Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busanda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuweza kuchangia katika Bajeti hii ya Mifugo na Uvuvi. Jimboni kwangu kuna migogoro kati ya wafugaji na wakulima katika sehemu moja inaitwa Ludete na nyingine inaitwa Katangalo kwenye Kata ya Kaseme. Kwa hiyo nimechukua muda kutafuta kwa nini migogoro hii ambayo nimeitoa kwangu na sehemu nyingine ndani ya nchi hii inaonekana kama ni changamoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikalichukua eneo zima la Tanzania ambalo ni kilometa za mraba 945,087 ambazo ni sawa sawa na ekari milioni 233,535,723 lakini nikachukua ongezeko ambalo nampogeza Mheshimiwa Waziri kwamba ng’ombe wameongezeka kutoka milioni 36.6 mpaka 37.9. Sasa nikatafuta mahitaji ya hawa ng’ombe bila kuingiza kuku, mbuzi wala kitu kingine chochote katika ile mifugo. Kwa kawaida ukienda kwenye researches utagundua kwamba kwenye mazingira yetu ya uoto ng’ombe anaweza kula kuanzia ekari sita mpaka ekari nane. Ukipiga hesabu utagundua kuwa mahitaji ya ardhi kwa ajili ya kuchunga hapa nchini kwa hiyo free range grazing inatupeleka kwenye milioni 303,200,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kimsingi hata kama ndani ya nchi hii wakabaki ng’ombe peke yao bado ardhi tuliyonayo haitoshi. Kwa hiyo sisi kama Watanzania tunatakiwa tuhame tutafute sayari nyingine, tuondoke na mbuzi na kuku kwa sababu ardhi hii haitoshi. Nataka kushauri nini hapo? Nataka kushauri kwamba tumepewa akili, elimu na maarifa kama wanadamu maana yake uoto wetu lazima tuuboreshe, malisho yetu sasa yafanyiwe kazi. Tumekuwa na ardhi tumesema kuna matumizi bora ya ardhi yamewekwa sehemu na sehemu lakini hayaheshimiwi kwa hiyo matokeo yake ni kwamba tunatakiwa sasa tuboreshe, wataalam tulionao waboreshe. Tunaona ng’ombe wakiongezeka tunapata mapato zaidi lakini bado malisho yetu hayatoshi na bado uwekezaji huu ambao nimeuona saivi umekwenda kwenye shilingi bilioni 460 hautoshi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kufanya transformation ya Wizara ya Uvuvi kwa shilingi bilioni 460, haiwezekani ni ndogo sana. Kwa hiyo tuiombe Serikali iangalie inapoenda kufanya transformation cost isije kwa gharama hii ndogo kama tunapata Pato la Serikali kwa asilimia saba kwenye mifugo na 1.8% kwenye Samaki, tuhakikishe kwamba tunaingiza fedha yakutosha kwa sababu tumeshaona ni reality ile kwamba tukiingiza fedha nyingi tunapata nyingi. Kwa nini hatuingizi fedha nyingi ili tupate nyingi zaidi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nigusie uvuvi kidogo kwa sababu ya muda. Kule Jimboni Busanda nampongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu vikundi kadhaa vimekopeshwa, sasa wanaanza kufanya uzalishaji huu. Wapo baadhi ambao walipewa zile boti za mita tano isivyo bahati nafikiri kuna mahali palifanyika makosa kwenye uvuvi, hazifanyi kazi vizuri ila kwenye vizimba zinafanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo wataalam wakaangalie upya kuona kama wale wanaotaka kuvua kwa hizo boti za mita tano zifanyiwe mabadiliko ili wazitumie tu kwenye vizimba. Vilevile chakula ni changamoto, kama wenzangu walivyochangia ndugu yangu Mheshimiwa Tabasam hapa chakula kina bei ya juu vilevile upatikanaji wake ni adimu. Kwa hiyo watu wetu wamepata mwamko mkubwa mwitikio ni mkubwa sana lakini upatikanaji wa chakula ni changamoto. Kwa hiyo niombe sana Mheshimiwa Waziri hili utusaidie kule Busanda ili tunapoanza sasa kushughulika na vizimba tushughulike na vizimba na vitu vyote viweze kupatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)