Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa fursa uliyonipa. Kwanza nianze kwa kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais hasa kwa kuwakumbuka sekta ya uvuvi, sekta ambayo kidogo ilikuwa imesahaulika katika vitendeakazi. Sitaki kurudia aliyoyasema Mabula lakini tayari na mimi ni mnufaika kwa maana ya Wilaya ya Ilemela. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuzungumzia suala la mikopo ya boti kwa vikundi vya ushirika ambavyo wamepata, ninaomba sana Serikali iangalie boti mlizowakopesha si zile walizoomba, waliomba boti za uvuvi mkawapa boti za kukusanyia Samaki, kwa hiyo hazifanyi kazi. Pia na zile mlizowapa wavuvi wanadai horsepower ni kubwa kuliko mahitaji waliyonayo. Kwa hiyo, unakuta gharama ya uendeshaji ni kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwakumbushe tu watu wa Wizara ya Mifugo ya kwamba mwaka 2022 tumefanya sensa ya watu na makazi japokuwa na wanyama au mifugo ilikuwa inahesabiwa lakini tungeomba kama Serikali kuwepo na sensa ya mifugo ambayo itakwenda kutupa picha halisi ya idadi ya mifugo tuliyonayo ili kuweza kuona uwekezaji tulionao na namna ya kuweza kuhudumia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Maafisa Ugani ni wachache pia kwa sababu hatuna idadi kamili ya ng’ombe, hawa tulionao tunao kwa makadirio lakini siyo, usitarajie mwenye mali akuambie ana ng’ombe 20 wakati ana ng’ombe 200, lakini ukienda specifically kwenye sensa ya mifugo tutapata idadi na tutaweza kuwahudumia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala zima la malisho. Tunayo maeneo ambayo yametengwa, ambayo kwa mujibu wa kumbukumbu umeonesha karibu hekta 81,000 ambazo zimetengwa kwa ajili ya ufugaji, tungeomba pia katika suala zima la namna ya kulisha basi wasaidiwe wale wavuvi na wale walioko kwenye viwanja vyenye urban farming wanaruhusiwa kufanya kazi hiyo. Kwa hiyo, na wao ni vizuri wakapata namna bora ya kuweza kuandaa malisho ndani ya maeneo yao, kwa sababu wamechukua eneo la urban farming, lakini hafanyi hiyo kazi anafanya shughuli nyingine. Kwa hiyo, hao nao ni vizuri wakaweza kupewa hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni suala zima la uvuvi ndani ya Ziwa Victoria ambao unaendelea. Ni vema kweli wanafunga ziwa kwa siku kadhaa, lakini unakuta wale wavuvi wa dagaa siku anazopata kufanya uvuvi ni chache ukilinganisha na wale wanaovua samaki, basi pengine na leseni kwa sababu ziko sawa zingetofautishwa kwa sababu hawa wanafanya kazi siku chache kuliko wale wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la royalty, watu wa samaki wanatozwa kwa dola, tungekuwa na usawa katika suala zima la utozaji, leseni ziwe za bei ya Tanzanian shillings badala wengine kulipa dola wengine wanalipa shilingi halafu anakuwa hana uhakika na kiasi anachotakiwa kulipa maana dola ina panda na kushuka kwa hiyo kwake inakuwa ni ngumu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, ningeomba kwenye suala zima la uwekezaji. Watu tunaowapa maeneo ya uwekezaji ni vizuri Serikali ikaandaa miundombinu ya msingi. Kwa mfano, kuwepo na majosho, malambo kwa ajili ya maji, kuwepo na umeme halafu yeye afanye zile shughuli zingine. Kama ni suala la kuongeza thamani pia itakuwa ni rahisi zaidi kwake yeye kufanya kazi hiyo, lakini tusipofanya hivyo ndiyo unakuta wanalalamika kila siku wanasema mazingira si rafiki lakini tungewaandalia kwa sababu tunazo ranch zetu zipo lakini wapo wale ambao wanachukua nje ya ranch, kwa hiyo inakuwa ni rahisi zaidi katika suala zima la kuweza kuwawezesha ili waweze kuwa na miundombinu rafiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala zima la vikundi ambavyo vimeomba mikopo, mpaka sasa kwenye Jimbo kuna vikundi zaidi ya 36 vimeomba, naishukuru sana Serikali kwa sababu tayari wameweka tengeo kwa ajili hiyo, changamoto iliyopo ni kwamba mikopo pengine inachelewa sana, naomba mikopo hiyo iweze kuharakishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la uboreshaji mialo. Tukumbuke kwamba hii mialo katika Ziwa Victoria na maeneo mengine wanauza samaki pia katika soko la European Union, sasa kama haijakaa vizuri kidogo itakuwa ni changamoto, naomba katika maeneo yote iweze kuboreshwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru sana Serikali, katika Jimbo langu kuna mialo mitatu inayokwenda kuboreshwa ambayo ni mwalo wa Kirumba, Mwalo wa Igombe na Mwalo wa Kayenze Ndogo shilingi bilioni 33.5 zimetengwa ni shukurani kwa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa fursa uliyonipa Mungu awabariki sana wakachape kazi, mwaafanya kazi nzuri. (Makofi)