Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuendelea kutupa afya na uzima kuendelea kuwatumikia wananchi waliotuchagua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kutoa pongezi nyingi sana kwa Serikali, nikianzia na Mheshimiwa Rais mwenyewe pamoja na viongozi wa Wizara hii, Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na wengine wote. Nasema hivyo kwa sababu Sekta hii ya Mifugo na Uvuvi ni sekta ambayo inachangia pato la Taifa kwa kiwango kidogo lakini ni kwa sababu tulikuwa hatujawekeza kwa kiasi kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii inaonesha jinsi ambavyo sasa Serikali iko serious kutaka sekta hii ichangie kwenye pato la Taifa. Ukiangalia mwaka 2021/2022, bajeti yake ilikuwa bilioni 169 lakini leo tunazungumza bajeti ya 2024/2025 bilioni 460 hii inaonesha kwamba sasa Serikali imeamua kwa dhati kabisa kuwekeza katika mifugo na uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana nilisimama katika Bunge hili nikasema maneno makali kuhusu suala la kufunga Ziwa Tanganyika, nilisema nikiwa na sababu. Sababu ya kwanza nilitaka Serikali isishirikiane na Serikali za Nchi za Zambia, Congo na Burundi kufanya maamuzi bila kushirikisha wananchi. Baada ya kusema maneno hayo, namshukuru Waziri huyu msikivu na mwana mapinduzi akaamua kutukusanya wote Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa, Wabunge wote tunaotoka Mikoa hii ya Rukwa, Katavi na Kigoma, tukafanya kikao akaanza kutupa uelewa sisi tukaelewa akashuka akaenda kwa wavuvi wetu kwenye maeneo mbalimbali akakutana nao, wakafanya mikutano ya hadhara kuwaeleza faida tutakazozipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni mwanasiasa najua kabisa kwamba wakati mwingine siasa inadharaulika mtu unaweza ukafika mahali akasema bwana wee hiyo unayosema ni siasa tu, lakini siasa ndiyo inayoongoza nchi. Lazima sisi wanasiasa tufike mahali tusimame katika uanasiasa wetu kwa ukweli ili kuiheshimisha siasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka hapa kabla ya kusema maneno haya ninukuu kwanza maneno ya Hayati Mzee Abeid Aman Karume aliyekuwa kiongozi wa nchi ya Zanzibar. Mheshimiwa Hayati Abeid Karume aliwahi kusema haya, “ni bora kumuudhi mtu siku moja kwa mambo mtakayokuja kukubaliana siku zote kuliko kumfurahisha mtu siku moja kwa mambo ambayo utakuja kumuudhi siku zote.” (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nikisimama hapa nikataka kufurahisha wananchi wa Kigoma, Rukwa na Katavi kwa kusema Ziwa lisifungwe ili leo wapige makofi lakini watakuja kunichukia siku zote, bora leo niwaambie naungana na Serikali kukubaliana Ziwa lifungwe ili waje wanipende siku zote. Hili nalisema kwa sababu mimi ni mtoto wa mvuvi, mapato tuliyokuwa tunayapata kwenye uvuvi katika Ziwa Tanganyika katika miaka ya 1970, 1980 na 1990 hadi miaka ya 2000, mapato hayo yameshuka kama ni kutoka asilimia mia mpaka asilimia kumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uvuvi katika Ziwa Tanganyika uko katika hali mbaya sana, kuwaambia wananchi twendeni hivyo hivyo ni kuwadanganya na kufika mahala kuwapotezea muda na siku moja watakuja watuchukie. Ni dhahiri Serikali yetu imefanya utafiti tena utafiti wa kimataifa wakishirikiana na Nchi hizi za Burundi, Zambia na Congo, wameona kwamba kufunga ndiyo njia itakayowasaidia wananchi, hasa kufunga kwenyewe wanafunga katika kipindi sisi tunaita kilimia, yaani mwezi wa tano, mwezi wa sita na mwezi wa saba, ni miezi ambayo Ziwa kwa kawaida huwa linajifunga, mapato yanakuwa madogo sana. Ninawasihi wananchi na ninaishukuru Serikali kwa kuja na utaratibu huu ili mtakapofungua wananchi wapate mapato makubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na naishauri Serikali kuongeza udhibiti katika uvuvi haramu. Ahsante sana. (Makofi)