Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Musoma Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nashukuru kupata nafasi ya kutoa mchango wangu, labda tutulizane kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naipongeza Wizara, hii kazi wanayoifanya ni kubwa kweli kweli, lazima tuwapongeze. Tuipongeze Serikali yetu na Mheshimiwa Rais kwa zoezi hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninachoanza kuwashauri ni naiomba Wizara ipitie historia ya mabadiliko ya elimu hapa nchini na hasa waanze kwenye kipindi, tunapata uhuru na miaka 10 ya kwanza ya uhuru, Mwalimu alifanya mabadiliko katika hiyo miaka 10. Kwa nini inabidi wapitie hapo? Ni kwa sababu inawasaidia kujua mahala ambapo hapakufanikiwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu wakati anafanya mabadiliko kati ya mwaka 1961 na 1971 toka kwa zilizokuwa shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu, alikuwa na Wizara moja tu ya Elimu na ukiangalia alivyokuwa amepanga Wizara ya Elimu ndiyo ilikuwa karibu sana na Ikulu. Bajeti ya Mwalimu karibu 20% mpaka 30% ya bajeti ilikuwa inapelekwa elimu. Alifuta darasa la nane, alitaifisha shule na shule zilikuwa na walimu kweli kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka shule yangu ilivyotaifishwa mwalimu wangu wa English wa form one alienda kufundisha English Makerere University, alikuwa anaitwa Brother Richard. Mwalimu alifuta Mitihani ya Cambridge ya Commonwealth. Kwa hiyo hii kazi tunayoifanya ni kubwa, tuwaunge mkono na tuisaidie Serikali, lakini watu wanabadilisha mitaala siyo tu kwa sababu ya kubadilisha mitaala. Kwenye karne ya 20 na 21 kila Taifa linajitahidi liyashinde Mataifa mengine kwenye nyaja ya teknolojia, sayansi na ubunifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha pili, ni kila Taifa linataka lipate bidhaa nyingi sana za kuuza, export oriented economic strategy. Ili kufanya hayo yafanikiwe vitu vitatu vinahitajika, mfumo wa elimu uwe mzuri ndiyo tunauongelea, Taifa liwe la watu walioelimika ni muhimu sana kuwa na educated population, halafu na wananchi wawe na ari ya kuleta maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimechukua mifano miwili tu wakati najaribu kutafakari mabadiliko yetu. Je, tuko sawa awa? Je, ni ya muhimu kufanyika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukichukua hiyo mifano usichukue mifano kwa watu ambao ni dhaifu, lazima uende kwenye Mataifa ambayo siyo dhaifu, lakini ambayo mnafananafanana, kwa hiyo, nimechukua mfano wa kwanza wa Seychelles. Seychelles ni kakisiwa kadogo, lakini tutatumia ratios proportion kulinganisha, mtu asije kusema Seychelles ni wachache, hapana ni suala la statistics ratios.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Seychelles kwa sababu ndiyo Taifa tajiri namba moja Afrika, GDP yake ni zaidi ya dola 20,000, hivyo ni vigezo vya World Bank na IMF, lakini kuna kigezo cha pili ambacho hatukitumii sana, HDI yaani Human Development Index. Sasa nikianza kueleza hiki muda wangu wote utaishia huku. Kwa kifupi ni kwamba, hiyo ndiyo inatoa kipimo cha maisha bora ya kila Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Seychelles ni nchi pekee kwa Afrika ambayo ipo ngazi za juu, HDI yake ni 0.802, Tanzania ni 0.532 na Kenya wanatuzidi wao ni 0.601. Sasa angalia mtindo wao wa elimu, wao wana sita, tatu, nne, nne (six, three, four, four) maana yake ni hivi, primary school wanaenda miaka sita, lower primary school miaka mitatu, upper primary school miaka minne na chuo kikuu ni miaka minne. Kwa hiyo, unaona ni karibu tunalinganalingana na mabadiliko ambayo Wizara ya Elimu imetuletea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilivyoacha Bara la Afrika nikaenda Bara la Asia ambalo limeendelea, Asia imeendelea kwelikweli, kule nimechukua South Korea. South Korea GDP yake per capita ni zaidi ya dola 32,000, HDI yake ni 0.717. Sasa angalia mtindo wake wa elimu, South Korea ni sita, tatu, tatu, nne; maana yake ni kwamba, kama mtu anaenda moja kwa moja, elementary school ni miaka sita, middle school ni miaka mitatu, high school ni miaka mitatu na chuo kikuu ni miaka minne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo ambao hawaendi chuo kikuu wanaenda kama sisi VETA, wao wanaita junior colleges, hao wanaenda kwa miaka miwili mpaka mitatu. Kwa hiyo, kwa kulinganisha Afrika, nasema kwamba, Tanzania mabadiliko yetu ni sahihi. Sasa natoa ushauri, kwanza ni lazima tukajipime kimataifa kwa haya tunayoyafanya, maana tunaweza tukajisifia sisi wenyewe tu, lakini twende huko tukajipime. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipimo cha kwanza naomba Tanzania ishiriki kwenye kitu kinaitwa PISA, siyo pizza. Maana yake ni Program for International Student Assessment, hii inapima watoto wenye miaka 15 kama mambo waliyojifunza shuleni yanaweza kutatua matatizo yanayowazunguka duniani, twende huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipimo cha pili ni TIMSS, yaani Trans International Mathematics and Science Study. Hii inachuka watoto walioko kwenye grade ya nane, wanaangalia ujuzi wao na maarifa waliyopata shuleni. Sasa haya ni mashindano yanayofanywa Kitaifa na Tanzania, naomba baada ya miaka miwili mitatu, Mheshimiwa Profesa aende kule PISA na TIMSS ndiyo tutajua kwamba, tuko sahihi, vijana wetu wa miaka 15 wakapambane kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili ni juu ya mambo yote tunayofanya. Naomba Mheshimiwa Profesa kwa sababu, hivi vitu unavifahamu uende ukafufue professional societies ambazo zimekufa kwa sababu, haya matatizo ya hisabati tungewapatia Chama cha Hisabati cha Tanzania. Matatizo ya chemistry, huwezi ukajadili tu mambo ya chemistry, wapatie hicho chama. Kwa hiyo, Waziri akafufue hizi, tena ni the cheapest consultant bodies. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa tatu ambao kusema kweli, naomba kusema ni kwamba, sikuafiki sana, ni haya ya tahasusi za form five na form six yaani combinations. Nimeangalia Profesa anazo 65, combinations 65 kwenye high schools na nimejaribu kuzichambua; Sayansi ya Jamii combinations tisa, ni 13.8%; Lugha combinations 11, ni 16.9%; Biashara saba, ni 10.8%; Sayansi saba, ni 10.8%; Michezo saba, ni 10.8%, Sanaa/Arts 16, ni 24.6%; na Elimu ya Dini ni nane, ni 12.3%. Kwa hiyo, ukichukua haya mapendekezo hizi combinations walizozifikia ukichukua vyumba viwili vya science na arts, hapa hatutayarishi Taifa kwenda kwenye science.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafunzi wengi watajaa chuo kikuu, tutakuwa na wanafunzi wengi kwelikweli chuo kikuu, lakini katika hao ambao watakuwa wanasoma real science ni asilimia 10 tu. Kwa hiyo, kama tunataka kwenda kwenye science na technology ni lazima tubadilishe hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni la chuo kikuu, muda hautoshi. Vyuo vikuu vyetu, ndugu zangu, Mheshimiwa Profesa siyo kazi yako. Mtu akiitwa Profesa inafaa ajitegemee, ajitume, atafute fedha mwenyewe, lakini akishindwa inabidi tumlee, lakini vyuo vyetu vikuu vya sasa hivi vimekuwa nationalistic, yaani ni vya Kitanzania mno, havina afya kitaaluma. Havina afya kwa sababu, huwezi kukuta Maprofesa wametoka nchi nyingine kama visiting professors wapo kwenye vyuo vyetu, huwakuti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kuhusu External Examiners. Nilivyokuwa bado mwanafunzi alikuwa anatoka Cambridge, Uingereza. Sasa hivi hawa wa madini, nadhani External Examiner, wanaweza kwenda kumchukua mchimbaji mdogo mdogo Musoma? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia juu ya exchange programs. Exchange programs kwa wanafunzi ni lazima ziwepo na mwisho ni training schools, hii ni muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo namalizia na wala sitakuomba muda. Nachukua jinsi nilivyojifunza geology miaka mitatu hapa hapa Tanzania na sasa hivi geology ni miaka minne. Nilivyokuwa mwanafunzi kila Jumamosi tulikuwa tunaenda field halafu tulivyomaliza mwaka wa kwanza, tukazunguka maeneo mbalimbali tunafanya mapping.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka wa pili, nilienda kufanya mazoezi Zambia, tukaandika ripoti. Sasa Mheshimiwa Profesa tatizo lingine ni hii ya wanafunzi kujitegemea, ni lazima uwekeze hela nyingi ili wanafunzi wakafanye professional training, ndiyo maana wanafunzi wa wakati huo, hata wanafunzi wangu, wameenda kufanya kazi Ghana na Australia wanakubalika, lakini wa sasa hivi hawawezi kukubalika huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)