Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Thea Medard Ntara

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, napata shida kidogo, wamezungumza maprofesa sasa naomba nami nifuatefuate mkondo huo wa maprofesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Wizara ya Elimu; Mheshimiwa Profesa Mkenda pamoja na Mheshimiwa Omari, Watendaji wote wa Wizara hasa katika taasisi mbalimbali chini yake kwa kazi nzuri wanayoifanya. Kuna mambo machache tu ambayo bado inabidi tuyasemee katika kuboresha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitaanza kwa kupongeza sana sana, suala la uboreshaji wa elimu kwa ujumla nikianza na majengo ya vyuo pamoja na maslahi kwa mikopo. Katika uboreshaji Kamati ilipita kuangalia haya majengo yaliyoongezwa katika vyuo, lakini niseme tu kwa masikitiko kile Chuo cha Nyerere Kigamboni, Unguja pamoja na Pemba bado Wizara inatakiwa iweke nguvu kwenye vyuo hivyo. Ujenzi au uboreshaji wa majengo unakwenda polepole sana, sasa sijui ni fedha bado haziendi huko, hatuelewi lakini sisi tunachotaka kuona pale majengo hayo yanaenda kwa speed pamoja na Nelson Mandela bado ujenzi wake haufurahishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye uboreshaji wa mikopo; Serikali imejitahidi sana kuongeza fedha za mikopo karibu shilingi bilioni 700, lakini kwenye bajeti ya elimu kuna ile shilingi trilioni 1.9. Maana yake ni hivi, kiwango kikubwa ndani ya hiyo trilioni kinakwenda kwenye mikopo. Sasa maana yake ni hivi ingawa 60% inaenda kwenye mikopo, lakini bado mikopo hiyo haitoshi, kwa hiyo zinazobaki zinakwenda kwenye maendeleo. Ndiyo maana tunasema Serikali inabidi iongeze fedha za maendeleo kwenye Wizara ya Elimu lakini pia fedha za mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo mikopo tumeweka ni sheria, hao wanafunzi wana haki ya kupata hiyo mikopo. Kwa hiyo, sisi tunasisitiza kwamba Serikali itafute mbinu, Bodi ya Mikopo itafute mbinu ya kuongeza fedha kiasi ambacho kisaidie watoto wetu wote wanaostahili wapate mikopo hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye suala ambalo nimelizungumza toka naingia Bunge hili 2020, wakati tunaanza Bunge 2021, kuhusu suala linalohusu teaching hospitals. Vyuo vyote au nchi zote universities zikiwa na teaching hospitals ndio zinazofanya vizuri sana. Teaching hospitals pamoja na military hospitals yaani hospitali za kijeshi pamoja na hizo teaching hospitals za university ni katika hospitali zinazofanya vizuri sana. Ninachoshangaa mpaka leo, hivi kuna mvutano gani kati ya Muhimbili na Mloganzila? Kuna mtu mmoja tu pale sijui niseme ni Mkurugenzi, hataki kuwapa Mloganzila University waichukue kama teaching hospital.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kigugumizi gani hapo ni suala la maslahi au ni nini? Leo hii mwalimu aliyekuwa anafundisha hapo UDOM, Mhadhiri aliyekuwa anafundisha UDOM ndiye yule aliyesaidia kugundua upandikizaji wa uti wa mgongo, tunaita uboho, uboho mnisikilize vizuri, aliyesaidia ni huyo Mhadhiri kutoka UDOM. Sasa leo wanaposema hatuwezi kuziachia hospitali vyuo vikuu wakati wataalam ndiyo wanatoka kwenye hivyo vyuo, haileti afya kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba watakapokuja hapa waniambie Wizara ya Elimu wana shida gani na Wizara ya Afya. Kwa nini wasikae pamoja wakaangalia? Tulikwenda pale Mloganzila kuna mambo nusu yanafanyika na MUHAS, nusu wamewaachia hiyo University yaani wala havieleweki. Niombe suala hilo la teaching hospital sasa lifikie mwisho. Kama wamewanyang’anya Mloganzila, kama wamewanyang’anya Benjamini, basi wajipange sasa, Waziri wa Mipango yuko hapa, wajipange watuambie au wanawajengea teaching hospital zao wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye maslahi na hilo nimelizungumza, hawa wakuu wa vyuo…

MHE. DKT. BASHIRU A. KAKURWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Kuna taarifa Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara. Taarifa, Mheshimiwa Dkt. Bashiru.

TAARIFA

MHE. DKT. BASHIRU A. KAKURWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa taarifa kwamba kwenye Ilani hii ya Chama Cha Mapinduzi tumeahidi teaching hospitals. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri na Serikali wajipange ama wawarudishie hizo hospitali zilizopo au wawajengee hospitali za mafunzo. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara, unaipokea hiyo taarifa?

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea, ahsante sana daktari mbobezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nije kwenye maslahi; nimezungumza kuhusu maslahi ya wakuu wa vyuo. Hawa watu wanakaa wanaangalia watoto pamoja na kufundisha, wanaangalia na discipline katika vyuo vyetu. Sasa hivi Waheshimiwa Wabunge watanikubalia kwamba vyuo vikuu vimetulia na kazi kubwa wanaifanya hao wakuu wa vyuo. Leo hii kuna mmoja aliongea hapa wiki iliyopita, aliongea kwamba hata ukiangalia sijui hizo per diem yaani maslahi yao wanalipwa chini, halafu kuna walimu pale pale wanafundisha nao. Hivi kweli kutakuwa na kuheshimiana kweli? Hebu tuangalie haya maslahi. Waliniambia kwamba hili suala tumelichukua tunalipeleka, tunalichukua tunalipeleka, leo wanalichukua wanaliweka wapi? Naomba suala hili walichukue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu wametulia tu wenyewe hawa ma-VC, maprofesa wametulia hawana kelele, wamekaa lakini wanaumia moyoni, hatuwatendei haki. Profesa anajua, hatuwatendei haki, wapo wametulia lakini wanaumia. Hamjasikia wanaandamana wala wanagoma, wanaenda wanafanya kazi zao, hebu leo hilo suala lifike mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naongea kama wenzangu pia nasisitiza umuhimu sasa wa kuona tunaongeza muda wa ku-retire. Leo wanalalamika hapa yaani Tanzania nzima tuna maprofesa 93 imagine na tunatakiwa tuwe na maprofesa 516, lakini full professors hao tunao 93 tu. Hebu wafikirie, halafu wakifika miaka 70 wanasema waondoke wengine hawajawajenga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko mimi nilifanya study yangu, wakati na-study, profesa aliyekuwa ananisimamia mimi alikuwa na miaka 85 and he was very good upstairs. Waongeze retirement halafu wahakikishe kwamba wanawaleta na maprofesa kutoka nje kama alivyosema Profesa Muhongo. Tuna maprofesa hapa ukifika Chuo Kikuu unakuta Profesa Komba, Profesa Kiwia, Profesa sijui Haule. Tunataka ukifika unakuta mchanganyiko wa maprofesa, Profesa Hoffman, Profesa sijui San Chan, lazima tuwape uhuru universities waajiri maprofesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashauri tu maprofesa au Waziri kwamba hata vyuo vyetu jamani exchange programme siyo lazima uende nje. Mtu anakaa anasoma pale UDSM miaka minne, hebu tutengeneze exchange programme za hapa ndani. Aende hata pale MUST kijana anakaa pale anasoma mambo, anatembelea UDOM yaani wanabadilishana within our universities. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nililisema kwamba hebu kila university ijitahidi kulea jiji au halmashauri ili tuone ule utafiti wanaofanya uonekane kule…

(Hapa kengele ililia kuashira kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nusu dakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nimwombe Mheshimiwa Waziri, sasa hivi tunasema watoto, hawa watoto pia ni watoto wake. Wizara ya Elimu ihakikishe kwamba unafuta kabisa haya mambo ya watoto kupelekwa kuchezwa au unyago wakiwa wadogo. Haya mambo yanaharibu, hawa ni watoto wake, wao wasome shule siyo watoto wadogo, darasa la kwanza mpaka la tatu wanapelekwa kuchezwa hasa mikoa hii ya kusini. Watoto wanachezwa, hawa ni watoto wake awalinde Mheshimiwa Profesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nawashukuru sana, nasema ahsante sana. (Makofi)