kiwanda kile, amekuwa Waziri naomba bilioni mbili kwa ajili ya machinjio yale na machinjio yale yanasaidia sisi hapa Dodoma. Napata shida kuelewa ni kitu gani kinawapa uzito kukarabati kiwanda kile na wafanyabiashara wetu kwenye maeneo ambayo wanataka wapelekwe wanafanyiwa hujuma, hawawezi kufanya kazi kule na hawawezi kusafirisha. Kwa hiyo, jambo hili sitakuja kulisema tena, lakini ni jambo ambalo linanisikitisha sana na Waziri anajua watu wetu wanavyopata shida na hujuma wanazofanyiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mara ya mwisho namwomba Mheshimiwa Waziri kukarabati kiwanda kile, kukarabati machinjio yale ili wafanyabiashara wetu waweze kuuza nje ya nchi. Kwa sasa Machinjio ya Kizota yanaruhusiwa kupeleka nyama katika nchi moja tu, nchi nyingine zote wamezuia kutokana na uchakavu na miundombinu ambayo haipo sawasawa. Hili jambo linasikitisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, waliopeleka habari ya kuzuia au waliotoa taarifa katika nchi hizo kwamba kiwanda kile ni chakavu ni washindani wao katika hivi viwanda tisa. Kwa hiyo, tunapata Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, kutoa nyama hapa Dodoma kuipeleka Dar es Salaam inachukua muda mrefu, lakini itakuwa ni dakika 30 unachukua nyama machinjio ya Kizota tunapeleka kwenye uwanja wa Masalato, nyama inaondoka masaa manne ipo Oman, Kuwait au Quatar. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, najua kiwanda hiki Waziri amekipeleka Ranch ya Kongwa, lakini pamoja na hiyo huu mwaka wa pili na kama nilivyosema uwepo wa Uwanja wa Ndege wa Msalato itakuja kufungua sana machinjio yetu na biashara yetu ya nyama.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine Kamati imesema, mnada ule wa Holoholo ushuru wa ng’ombe ni 30,000 na Kamati inapinga kwamba ni hela nyingi. Mimi napinga wazo la Kamati kwamba si hela nyingi, kwa sababu tuna viwanda vya kutosha, vipo 10. Unataka ng’ombe wetu wapelekwe nje ya nchi na wakipelekwa nje ya nchi nao wanafanyiwa processing, wanauzwa kwenye masoko ambayo tunaenda kushindana nao, lakini kwako hapo wamechukua bure na wanakuja kununua kwenye minada yetu ya kawaida katika price zetu za hapa ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachosema, ushuru pale uwe ni shilingi 100,000, ng’ombe kutoka nje ya nchi. Tena ni hela ndogo sana, walau iwe hata 200,000 kwa ng’ombe. Lengo si kupata ushuru, ng’ombe wako waende nje, tunachotaka ng’ombe wabaki hapa kwa sababu, tuna machinjio ya kutosha ili tuweze kuuza sisi wenyewe lakini mbuzi kupelekwa nje ya nchi kuvuka pale mpaka wa Namanga ni 6,500, that is a dumping price, nataka na mbuzi angalau iwe shilingi 50,000. (Makofi).
Mheshimiwa Naibu Spika, wala sio sifa kumuuza mnyama akiwa hai, kuwapelekea nchi jirani, sio sifa na kwa dunia hii ya leo unapeleka mnyama akiwa hai, huwezi ku-process, nyama inaenda kwenye nchi Jirani, ng’ombe anachinjwa halafu tunakutana kwenye masoko. Ninachotaka kusema hata 50,000 kwa mbuzi bado kidogo angalau wafanye 100,000, ng’ombe iwe 200,000 iwe 300,000. Lengo ni ku-discourage, tusipeleke wanyama wetu wakiwa hai kwenye nchi majirani zetu ambao tena katika masoko yale tunaenda kukutana nao, Mheshimiwa Waziri naomba sana hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kuhusu Jimbo langu nina mambo mawili. Kuhusu wafugaji katika Kata ya Zanka. Kata ya Zanka tumeingiliwa na Serikali. Kuna upande bonde la maji wamechukuwa kwamba wafugaji hawatakiwi kuingia huku. Ukivuka lami kidogo jeshi nao wamechukuwa kwamba ni eneo la mazoezi. Kwa hiyo, wananchi wa Kata ya Zanka hasa hasa Kijiji cha Zanka kimsingi hawana pa kulisha ng’ombe, huku unakutana na bonde mkono wa kushoto, huku unakuta jeshi wanasema wanataka kufanyia mazoezi, sasa na hilo ni jambo la Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kweli kwa dunia ya sasa hivi ufanyie mazoezi hapo Zanka? Urushe mambo yako hapo Zanka? Kwa hiyo, naiomba sana Serikali jambo hili waliangalie walifute. Kama ambavyo Mawaziri wale nane walizunguka hapa ni karibu, waende wakafute ile ni aibu na wananchi wanatushangaa. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nollo ahsante, muda wako umekwisha.
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)