Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkuranga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na mimi kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na mwingi wa ukarimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, naomba nichukue fursa hii kurejea tena kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini katika Wizara hii. Naomba pia nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa wasaidizi alionipatia wakiongozwa na Mheshimiwa Alexander Mnyeti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme mbele ya Bunge hili leo, wengi wanavyomfahamu Mheshimiwa Mnyeti na yule Mnyeti anayefahamika, ya kwamba ni mtu kama mkorofi hivi. Nataka nikuhakikishie wewe na Bunge lako, kwamba Mheshimiwa Rais ni Mama mwenye maarifa makubwa sana. Ameniletea huyu Mnyeti tufanye kazi; na yeye amesema katika hadhara hii namna ambavyo amekutana uungwana wa kiwango cha juu kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo wakati tunafanya mjadala wa kujibu hoja tukiwa mimi na yeye na Katibu wetu Profesa Riziki Shemdoe akaniambia, Mheshimiwa Waziri unafahamu miaka miwili mitatu mpaka juzi tu hapa mimi ustaarabu kwangu ulikuwa mbali sana; lakini kwa hakika nimeingia mahali hapa na baada ya kukutana na wewe na hii timu ya Wizara ya Mifugo na uvuvi niseme namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kunileta kufanya kazi na timu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa Misungwi wamepata Mbunge, ni mtu mkweli, ni mtu mwenye msimamo na kwa hakika mimi ananisaidia vyema sana. Wakati mwingine ninapoona hapa panahitaji namna ya mtu mwenye haiba yake namtanguliza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yuko hapa Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nataka nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu anifikishie salamu nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais. Nataka nimwambie kwamba combination tuliyonayo katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi ingekuwa ni timu ya mpira, basi ni ile iliyochukua ubingwa siku ya jana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mara baada ya kuyasema hayo naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, niseme kwa kunipa Profesa Shemdoe. Mwaka jana nilisema hapa kwamba ninayo timu nzuri na nikamsifu. Sikumsifu kwa burebure; ni mtu msikivu na ni mtu anayeelekezeka. Sisi sote ni viongozi na tunafahamu, kwamba uongozi ukiachilia mbali masuala ya kiubunifu, uongozi ni masikilizano. Ikiwa ndani ya nyumba hakuna masikilizano kila mmoja anakwenda kivyake, hakika nyumba hiyo haiwezi kuleta mazao mema. Leo tunazungumzia Wizara ya Mifugo na Uvuvi juu ya 4Rs za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na sisi tumejikita katika hizo, tumejikita katika Ilani yua Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi; tumejikita katika Mpango wa Taifa (Dira ya Taifa). (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, 4Rs zimetafsiriwa katika Sekta ya Mifugo na Uvuvi, leo nilikuja hapa na katika ujio wangu nilikuja na mbegu ambazo zimekuwa parked kutoka Wizarani. Shirika letu la Utafiti wa Mifugo (TALIRI), lakini na mashamba yetu ya mifugo pale tunakwenda kutengeneza uhimilivu. Katika zile 4Rs liko jambo la Resilience na sisi tunakwenda kutengeneza uvumilivu na mimi kwa kuheshimu michango ya Waheshimiwa Wabunge na kwa kuheshimu mchango wa Kamati yetu ya Bunge ambayo ni Kamati mahiri sana na imekuwa ikitushauri vyema wakati wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaombe Waheshimiwa Wabunge hakuna uchawi katika jambo hili. Niko tayari Wabunge wa majimbo yote kuwapatia mbegu za malisho waende nazo kwa ajili kwenda kuhamasisha wafugaji wetu wapande. Tutatoa mbegu za malisho ya nyasi na tutatoa mbegu za malisho aina ya Jucow na ninayo furaha kubwa katika ufuatiliaji katika banda letu la wiki ya protini hapa Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana umewaalika Wabunge na wameitika, habari niliyonayo leo wameona namna ambavyo nchi yetu ina mazao ya kutosha ya protini na wale ambao hawakupata, nataka niwaambie ya kwamba wasiwe na wasiwasi, protini bado tunayo ya kutosha. Tunatengeneza 4Rs, zile 4Rs za kustahamiliana na uendelevu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kutengeneza upya Sekta ya Mifugo na Uvuvi katika Bandari ya Kilwa Masoko ambayo ndugu yangu Ally Kassinge ameisema kwa lugha nzuri ya kupendeza sana ni katika kutengeneza upya Sekta ya Mifugo na Uvuvi. Sekta ya Uvuvi iweze kuwa na mchango mpana na mkubwa katika Taifa letu. Yale ndiyo maono na ile ndiyo tafsiri ya zile 4Rs za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema na haya maneno naomba yachukuliwe na Waheshimiwa Wabunge, hakika migogoro ya wakulima na wafugaji na watumiaji wengine ni lazima sisi sote tuhakikishe kwamba tunakwenda na msimamo huu; kama mfugaji anadhani kwamba yale mahindi ya yule mkulima aliyeyaweka pale shambani kwake ni matamu sana sisi tunayo Jucow ambayo ni tamu zaidi ya yale mahindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, basi kama mmoja katika wasemaji alivyoshauri hapa akasema, “kwa nini wakulima wasilime nyasi tu ili wawauzie wafugaji?” Mimi nasema Waheshimiwa Wabunge njooni tuwapatie mbegu twende tuwapelekee wafugaji wetu; wajifunze na wakubali kwamba dunia imebadilika na hakuna jambo lingine isipokuwa ni lazima tupande nyasi zetu na tuweze kuvuna kwa ajili ya malisho wakati wa kiangazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme pia juu ya ufungwaji wa Ziwa Tanganyika, amejibu vyema Naibu Waziri. Ameeleza baadhi ya hoja na amezitolea ufafanuzi mzuri na hili la Ziwa Tanganyika limesemwa hapa na Wabunge wengi wa eneo hili la ukanda wa Ziwa Tanganyika. Kwa kuwa Naibu Waziri wangu ameshalisema jambo hili maelezo yangu yatakuwa ni mafupi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge leo tunaomba vizimba viende Ziwa Tanganyika, lakini nataka niwaambie, katika ule mkataba niwajulishe ndugu zangu kwamba kabla ya huu mkataba ambao leo tunauzungumza hapa Bungeni Ziwa Tanganyika hapakuwa na ruhusa ya kuweka vizimba. Huu mkataba moja ya faida yake katika zile protocols zilizosainiwa na kukubaliwa ni pamoja na kukubaliana kuanzisha miradi ya kuweka vizimba. Hili dunia yote inajua capture fisheries (uvuvi wa asili) duniani kote unaanguka. Hii ni hoja ya mabadiliko ya tabianchi na hii ni hoja ya ukuaji wa population ya dunia. Kwa hiyo, hakuna jambo lingine ni lazima mwanadamu atumie vyema maarifa yake kwa kupanda samaki mle ili kusudi waweze kumpatia mazao.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vizimba ni kitu cha uhakika zaidi kuliko hata hii capture fisheries. Wakati mwingine mvuvi anatoka anakwenda katika maji kwa sababu ni mawindo; anakwenda kuwinda, hana uhakika. Anarudi aidha amepata kilo moja, kilo mbili au hakupata kabisa lakini vile vizimba ni kitu cha uhakika. Ukiweka samaki 4,000 wataokufa hawawezi kuzidi 20% ya hao 4,000, watakaobaki wote utawavuna.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaombe ndugu zangu kwamba, sisi Wizara ya Mifugo na Uvuvi tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan; amefanya kazi kubwa sana mno pale Mwanza, ameianzisha. Ule mwendo aliouanzisha nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wa Tanganyika wote. Nikushukuru sana kaka yangu Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda, umesema kwa ufundi wa hali ya juu namna ambavyo hatupaswi kurudi nyuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 15 Agosti, nitakwenda Kigoma nitahakikisha pia namwelekeza Naibu Waziri wangu aende Rukwa. Tutakwenda kuwaonesha namna ya mazao yatakavyopatikana mara baada ya kipindi hiki cha ufungwaji wa ziwa na kipindi hiki cha kilimia kitakapokuwa kimepita; kwa namna tulivyojipanga tutakapokwenda tarehe 15 Agosti, hatutakwenda mikono mitupu kwa sababu moja ya tatizo kubwa tulilonalo katika eneo hili ambalo ni tatizo la cost harvest loss, upotevu mkubwa sana wa mazao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tutakuwa tumezalisha samaki wengi sana nina wasiwasi mkubwa tusije tukawapoteza samaki wale. Pale Wizarani nimejipanga na timu yangu tunanunua maguduria ya kuhifadhia samaki ili kusudi tukayagawe kwa akinamama wa ukanda mzima wa Ziwa Tanganyika ili watakapovuna yale mazao tarehe 15 Agosti, wakiwemo wale wa Katavi, wa Kigoma na wa Rukwa, wasije wakapoteza mazao yao, hili nataka niwahakikishie tutalifanya, watuunge mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama viongozi tukiwa na lugha mbilimbili itatusumbua sana na kuwapoteza hawa wananchi. Kama Serikali hatuna nia mbaya kwa sababu ni ukweli wakati wa kipindi cha Mei, Juni na Julai hiki ni kipindi cha baridi na samaki anakimbia. Anafanya hibernation; anajificha kutokana na ile baridi. Kwa hiyo, hata hawa wavuvi ukiwaambia wabaki tu. akienda hapati cha maana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwahakikishie, ni utafiti na ni jambo la uhakika siyo jambo la hila; siyo jambo la kusema kwamba tunawafanyia watu hiyana na kuwaonea. Wazo lililotolewa la kwamba tulinde mazalia ndiyo maana nikasema Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kupambana na vita dhidi ya uvuvi haramu, matumizi ya maarifa ni makubwa zaidi kuliko matumizi ya nguvu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunanunua ndege zisizo na rubani, huyo ndiyo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yaani leo Wizara ya Mifugo na Uvuvi inanunua ndege zisizo na rubani; hiyo ndiyo habari ya mjini. Tuna ndege zisizo na rubani zisizopungua saba, zile ni za high resolution, zitakuwa zikitembea umbali wa kilomita 100 kwa masaa mawili. Ndege zile zitapiga picha vyombo vyote vya uvuvi na zitatuma taarifa zile katika vituo vyetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi tutakuwa tukifanya tracking na traceability, tunakwenda kuanzisha mradi wa kufunga vyombo maalum katika kila boti ili kusudi tupate takwimu na taarifa za wavuvi wetu ambazo leo hii hatunazo. This is science na unajua uvuvi ni purely science, hata wale wavuvi walioko kule ni wanasayansi; huo ndiyo ukweli wenyewe. Kwa hiyo na sisi tunaambatanisha hilo jambo. Tunaweka drones, zinapiga picha, tukitoka katika kituo tukiwa tunakwenda kumkamata mtu tunakwenda kwa uhakika kwamba huyo mtu yuko umbali gani, kilomita ngapi, east or west; tunaenda straight katika lile eneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii itatupunguzia matumizi mabaya ya muda, lakini itapunguza pia gharama za mafuta ambazo tumekuwa tukizitumia kwa kiasi kikubwa sana. Tusingetamani kukanyagana na watu wasio na hatia; tunataka tukienda kumshuku mtu awe ni mtu ambaye kweli huyu records zinaonesha ni mvuvi haramu. Waheshimiwa Wabunge hili nimeona nilieleze kwa kina sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, wengine wamechangia juu ya migogoro ya wakulima na wafugaji na watumiaji wengine. Nimeeleza hapa jitihada ambazo tunazifanya; mmeona kwa mara ya kwanza sisi tunaingiza sokoni mbegu za malisho; kwa sababu hapo mwanzo tulikuwa tunawahamasisha wafugaji wetu kwamba pandeni malisho; lakini mfugaji anakuuliza mbegu ziko wapi? Sasa leo tunapozungumza hapa madukani tutakuwa na mbegu. Kwa hiyo, wafugaji wote waliopo katika Bunge hili nawahamasisha sana kama nilivyosema tunayo Jucow na tutakuwa na kampeni madhubuti kabisa ya kupita sehemu moja hadi nyingine ya kupanda hizi Jucow na tutapanda na nyasi nyingine ambazo labda zitamea katika hayo maeneo, siyo kila mahali nyasi ambazo zinatakiwa kupandwa zitafanana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu lazima tumshukuru sana Mheshimiwa Rais, nimewasikia hapa baadhi ya Wabunge wakizungumzia juu suala la kwa nini Wizara inakubali maeneo ya wafugaji yaondoke, lakini lazima niseme ukweli, kila mmoja hapa anafahamu juu ya Mradi wa Mawaziri Nane na Vijiji 975, ni katika zile 4Rs Mheshimiwa Rais amefanya Reconciliation kubwa sana. Siyo katika siasa tu, ametoa ardhi kubwa hapa; ardhi ya Serikali imetolewa imepelekwa kwa wafugaji wa nchi hii. Lazima tukubali na wakati tunaomba ni lazima pia tushukuru. Namshukuru sana Mheshimiwa Mwijage, pale Muleba Ranch ilikuwa ni mgogoro mkubwa sana. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia akatutuma sisi Mawaziri nane, tulikwenda pale tumeumaliza ule mgogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi leo Muleba wanasherehekea na wanataka kufuga kisasa; this is 4Rs na hiyo ndiyo nguvu ya 4Rs, reconciliation. Kwa hiyo, hii hoja ya kwamba maeneo ya wafugaji yanachukuliwa sisi tumeichukua na tutazungumza na wenzetu. Ni lazima Waheshimu GN za Serikali. Hilo halina mjadala lakini mle wanakofanya vizuri ni muhimu kushukuru na kupongeza. Ranch za NARCO zimetolewa nyingi sana kuanzia Ruvu kwenda Mkata na kwenda kila mahali katika nchi hii. West Kilimanjaro kote tumemega kwa ajili ya kuwapa wananchi ili kusudi waweze kufanya shughuli zao. Kwa hiyo, hiyo ni nguvu kubwa sana ya utayari wa Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha kwamba tunaishi kwa maridhiano, tunaishi kwa kuvumiliana; tunaishi kwa umoja na tunajenga uchumi wetu jumuishi, tunajenga uchumi wetu upya na tunasonga mbele kwa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge Ole-Shangai amesema anataka kunishikia shilingi kama sijasema kuhusiana na chanjo ya mifugo. Mheshimiwa Ole Shangai hana haja ya kushika shilingi yangu kwa sababu tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 25; tunakwenda kuchanja katika nchi hii. Hili jambo la kuchanja tulikuwa tumewaachia sekta binafsi kwa miaka mingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukubaliana juu ya kubadilisha mfumo wa uchumi katika Taifa letu miaka ile ya mwanzo wa 90, sekta binafsi ikaachiwa jambo hili la kuchanja. Hapa karibuni tumekubaliana hatuwezi kuwaacha wafugaji wa Taifa hili wawe watu wa kuonewa, kwa sababu huko barabarani kuna vishoka wengi sana. Vishoka ni wengi sana huko mtaani. Mtu mmoja yeye anatembea katika pikipiki yake: yeye ni daktari, yeye ni nesi na yeye ni kila kitu; dawa zenyewe hatuna ithibati nazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuwaondoa vishoka hawa, Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetenga zaidi ya shilingi bilioni 25 tunakwenda kuchanja. Umetaja CBPP, PPR na Newcatle zimo. Lazima tukubaliane, akinamama wengi sana kule vijijini wanafuga kuku na kwa hakika kikipita kideri/mdondo kuku wengi sana wa wale akinamama hufa na wanarudi nyuma sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapeleka hizo dawa na tutatoa ajira ya muda mfupi kwa vijana walioko mtaani wasiokuwa na kazi waliosomea shughuli za mifugo. Sisi tutakwenda kuwapa temporary jobs katika wakati ule wa kufanya shughuli hii ya chanjo, Rais Dkt. Samia hoyee, ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeeleza juu ya uvuvi haramu na Wabunge wengi hapa wamenishauri juu ya kuyalinda mazalia. Nimeeleza katika hotuba ya bajeti ya kitabu ukienda ukasoma mle utakuta tunanunua yale maboya na hizi ni stainless steels; tumeshaanza kuyafunga. Mahale kule Kigoma tumefunga, lakini zimefungwa maeneo ya Mgambo pale Uvinza na mimi mwenyewe ndiyo nilikwenda kuzifunga. Zimetengenezwa hapa Tanzania na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Faculty yetu ya Engineering.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikwenda nikiwa Naibu Waziri mwaka 2029, hata juzi nilipokwenda na kuuliza vipi yale maboya, yanaendelea kufanya kazi? Wamenambia zinafanya kazi vizuri sana. Mpaka leo hii ni miaka mitano yale maboya yanafanya kazi vizuri sana. Siyo tu pale Mgambo lakini na Muyobozi mpaka huko Buhingu kama unaenda Kalya; hiyo ni Uvinza na wavuvi wanaheshimu ile mipaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tutakwenda kufanya hivyo Ziwa Victoria; tutalinda yale mazalia. Tutaendelea kufanya hivyo Ziwa Tanganyika na kwa mwaka huu tumetenga fedha na tunakwenda kununua haya maboya; tunakwenda kulinda yale maeneo yote ya mazalia. Tunayatangaza katika Gazeti la Serikali atakayekwenda kugusa eneo lile ama zake ama zetu hatutamuacha salama kwa sababu tukilinda yale mazalia vizuri stock ya samaki wetu itaongezeka sana. Kwa hiyo, nataka tupate ushirikiano na naamini Bunge hili kwa namna lilivyokasirishwa na vitendo haramu vya rasilimali zetu, watatuunga mkono, ahsanteni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu vizimba na boti; boti zinatoka kutoka 160, Rais ameridhia tunapeleka mpaka 450, wavuvi wa nchi hii tupewe nini? Zile boti zinafungwa mpaka tracking systems, mle ndani kuna nyavu, GPS na mpaka kile kipampu cha kutolea maji. Lazima tukubaliane reformation and rebuilding ya hii sekta, Rais Dkt. Samia amepania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, wale Wabunge wote ambao wana mahitaji ya hivi vifaa akiwemo ndugu yangu, kaka yangu Mheshimiwa Mpembenwe, alisema mwanzoni kabisa akanikumbusha kwamba, wale wapiga kura wa kule Maparoni, Kiongoroni, Mbuchi, Mtunda, Salale na Nyamisati wote wanataka haya maboti. Kaka ahakikishe kwamba, anawaandaa wapiga kura wetu wa eneo hilo wakidhi vigezo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme hapa katika Bunge hili ya kwamba, kazi ya kuandaa yale maandiko siyo kazi ya wale wavuvi. Mmoja katika wasemaji hapa amesema vizuri, wavuvi hawana hayo maarifa, Mabwana Samaki walioko kule vijijini ndiyo watu wanaopaswa kuwaelekeza wavuvi wetu ni hatua gani ya kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa maelezo hapa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wetu, bahati nzuri wengi wameipokea hii vizuri sana, wawaelekeze Mabwana Samaki. Isiwe kazi yao wao ni kwenda kunyang’anya ushuru tu. Watoe michango ya kimaendeleo kwa wavuvi wetu ili kusudi wale wavuvi wapate hizi fursa zinazotolewa, wapate kunufaika na hizi fursa ambazo Serikali yetu ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inazozitoa. Kwa hivyo, nimewasikia Wabunge wote mnahitaji haya maboti. Maboti 450 ni mengi, nataka niwahakikishie, leteni maombi mumkabidhi Naibu Waziri, mnikabidhi mimi, mumkabidhi Katibu Mkuu na yeyote mnayemjua katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Nataka niwahakikishie maboti ya kisasa yatapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu ni mtu hakopeshwi boti isipokuwa tunajadiliana anataka boti la size gani. Sisi tunayo ya mita tano, mita saba, mita kumi, mita kumi na mbili na mita kumi na nne kwa hivyo, mvuvi ana-shop yeye mwenyewe. Kwa sababu, huu ni mkopo kwa hiyo, sisi hatumlazimishi, sisi hatumuamulii. Wewe unakubaliana na maafisa wetu unataka boti la aina gani na size gani, huu ndiyo utaratibu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nimefurahi sana kwa majibu ya Naibu Waziri aliposema, kama kuna jambo specific ambalo Mbunge ameletewa kama malalamiko, sisi tuko tayari kupokea yale malalamiko, ili kusudi yule mvuvi asiende kulipa kitu asichostahiki. Kwa sababu, mwisho wa siku ule ni mkopo na kwa hivyo, anahitajika afanye lile jambo katika utaratibu ulio sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya Wabunge wameshauri hapa ya kwamba, maeneo ya ukulima wa mpunga tupande na samaki. Namshukuru sana kaka yangu Mheshimiwa Hussein Bashe, Waziri wa Kilimo, mimi na yeye tumekubaliana Na Kwa kuwa, Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni moja, tunafanya kazi kama mwili mmoja, ndiyo. Nataka niwaambie tunafanya kazi pamoja, kiungo chochote kikipata hitilafu mwili mzima unaharibikiwa, ndivyo kama kidole kimekatika basi mpaka kichwa kinauma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kusema hivi Wizara ya Kilimo inatengeneza skimu za umwagiliaji. Ninayo barua hapa ya mwandamizi, Waziri wa zamani wa Ardhi, mzee wangu Mheshimiwa Lukuvi anasema, Pawaga na pale Isimani, Idodi, wanataka tuwatengenezee mabwawa ya samaki. Sasa kwa sababu, pesa hizi za Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kutengeneza skimu za umwagiliaji sisi tumefunga mkataba wa kushirikiana. Palipo na skimu ya umwagiliaji tunakwenda na mambo mawili, kila unapoona skimu ya umwagiliaji tunatoa ember-out na pia, tunatoa mabirika ya wafugaji kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kufanya jambo moja la kuwafaa Watanzania kwa gharama ya Watanzania, huyu anafanya chake na huyu anafanya chake. Tunafanya kwa pamoja ndiyo maana katika miradi hii yote vijiji hivi alivyovitaja mzee wangu Mheshimiwa Lukuvi, nataka nimhakikishie yeye na Wabunge wengine wote ya kwamba, katika skimu zile za umwagiliaji tunatoa ember-out kwa maana ya lile birika la kunyweshea maji. Vilevile, tunaenda mbele zaidi tunapandikiza na samaki, unavuna mpunga na unavuna sato. Halafu ukikaa pale mezani mambo ni mazuri sana kwa hivyo, kila Mbunge mwenye skimu ya umwagiliaji ananidai mbegu za kupandikiza za samaki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Profesa. Ndakidemi, ameibua hoja hii na wengine wamesema. Mzee aje achukue vifaranga vyake vya samaki, twende tukapandikize, wakiwa wanavuliwa baada ya miezi mitatu, minne tualike au tupigie hata picha tuone ukubwa wa yule sato atakavyokuwa amenenepa. Halafu wakivuna ule mpunga, wakiweka pale mezani inabakia kazi moja tu ya kusubiri mwaka 2025, watu watakichagua tena chama ambacho kinawaongoza vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, baadhi ya Wabunge humu wamezungumza juu ya upatikanaji wa maji ya kunywa mifugo yetu. Narudi tena katika hoja ile ile, namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu wetu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa na Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko. Wakati wote msisitizo wao umekuwa ni tusifanye jambo moja huyu kivyake na yule kivyake. Na sisi tumelishika jambo hili ndiyo maana mimi na ndugu yangu Aweso penye mradi wa maji ya kunywa binadamu tunapeleka na maji ya kunywa mifugo pia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Aweso ana mabwawa 100, fedha zile ni za kwetu sisi Watanzania. Ya kazi gani mfugaji aliyeko pale ahangaike kwenda kilomita 100 kwenda kuyasaka maji wakati maji yako mahali palepale? Kwa nini, asitengeneze ember-out?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hii miradi yote ya skimu za umwagiliaji, miradi yote ya maji ya kunywa binadamu, kama iko mifugo pale, imefanyiwa design ya kutoa yale maji, kwa ajili ya mifugo yetu. Mifugo yetu ni hazina yetu na utajiri wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ununuzi wa meli. Je, hizo meli ni nane, nne, tano au ngapi? Mheshimiwa Tunza Malapo ameuliza. Meli ni nane, nne Tanzania bara na nne Tanzania Visiwani. Visiwani watanunua upande wa visiwani, Zanzibar, na sisi tutanunua nne za kwetu. Tumekubaliana na ninamshukuru sana Mheshimiwa Chief Whip wetu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mama yangu Jenista Mhagama, ametuongoza vizuri sana katika hili jambo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumefikia makubaliano. Mwanzoni hili jambo lilikuwa linaratibiwa na Wizara moja kwa moja, lakini sasa tumelitoa kwa mashirika yetu Tanzania kwa maana ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, TAFICO, watakwenda kutangaza tenda ya kwenda kununua hizi meli nne. Kwa upande wa Zanzibar, ZAFICO watafanya wao wenyewe. Siyo jambo liwe centralized Wizarani kwa sababu, tunataka wapate ufanisi. Wapate wanachokitaka, wapate kitu ambacho kitawazalishia na ndiyo maana wakati natoa hotuba hapa nimesema TAFICO inafufuka. Kwa hivyo, meli ni nne. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kilichotuchelewesha ni wahisani ambao tunashirikiana nao, IFAD, kwa maana ya wale wanaotukopesha hizi pesa. Hawa wahisani wetu walitaka ni lazima tufanye environmental and social impact assessment ya namna ambavyo tutaendesha pamoja na feasibility study kwa sababu, TAFICO hataendesha yeye mwenyewe pia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekubaliana itakuwa ni PPP, tunakaribisha sekta binafsi. TAFICO bado ni Shirika la Serikali, meli ile akiiendesha TAFICO, yule mkurugenzi kikiharibika kifaa, yataanza yale yale ya kuanza kutafuta hicho kifaa, dokezo litoke kwangu, liende kwa yule, liende kwa yule, meli imesimama pale. Tunataka sekta binafsi ifanye kazi hiyo. Hakika nawaambia hii ni kwa ajili tu ya kuvutia kwa sababu, hii kazi itafanywa zaidi na sekta binafsi, lakini sisi tunataka tuiaminishe kwanza sekta binafsi ili ivutike na baadaye ije ituunge mkono, haya ndiyo malengo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu bila ya sisi wenyewe kuwa na national fleet, bila ya kuwa na meli ya kwetu, sisi wenyewe ni nani huyo atakayekuja pembeni akatuamini kwamba, tunayo mazao ya kutosha? Ndiyo maana tukasema TAFICO itaanza. Kwa hiyo, dada yangu Tunza na Wabunge wote mjue tu kwamba, kazi hii inaendelea vyema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wamezungumzia juu ya Mamlaka za Mifugo na Uvuvi. Ni kweli jambo hili Wabunge wamekuwa wakilisema sana na sisi tunafanya jitihada kubwa. Kamati yetu ya Bunge imetusukuma ipasavyo juu ya jambo hili. Jambo limefikia mahali pazuri sana, msiwe na hofu, na sasa tunakwenda katika kulimaliza hili jambo. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri omba pesa.
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mwisho nimalizie na hoja ya ujenzi wa Bandari ya Kilwa-Masoko. Kwa kweli, tunashukuru sana 53% si haba, na tunakwenda vizuri mno na sasa tunakwenda kuimaliza. Itakuwa ni bandari ya mfano na hiyo inakwenda kutufungulia bandari nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka tufungue huu Ukanda wa Mashariki, tuweke viwanda vya kutosha na meli zote za kimataifa zije Tanzania kwa hiyo, tutakuwa na ile ya pale Bagamoyo vilevile. Huo ndiyo mpango wetu, siyo ziende huko kwingine, zitakuja hapa Tanzania. Tunayo maji ya kutosha na tutatumia vyema fursa ya uwepo wa haya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema haya, naomba kutoa taarifa kuwa Bunge lako lilikaa kama Kamati…
NAIBU SPIKA: Aahh, haa. (Kicheko)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, bado? Aah, okay.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema haya na ufafanuzi wote nilioutoa hapa, ninayo matumaini. Waheshimiwa Wabunge nawaomba kwa heshima kubwa na taadhima mtuunge mkono twende tukafanye kazi, tukafufue na tukaendeleze vyema sekta hizi za mifugo na uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2024/2025, Wizara inaomba kutumia jumla ya shilingi 460,333,602,000. Kati ya fedha hizo, shilingi 97,215,432,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 363,118,170,000 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Mchanganuo ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za matumizi ya kawaida ni shilingi 97,215,432,000…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri inatosha, toa Hoja.
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)