Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa maelekezo yake kwenye Bunge hili ambayo yamepelekea mabadiliko makubwa kwenye sera, lakini na mfumo mzima wa elimu nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kusimamia zoezi hili kikamilifu. Kwa kweli naweza kusema sisi kama Wabunge tumeshiriki kwenye maeneo mbalimbali, alitupitisha pamoja na Kamati yake Maalum ambayo ilikuwa inashughulika na namna ya kuboresha mtaala. Tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake nzima bila kuwataja kwa sababu ya muda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumza kuhusu kuandaa mpango wa kuboresha shule za msingi. Katika nchi hii ukienda katika halmashauri zetu ukakuta namna ambavyo tumejenga shule za sekondari ukamtazama mwalimu wa sekondari, mwanafunzi wa sekondari, shule ilivyo nzuri na inavyopendeza, lakini ukatembea kilometa mbili ukaenda kwenye shule za msingi, ziko shule za msingi madarasa yako abandoned, ziko shule za msingi ofisi ya walimu ukiingia huwezi kutamani yule mwalimu akafanye kazi pale, imechakaa kiasi cha kutisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sasa nimefurahi kuona kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri wanakwenda kuandaa mpango. Nimwombe jambo hili, nadhani lipewe kipaumbele kikubwa, shule za msingi zimechakaa sana na shule nyingi ni za zamani sana. Huko ambako wanatoka watoto wa shule ya msingi wanaenda kusoma sekondari, shule zimechakaa sana. Unakuta kuna darasa moja jipya ambalo limejengwa pengine kwa fedha za Mheshimiwa Rais zilizokuja juzi au kwa P4R ndilo linagombaniwa na walimu kuwa ofisi au linagombaniwa kuwa shule za watoto wale wa awali. Madarasa mengine yote yamechakaa, hayana floor, hayana madirisha yamechakaa kiasi cha kutisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri jambo hili siyo tu litolewe mwongozo, nadhani kama Serikali tunahitaji kutafuta fedha hata nje ya bajeti hii kuhakikisha kwamba zoezi hili linafanyiwa kazi haraka na linakamilika. Nataka nitumie fursa hii pia kuzungumza kwenye eneo hili la utekelezaji wa mtaala mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri kama nilivyosema. Naungana na wanaosema tuanze pamoja na mapungufu yaliyopo, tuanze na kuanza kutatuambia wapi tuna mapungufu gani na tuyafanyie kazi gani. Lazima tukubali kwamba tunaanza tukiwa hatujajiandaa kiasi cha kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaanza tukiwa hatuna walimu wa kutosha na pengine tunaanza hata vyuo vyetu sasa hivi ambavyo bado vinazalisha walimu kwa mfumo wa zamani. Sasa lazima tukubaliane tuna transition hapa ambayo tunatakiwa kuifanyia kazi na tuwekeze kwa nguvu kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kutoa ushauri kwenye eneo hili. Jana kuna mzungumzaji mmoja alizungumza kidogo hapa kwamba shule nyingi Tanzania zina uhaba wa walimu. Shule nyingi za primary, za secondary sasa hivi tumejenga hazina walimu lakini tuna walimu wengi wanaomaliza vyuo vya kati na vyuo vikuu ambao wako mtaani, wako stranded na wamekuwa wakinyimwa au wakiomba na kukosa nafasi za kwenda kufanya mazoezi au kujitolea. Sasa nikafikiri kwamba huu ni muda muafaka kwanza tufanye maboresho haya tuliyoyaleta ya mtaala kwenye vyuo vyote. Hawa wanaomaliza sasa hivi wote wawe tayari wana hizo taaluma mpya ambazo tunataka ziende zikafundishwe huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, isitokee sasa hivi mwaka huu anamaliza mwanachuo ambaye atakwenda kuanza kusubiri ajira huko nje, halafu baadaye arudi tena kwenda kwenye short course kwenye semina kuja kufundishwa wakati bado yuko chuo. Kwa hiyo hawa walioko vyuoni wapate faida ya kukutwa na mtaala huu mpya, wafundishwe wakiwa vyuoni, waandaliwe tayari kwenda kusubiri soko linalokuja, lakini Mheshimiwa Waziri ajue hapa tumetengeneza tatizo lingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna maelfu ya walimu huko nje ambao wanasubiri ajira lakini wataachwa nje na mabadiliko ya sera na mabadiliko ya mtaala. Nadhani mwaka jana zilipotangazwa nafasi za kazi zilikuwa 7,000 au 8,000 na walioomba ni 120,000. Maana yake huko nje ya soko wapo wahitimu walimu 200,000 ambao hawana ujuzi na mtaala mpya unaofundishwa ambao wanasubiri kuajiriwa. Pia, tuna maelfu ya walimu ambao watamaliza mwaka huu na mwakani ambao watakutwa na mtaala mpya ambao watakuwa na sifa za kuajiriwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunafanya nini ili hawa walioko nje wanaodaiwa na Bodi, ambao watakuwa hawana sifa ya kuajiriwa, ambao wataingia kwenye soko wajikute hawawezi kuajiriwa kwa sababu, hata mwajiri binafsi hawezi kuajiri mtu ambaye tayari Serikali imebadilisha mtaala na huo mtaala yeye hana. Nafikiri hili tunahitaji kulifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kumaliza tatizo la sifa kwamba okay, ulikuwa unajitolea wapi? Tuweke utaratibu mahususi kwa mfano wapo watu wanatoka kwenye vijiji vyao na kwenye kata zao waende straight kwenye halmashauri zao wakajitolee kwenye hizi shule mwaka mmoja au miaka miwili baada ya hapo mfumo kama ajira zitawakuta wapate ajira kama hakuna watakuwa tayari na hiyo sifa ya kujitolea. Kwa hiyo, hatutahangaika tena kwenda kumtafuta mwalimu ili amwandikie mtu barua ili aweze kupata sifa ya kujitolea. Hili litolewe mwongozo kati ya Wizara hii na Wizara ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la tatu, nashukuru kwamba Chuo cha VETA cha Geita kimeanza kufanya kazi. Of course, kimejengwa kwa takribani miaka sita au saba; tunashukuru sana kimeanza kufanya kazi. Kimeanza kufanya kazi kwenye aina mbili za taaluma, electrical na plumbing.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mheshimiwa Waziri anakumbuka vizuri wananchi wa Geita wao wame-capitalise na shughuli za madini. Shughuli za madini ndiyo biashara kubwa lakini ndiyo ajira kubwa ya vijana wa Geita. Matarajio yangu ni kuona chuo kile kinaambatanishwa na tahasusi ambayo itakwenda kushughulika na taaluma ya madini tangu kwenye utafiti ngazi ya chini, uchimbaji, uchenjuaji na kwenye kuongeza thamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hatapata shida kule Geita kwa sababu tunao mgodi ambao Profesa Muhongo amesema hapa, kwamba watu wanaotaka kujifunza wanaweza kujifunza masaa yoyote kwa sababu ni mgodi mkubwa na umekuwa ukitoa ushirikiano huo wa kutoa taaluma kwa wachimbaji wadogo wadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe, hizi kozi ambazo zimeanza, tunamshukuru tumeanza, si haba, sasa atuletee walimu na vifaa, lakini pia tufanye maandalizi ya kufanya hicho ambacho wananchi wa Geita tulikuwa tunapigia kelele kama chuo cha mkoa. Vijana wengi katika eneo lile wangetamani kupata taaluma inayoambatana na kazi asili inayozunguka eneo lile. Sisi kule hakuna mtu utamlazimisha kufanya kazi, kila mtu anafanya kazi kwa sababu wanajua umuhimu wa kazi. Kinachotakiwa ni kuwaongezea taaluma. Tuwaongezee walimu na tuwekeze kwenye chuo kile. Kile ni chuo kikubwa sana lakini hakina fence; na Waziri anafahamu, chuo cha Serikali hakina fence, walinzi wawili. Nimwombe Mheshimiwa Waziri kama inawezekana tutenge bajeti ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la nne ni kwenye eneo la mikopo. Wazungumzaji waliotangulia wamezungumza vizuri sana. Napata tabu sana na hii means test. Miaka yote niliyokaa hapa Bungeni kila mwaka anayestahili ndiye anayekosa. Inawezekana siyo kosa la wale waliotengeneza huo mfumo, lakini nafikiri huu mfumo hauna sifa ya kumtambua mwenye shida. Nina mfano wa watoto watatu ambapo mmoja hata kwa kuambatisha vielelezo vya mzazi wake amekatwa miguu yote; huku mama yake akiwa ni mama wa ndani; ameweka vigezo vyote kwenye mfumo lakini mfumo unamtema; na yuko chuoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya vyuo vyetu vyote viwe vya Serikali au viwe vya binafsi ni kama vya wafanyabiashara. Anafahamu kabisa kwamba huyu mtoto, okay fine, ameomba dirisha la kwanza amekosa, la pili amekosa lakini bado wanamfukuza shuleni. Nimehangaika sana na Mkurugenzi wa Bodi aliyekuwepo na wa pili aliyefuata na huyo ni mtoto mmoja. Nadhani iko sababu ya kupendekeza jambo kama tumeongeza idadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja tu, nimalizie. Tumeongeza wanufaika, kwa maana ya diploma na hivyo tumeongeza mzigo kwa Serikali. Inawezekana Waziri hatapata fedha nyingi lakini wahitaji vyuoni ni wengi. Niombe, kama mwanafunzi amepata sifa ya kuwa enrolled kwenye chuo tutafute mfumo mwingine ambapo aliyeomba awe na haki ya kupata flat rate kwanza, angalau minimal amount, flat rate kwa watu wote kwa kuanzia, ili nyingine mzazi wake aweze kupambana kuliko unaweka vigezo ambavyo mfumo hauwezi kuwatambua wanaohitaji
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.