Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa hii nafasi ya kuchangia kwenye hii Wizara ya Mifugo na Uvuvi, lakini kipekee namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza kwenye sekta ya mifugo na uvuvi hususan kule kwetu Manyoni Mashariki. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Ndugu yangu Ulega pamoja na Naibu Waziri, Katibu Mkuu Profesa Shemdoe Mwalimu wangu wa Chuo Kikuu cha Sokoine kwa kazi kubwa ambayo wameifanya kule Manyoni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii Wizara imefanya mambo makubwa sana kule Manyoni. Kwanza, kwenye upande wa majosho ndani ya miaka mitatu Manyoni tumeweza kujenga majosho nane na haya ni mabadiliko makubwa sana kwa Manyoni kwa sababu miaka mitano ya nyuma iliyopita hakuna hata josho moja lililojengwa. Kwa hiyo, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa hii juhudi ambayo wameionesha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bado tuna maeneo ambayo yanauhitaji wa majosho ikiwepo Kijiji cha Kasanii, Kijiji cha Magasai, Kijiji cha Simbanguru, Kijiji cha Dabia vilevile Kijiji cha Udimaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ningependa kuchangia upande wa minada. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri, katika Tarafa ya Kintinku Manyoni wamejenga mnada wa kisasa wa zaidi ya milioni 270, tayari mnada umekamilika, kuna mambo machache tu ambayo wanatakiwa kuyamaliza, na niseme Mheshimiwa Waziri Mkoa mzima wa Singida hakuna mnada wa kisasa uliojengwa kama ule wa Manyoni. Nakushukuru sana na tunakusubiri uje Manyoni katika Kata ya Kintinku uje uone ule mnada na uje utufungulie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunalo ombi moja, pale ndani tunahitaji kukamilisha vyoo, kujenga ofisi kwa ajili ya mapato na kujenga lile eneo dogo kwa ajili ya kutunzia mifugo. Mimi nilete salamu hizi za watu wa Manyoni kwa kazi kubwa ambayo wameifanya, kwa kweli ameweka historia kubwa sana kwa wafugaji wa Manyoni nasi tunamuahidi Mheshimiwa Rais, wafugaji wamenituma mwakani wafugaji wote watamuunga mkono Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho kabla sijamalizia kuhusu minada. Namshauri Mheshimiwa Waziri, sasa tuachane na suala la kuuza ng’ombe kwa kukisia urefu, uzito na umbile twendeni kwenye kutumia mizani. Amejenga mnada wa kisasa Manyoni, tunataka sasa kwenye ule mnada watu wauze ng’ombe kwa kupima kwenye mizani, huo ndiyo ushauri wangu ambao nampa Mheshimiwa Waziri leo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ni kuhusu mamlaka ya kusimamia sekta ya mifugo, wenzangu wengi wameongelea. Najua hili liko ndani ya uwezo wa Mheshimiwa Waziri, ameipambania Sekta ya Mifugo, bajeti yako imeongezeka tunataka sasa tuanzishe mamlaka ambayo itaenda kuwakomboa wafugaji wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1974 Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipitisha mamlaka ya kusimamia Sekta ya Maendeleo ya Mifugo, Sheria Namba 14 ya mwaka 1974 na aliisaini Julai. Nina maswali machache kwa Mheshimiwa Waziri, ni sheria gani ya Bunge iliifuta mamlaka hii? Nadhani tukipata huo uelewa itakuwa ni rahisi na sisi kujua kwamba, kwa nini ile mamlaka ya zamani ilifutwa na je, hii tunayoenda kuianzisha itatofautianaje na ile mamlaka ambayo ilikuwepo kipindi hicho? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho ni ombi. Nimesikia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, anaanzisha zile milk collection centre, vituo vya kukusanyia maziwa. Nimechangia sana hapa Bungeni kuhusu uzalishaji wa maziwa kule Manyoni, namwomba Waziri anapoenda kuanzisha hivi vituo asisahau wafugaji wa Manyoni. Sisi tunafuga sana mifugo, tuna ng’ombe wengi sana zaidi ya laki moja na tisini na tano kule. Kwa hiyo, namwomba Waziri anapoenda kuanzisha vile vituo vya kukusanya maziwa asisahau Manyoni hususan Manyoni Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, narudia kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, lakini nikmongeze Mheshimiwa Waziri anafanya kazi kubwa, tunamkaribisha sana Manyoni, karibu sana Manyoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)