Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vunjo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ili nichangie kwenye hili jambo ambalo ni la msingi. Ni sekta ambayo inagusa kila mtu katika nchi hii na hata nje ya nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanaothubutu kutekeleza mambo magumu ni wachache sana hapa duniani na naomba niseme kwamba Mheshimiwa Rais wetu kweli ana uthubutu…
MWENYEKITI: Waheshimiwa naomba tutulie, tumtazame na tumsikilize Mheshimiwa.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tumpongeze sana kwa kukubali kutengeneza sera mpya na mitaala mipya ambayo itaenda kubadilisha kabisa mfumo wa elimu nchini. Mfumo siyo kitu rahisi sana kubadilisha ni kitu kigumu na ni kitu ambacho ni nyeti, ni kitu ambacho lazima kweli twende kwa usahihi wake. Profesa Muhongo alituelimisha hapa lakini nataka niseme kwamba ni kitu cha msingi sana, kwa hiyo tukichezea tutakuwa tumeharibu sana shughuli zote hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Profesa Mkenda na Naibu wake Mheshimiwa Omari na Timu yake yote kwa kazi ambayo wanafanya, tunaiona. Najua ni ngumu lakini kama anapata usingizi, basi naye ni mtu anayethubutu sana, lakini ukweli ni kazi ngumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sitaki kuingia kwenye viatu vya wale maprofesa walioanza kuzungumza. Nianze kwenye jimbo langu, kule kwenye jimbo langu nina wakazi 255,000 na hatuna Chuo cha Ufundi cha VETA, ina maana kwamba mwanafunzi aliyemaliza shule ya msingi au sekondari akitaka kupata mafunzo ya ufundi lazima atumie shilingi elfu nne mpaka elfu kumi kwenda Moshi Manispaa ambako ndiko karibu vyuo vyote vya VETA vimewekwa. Sasa naomba sana kwamba kusema kweli hili halitatufikisha mbali, naomba sana Serikali ione namna gani ya kutupa fedha tuweze kujenga angalau chuo kimoja cha VETA kwenye Jimbo langu la Vunjo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna shule moja pale kwenye kata ya Mwika Kaskazini inaitwa Shule ya Lole ilikuwa shule ya awali, msingi na ufundi wa VETA lakini kuanzia mwaka 2000 shule hii haijatoa tena masomo ya ufundi kwa sababu imekosa walimu na karakana zake zimekuwa ni chakavu sana. Pia, majengo yale hayafai yanastahili kupata ukarabati ili tukipata na walimu basi tunaweza pia kuanza shughuli ya kuanza kufundisha vijana pale. Hayo ni ya Vunjo, ya Vunjo yako mengi lakini ngoja niseme hayo mawili ili niweze kuzungumza na mengine ambayo nafikiri ni ya muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyozungumza Mheshimiwa Profesa Muhongo, lakini kitu ambacho hakukisema nafikiri ni ile nadharia ya education for Self-reliance ilikuwa inalenga sera hii hii ambayo tunataka kutengeneza sasa hivi, isipokuwa kwa namna moja au nyingine tulitekeleza bila kuwa consistent na bila maandalizi ya kutosha. Kwa hiyo ikaonekana baadaye tuka-abandoned ule mfumo wa education for self-reliance ambapo watu walijifunza nadharia, lakini na vitendo pia vilikuwepo. Nakumbuka tulikuwa tunalima sana, lakini hatukuibuka kuwa wakulima wazuri kama tulivyotarajiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nasema kwamba tumejaribu lakini tukashindwa, tukaacha tukarudi kule kule, kwa sababu mfumo ni vigumu sana kutekeleza na unahitaji rasilimali nyingi ya fedha na watu. Kwa hiyo, nasema kwamba, sidhani kama bajeti ambayo imetengwa na hata hii nimekuwa naiangalia, haitatosheleza. Kama kweli tunataka kwenda na kasi ambayo Mheshimiwa Rais anaonesha, anataka kwenda nayo na Wizara inataka kuonesha kwamba inaweza kwenda nayo, basi ni lazima tutenge fedha za kutosha kutengeneza miundombinu ambayo inastahili hususan kwenye mkondo wa amali ili watu waweze kujiandaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu ya sasa siyo ile ya zamani, naona wanazungumzia masuala ya seremala na masuala ya ufundi uwashi, sasa hivi kwenye mkondo wa amali tunahitaji kwenda na teknolojia ili tujue kwamba kama ni ufundi wa magari siyo yale magari ambayo unachochea, ni magari ambayo yanatumia umeme na mfumo wa kidijitali ambao ni wa kisasa, hivyo hawa vijana lazima waandaliwe na vifaa kwenye zile karakana ni lazima viendane na mahitaji hayo ya sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kama tutaenda kujenga ili mradi tunajenga madarasa na kuweka vifaa vya zamani ambavyo ni vizito sana, hatutafika mbali, by the time tunafika kule utakuta wale vijana hawatapata kazi na hataweza kujiajiri kwa sababu hakutakuwa na mahitaji hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti inaonekana haitoshi, kwa sababu gani? Ukiangalia data zilizo kwenye randama, kwa mfano, nalenga tu kwenye upande huu wa mkondo wa amali. Katika mwaka uliopita wameongeza uandikishaji wa wanavyuo lakini kwa upande wa technical education training utakuta kwamba shule ziliongezeka na ndizo zilizoongeza wanachuo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya shule za TET (Technical Education Training) zilikuwa 465 Mwaka wa Fedha 2022/2023, zikaongezeka zikafika jumla ya vyuo 474, vimeongezeka vyuo tisa kwenye huo mwaka ambao tunatekeleza bajeti yake, kati ya hivyo Serikali haikuongeza chuo hata kimoja, vyuo vyote tisa vimetokana na private sector. Sasa, kama kweli tunajenga huo mkondo tutaujenga bila kuongeza vyuo na tutategemea private sector?
Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo katika VETA. Vyuo vya VETA jumla vilikuwa 687 ilipofika Juni, 2023. Katika miezi hii tisa vimeongezeka 145 na kufikia 830. Kati ya hivyo nyongeza ya 145 Serikali imeongeza chuo kimoja tu na vyuo vingine 144 ni vya sekta binafsi. Sasa najiuliza kwamba, je ni kweli kuna nia ya kwenda na kasi hiyo ambayo inastahili? Tunataka 2027 tuanze kutekeleza full-blown? nafikiri tunahitaji bajeti sana kwenye suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba strategy bila kuwa na execution inakuwa ni ngumu sana kufika mbali. Kwa hiyo, nafikiri lazima watu wajipange zaidi na pengine tujaribu kuiga ili kuona hawa wenzetu wamefanyaje katika nchi zile. Seychelles ambayo ameitaja Mheshimiwa Muhongo iko juu sana, kwa Afrika ni namba moja kwa mfumo bora wa elimu. Kwa hiyo, tujaribu kujifunza ni kitu gani na wametekelezaje ili tusije tukarudia makosa na nafikiri kule tulikotoka tungeweza kwenda incrementally tukaboresha ile Sera ya Education for Self-Reliance, halafu tukaiongezea vitu vingine ambavyo havikuwepo hususani kuboresha namna karakana ambazo zilikuwa zinatumika, zile workshops kwenye shule zetu zilizokuwepo middle schools, tungeenda vile pengine tungekuwa tuko mbali zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)