Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuishukuru Wizara nzima, nasema hongereni sana kwa kazi nzuri mliyoifanya na kwa hotuba nzuri mliyoitoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, naomba niongelee kuhusu malisho pamoja na mambo mengine. Mifugo inahitaji chakula, maji na chanjo kusudi iwe na afya. Kwa hiyo, niongelee kwenye upande wa malisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, upande wangu wa Morogoro, ili upunguze migogoro ya wafugaji na wakulima ni lazima uwe na malisho mazuri. Kwa hiyo, nasema ingawa Wizara imesema jinsi ya kueneza malisho, naomba sana wafugaji wote waweze kupata elimu ya kuwa na malisho, ili kusudi kupunguza migogoro ya wafugaji na wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo kubwa ni ingawa Mheshimiwa Waziri amesema kuwa mbegu zipo, lakini nasisitiza kuwa mbegu ziendelee kuzalishwa kwa wingi na ziweze kuonekana madukani. Pia, elimu itolewe, Maafisa Ugani waweze kuwa karibu na wafugaji, ili waweze kupata elimu ya kilimo cha majani haya ya malisho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni, naongelea kuhusu kuku wa kienyeji. Watu wote humu mnapenda kuku wa kienyeji na watu wengi wanapenda kuku wa kienyeji, lakini sijasikia vizuri kwenye hotuba jinsi ya kuendeleza kuku wa kienyeji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanawake na vijana wengi wanafuga kuku wa kienyeji. Mheshimiwa Waziri akija ku-wind up, naomba aniambie jinsi ya kuendeleza kuku wa kienyeji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, naongelea kuhusu mambo ya uhaba wa samaki. Uhaba wa samaki ni kwa sababu ya uvuvi haramu. Uvuvi haramu umeanza muda mrefu na kuudhibiti imekuwa kazi. Mheshimiwa Waziri namwamini, kijana wangu namwamini, naomba sana uhaba huu wa samaki usiendelee kutokana na uvuvi haramu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na uhaba wa samaki viwanda mbalimbali vimefungwa, bei ya samaki imekuwa juu na bado nchini tuna utapiamlo. Tumesema, samaki anachangia 30% ya protini, lakini kama bei iko juu watu hawawezi kununua samaki. Kwa hiyo, nakuomba sana, uhaba huu na uvuvi haramu uweze kutokomezwa kabisa. Naomba sana uangalie ufugaji wa vizimba na ufugaji wa mabwawa, ili kusudi tuweze kuwa na samaki wa kutosha ambao wanaweza kuenea na kuwa na protini ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa ni kuhusu BBT. BBT ni nzuri sana, ninaomba uiendeleze. BBT kwa upande wa unenepeshaji wa mifugo naona mmeanza vizuri kwenye mikoa mbalimbali, ikiwepo Kikurura na Kongwa, jana tumeona wamefanya mambo mazuri sana. Naomba yaendelee, ili kusudi vijana na akinamama waweze kuendelea vizuri kujiajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, BBT inatoa ajira, inaongeza pato la Taifa, inaongeza pato la familia na vijana wanapata ajira. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri aangalie sana kuhusu hiyo BBT. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nikiwa na dakika ya mwisho, naomba niongelee mtiririko wa fedha. Naomba sana mtiririko wa fedha uwekwe vizuri, hela zote ziweze kutoka kama zilivyobajetiwa na miradi yote iweze kutimia vizuri. Naamini kutokana na mifugo, Pato la Taifa litakua kutoka asilimia saba na pato la uvuvi kuwa asilimia moja point nane. Namwomba sana Waziri aangalie hilo na Mwenyezi Mungu awabariki Wizara nzima, wafanye kazi nzuri, naunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)