Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Elimu. Awali ya yote napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuangalia na kujali sana Sekta ya Elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nawapongeza Waziri, Naibu Waziri pamoja na timu nzima ya Wizara ya Elimu. Kazi inayofanyika katika elimu inaonekana, inatambulika na tunaona kabisa kasi ya kuwa na wasomi waliobora katika nchi yetu hii inaonekana. Kazi tunayofanya sasa hivi kama ni nyumba tuna mwaga maji juu ya bati ili kubaini wapi kuna matundu. Kwa hiyo nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu leo utajielekeza kwa vyuo vyetu vikuu. Wameongea wachangiaji wengi na jambo linapojirudiarudia linamaanisha kwamba hapo kuna changamoto; nianze na mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mikopo Mheshimiwa Waziri ni changamoto. Mikopo hii wanafunzi wenye stahiki wengi hawapati. Mwanafunzi ana vigezo vyote, dirisha la kwanza hapati masomo yameanza anaambiwa subiri dirisha la pili. Anasubiri hana raha kisaikolojia anaathirika dirisha la pili bado anaambiwa subiri dirisha la tatu, kuna shida gani? Kama ana vigezo vyote Mheshimiwa Waziri na timu na Afisa Mikopo leo yuko hapa kuna tatizo gani wanafunzi wenye vigezo kupata mikopo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi wanafunzi wanapata mikopo nusu. Kuna chuo kimoja jana niliongea na Mshauri, wanafunzi wawili; mmoja yeye amepata mkopo wa chakula pamoja na malazi, lakini ada hajapata, hawezi kufanya registration hawezi kusajiliwa. Akachukua ile hela ya chakula na ile ya malazi akapeleka kwenye ada. Sasa anakula mlo mmoja wa jioni tu. Huyu ni daktari hapati chai asubuhi wala mchana hapati chakula, anakwenda kwa huyu Mshauri akilia. Jamani hawa wanafunzi wa vyuo vikuu ni watu wazima. Mtu mzima anakwenda ofisini analia hajapata fedha amepata nusu kuna changamoto gani tukiwapa kwa sababu huu ni mkopo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mwingine siku hiyohiyo ya jana yeye amepewa ada hajapata hela ya malazi, hajapata chakula. Anakwenda vilevile akilia analalamika. Sasa ataishije ameishia kubaki kwenye mikopo ambayo binafsi inatia uchungu kama uchungu wa masuala ya kausha damu. Mwanafunzi huyu atasoma nini? Anakuja kuwa daktari vipi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kulingana na muda niseme tu kwamba ofisi za wahadhiri. Ni kweli juhudi ni kubwa, inaonekana ofisi zinajengwa katika vyuo vikuu, nipongeze sana Wizara kwa kazi hiyo, lakini hizi ofisi mpangilio wake ni kuwa wahadhiri wawili kukaa katika ofisi moja. Wahadhiri pia ni walezi wa wanachuo na hawa wanachuo ni watu wazima, wengine wametoka makazini, wameoa na wana familia. Kuna nyakati wanahitaji kuongea na wahadhiri kuhusu labda maendeleo yao ya kimasomo au mambo yao binafsi, wanahitaji faragha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ofisi ina wahadhiri wawili, mwanafunzi akifika akakuta wahadhiri wawili hawezi kuongea kwa sababu pengine hataki jambo lake likasikilizwa na mtu mwingine anataka amsikilize mmoja. Sasa anagonga ofisi, akigonga ofisi akiona watu wako wawili anarudi anasema samahani nimekosea kumbe hakukosea na Mhadhiri huwezi kutoka na mwanafunzi mkakaa canteen haiwezekani. Tuangalie hilo kuona kwamba ofisi za wahadhiri awe peke yake. Yeye mwenyewe apate faragha ya mambo yake, lakini vilevile na wanafunzi waweze kuwaona wale wanaoweza kuwapatia ushauri wa kimasomo, binafsi na mambo mengine ambayo ni mahitaji kwa wanafunzi wetu wa vyuo vikuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye sehemu ya malazi. Kuna uhaba mkubwa wa malazi, kwa mfano katika Chuo Kikuu cha MUHAS ni 30% ya wanafunzi ndiyo wana malazi wengine 60% wanajitafutia. Chuo Kikuu cha MUHAS kiko katikati ya jiji, wanafunzi wengi wanapata malazi sehemu mbali kwa sababu hawawezi kulipia yale majengo yanayozunguka na hali kadhalika na vyuo vikuu vingine. Tuangalie kuwapatia hawa wanafunzi malazi japokuwa juhudi ipo, lakini hiyo juhudi iende kwa kasi angalau kutoka kwenye 30% ipande juu ili wanafunzi wetu wapate muda mzuri wa kujisomea na nafasi nzuri ya kuishi badala ya kutumia muda mwingi barabarani na kero za mitaani itawafanya kutokuzingatia masomo yao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niende kwenye jambo moja ambalo limekuwa ni kero, hili ni suala la mafunzo kwa vitendo. Mashirika mengine siyo yote hawawakubali wanafunzi kwenda kufanya mafunzo katika taasisi zao. Kwa nini? Hawa wanafunzi wanasoma masomo Fulani, hawa wanachuo wanataka kwenda kufanya attachment, placement au kufanya mafunzo kwa vitendo katika taasisi fulani, taasisi ile inawakataa sababu gani kuwakataa hawa wanafunzi? Tunaposema tukitoka pale waive, yaani wawe wabobezi watakuwaje wabobezi kama hawafanyi kwa vitendo na hawajifunzi kwa vitendo? Ushirikiano na hizi taasisi ni muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri atoe tamko kwa taasisi angalau zote ziwakubali wanafunzi wa vyuo vikuu wanapotaka kwenda kufanya mafunzo kwa vitendo na kuwasaidia ili tuweze kupata product bora ya hawa wanafunzi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la TEHAMA kuna mabadiliko sasa ya teknolojia. Badala ya ile kukaa library muda wote kuna kutumia maendeleo ya teknolojia. Mheshimiwa Waziri hili suala liangaliwe katika maeneo kama madarasani kuwepo na mitandao. Wanafunzi watumie madarasa yao kujisomea, kutumia TEHAMA katika maeneo ya mabweni na mazingira wanayotumia kujisomea, hebu TEHAMA au internet na huduma hizo ziwe zinapatikana katika vyuo vyetu vikuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa niongelee suala la wanafunzi wenye mahitaji maalum. Hawa wanafunzi wapo, tunaomba wapewe vipaumbele na mahitaji maalum yako tofauti tofauti. Miundombinu kweli jitihada ni kubwa, lakini kuna mahitaji mengine ya binafsi ambayo huenda ni ya mtu mmoja mmoja hebu yaangaliwe. Haya yatakapogundulika, wakaletewa, yazingatiwe ili wanafunzi hawa nao waweze kupata elimu sawasawa na wengine ikiwemo mikopo 100% na kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono Wizara hii na kuipongeza sana. (Makofi)