Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ludewa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Wizara hii. Kule Ludewa nina kata nane ambazo zimegusa maji, Kata ya Lumbila, Kilondo, Lifuma, Makonde, Lupingu, Lwela, Manda na Ruhuhu wananchi wake hawapungui 30,000 ambao wanategemea shughuli ya uvuvi kwenye maisha yao ili kuweza kupata mkate wa kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nipende kuchukua nafasi hii kushukuru sana Wizara hii; Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kupanga mpango wa kujenga soko la samaki pale Manda. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutuletea shilingi milioni 809 kwa ajili ya ujenzi wa soko la samaki ambalo litakuwa na kisasa lina yale majokofu kwa ajili ya kuhufadhi samaki kwa hiyo nishukuru sana, Wananchi wa Ludewa wamefurahi sana na wanaishukuru sana Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kumekuwa na changamoto kwenye lile ziwa ya uhaba wa samaki kutokana na tabia zake. Kwa hiyo niombe Serikali itenge fedha za kutosha kwa ajili ya kufanya tafiti kwenye ziwa hili (Ziwa Nyasa) ili kuweza kujua kwa nini kunakuwa na uhaba wa Samaki. Vilevile niliusikiliza mchango wa kaka yangu Mheshimiwa Mabula niliona anawashauri Wizara kwamba mjikite kwenye Ziwa Victoria kwanza mpaka uzoefu upatikane. Mheshimiwa Waziri mimi napenda nikuhakikishie kabisa Wananchi wa Ludewa wameshajiandaa kufuga samaki kwa njia ya vizimba na kwa kutumia Mfuko wa Jimbo tuliweka kizimba kimoja cha majaribio, matokeo yake Mheshimiwa Waziri yamekuwa mazuri sana. Tulikwenda kwa kushirikiana na watu wa TAFIRI walipita maeneo yote, wameainisha maeneo ambayo hayana mawimbi makali ambayo yanafaa kwa ajili ya ufugaji wa samaki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tuliweka kizimba cha kwanza kwa kutumia fedha ya Mfuko wa Jimbo, kwa hiyo tumevuna samaki wa kutosha wenye uzito unaoridhisha. Kuhusu vifaranga, tulifuata ushauri wote ambao TAFIRI walitushauri, tulikwenda kuchukua pale Ruhila kwa kweli wamefanya vizuri sana. Kwa hiyo naomba kwenye vile vizimba 400 ambavyo Mheshimiwa Waziri amesema vipo na sisi wa Ziwa Nyasa kule Ludewa tuweze kupewa vizimba vya kutosha kwa sababu tuna maeneo tumeshaainisha pale Lupingu. Kuna maeneo tumeshaainisha Iwela, Manda na maeneo mengine ya Lumbila na Kilondo ambayo yanafaa sana kwa sababu hayana mawimbi makali sana, kwa hiyo yanafaa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika kuna yale mahema ya kisasa kwa ajili ya kukaushia dagaa, tunaomba sana Mheshimiwa maeneo ya Lifuma wanapata sana dagaa wale wa Ziwa Nyasa na wale dagaa ni wazuri sana na ni watamu mno. Watu wanatoka mpaka kule DRC na nchi nyingine jirani wanawafuata pale Makonde na Lifuma. Kwa hiyo tunaomba sana utusaidie teknolojia ya kuwaanika wale dagaa ili waweze kufaa kwenye soko la ndani na soko la Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiweza kuweka hivi vizimba tutasaidia soko lile lipate samaki wa kutosha na hii hoja niliyoisema ya utafiti kuna Mto Ruhuhu ambao unatenganisha Wliaya ya Ludewa na Wilaya ya Nyasa. Ukifika Mwezi wa Sita au wa Saba kuanzia huu wa Tano wavuvi wanapata sana samaki aina ya mbelele lakini samaki wote wale wakivuliwa wanakuwa na mayai tumboni. Kwa hiyo nadhani tafiti zikifanyika wanaweza wakatoa elimu kwa wavuvi huenda ule ndiyo msimu wao wa kwenda kutaga kule kwenye mto au vitu vingine lakini kwa kuwa wavuvi hawajapata elimu ya kutosha wanawavua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru Serikali kwa kutafuta eneo Kata ya Ruhuhu kwa ajili ya kituo cha utafiti wa ukuzaji viumbe maji. Eneo hili litasaidia sana kutoa elimu kwa wavuvi juu ya kuhifadhi mazingira ya ziwa nyasa na kuhakikisha samaki wanapatikana wa kutosha. Kumeanza kuonekana samaki wageni ambao inaonekana wanatoka nchi Jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa manufaa ya muda niseme naunga mkono hoja lakini niombe pia Wizara hii...
NAIBU SPIKA: Ahsante.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)