Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza kabisa, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia Wizara ya Elimu. Napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Profesa Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Kipanga, Katibu Mkuu Profesa Carolyne Nombo pamoja na wafanyakazi na watendaji wote wa Wizara ya Elimu kwa kazi nzuri wanayoifanya. Kwa kweli wanaitendea haki Wizara ya Elimu. Wameleta mabadiliko makubwa, tunawashukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa bajeti kubwa ya elimu aliyoitoia ambayo ni shilingi trilioni 1.96; kwa hiyo tunampa pongezi. Natoa ushauri kuwa, ingawaje bajeti ni kubwa, naomba iendelee kuongezeka mwaka hadi mwaka kwa sababu bado haitoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo ada, naomba niongelee kuhusu mikopo ya wanufaika wa vyuo vikuu, elimu ya juu. Bajeti imekuwa ikipanda mwaka hadi mwaka. Nawapongeza Mheshimiwa Rais pamoja na Waziri kwa kazi nzuri wanayoifanya. Hata hivyo bado wanufaika ni wengi kufuatana na vigezo na nashukuru wamepandisha, kweli wengi wamepata lakini bado wanaopaswa kupata ni wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri na naomba hiyo bajeti, kama swali nililouliza hivi majuzi kuhusu mikopo ya vyuo vikuu; naomba iwaangalie vizuri kusudi na ambao wanastahili kupata waweze kuendelea kupata. Chukulia mtoto amesomeshwa na mama yake ambaye ni mama ntilie (Mama Lishe); ni mama anayeuza chapati au mbogamboga na ameweza kumsomesha mtoto wake kwenye secondary schools za private lakini bahati mbaya amekosa vigezo vya kupata mikopo. Naomba utafutwe mfumo ambao unaweza kuwasaidia watoto wengi ambao wanaomba mikopo ili waweze kupata mikopo na kuendelea na kutimiza ndoto zao. Maana wanapokosa mikopo wanarudi nyumbani kwao. Wengine wanakuwa tayari wamekwishakwenda vyuoni; lakini kwa sababu ameshindwa kulipia, amekosa mkopo anarudishwa nyumbani. Hivyo ndoto yake inakuwa imeishia hapo hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba itafutwe jinsi ya kuangalia hawa wanafunzi ambao wana ndoto ya kuwa marubani, ma-engineer, maprofesa na wahadhiri ili nao waweze kuendelea kupata mikopo. Naamini Mheshimiwa Waziri amenisikia na naamini alinijibu. Hata hivyo, bado naendelea kukazia hapo hapo kuwa mfumo wa jinsi ya kuwapatia mikopo hawa wanafunzi ambao ni wahitaji uangaliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kwenye vyuo vikuu. Napongeza, ni kweli campus nyingi za vyuo vikuu zinafunguliwa lakini ziangaliwe. Kwanza, tuboreshe vyuo vikuu vilivyopo ambavyo ni vyuo vikuu mama, kikiwemo Chuo Kikuu cha SUA, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha UDOM na vingine ambavyo ni vyuo mama. Tusizalishe sana campus nyingi, si lazima kila mkoa uwe na campus za vyuo vikuu, badala yake tunaweza tukaboresha hivi vyuo vikuu vilivyopo vikaweza kuwa na mikondo mbalimbali na degree mbalimbali ambazo zinaweza zika-cover wale wengine kwenye vyuo vikuu hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na napongeza ukarabati unaoendelea. Kwa mfano Chuo Kikuu cha Sokoine. Naipongeza Serikali kwa sababu imeweza kujenga maabara nzuri sana ya Kimataifa ambayo ipo hapo. Kwa hiyo, naamini kuwa hata vyuo vikuu vingine ukarabati na ujenzi unaendelea, lakini kama wenzangu walivyosema, kwamba hostel (mabweni) bado ni tatizo. Kwa hiyo hawa watoto waangaliwe. Wengine ni watoto wadogo, wametoka nyumbani kwao hawajazoea kukaa nje nje. Kwa hiyo wakijengewa mabweni itakuwa ni nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu tafiti, naomba tafiti za vyuo vikuu nazo ziangaliwe. Wahadhiri ambao wanafanya utafiti waweze kupewa fedha za kutosha kwa sababu kwenye sayansi na teknolojia lazima uweze kufanya utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa mafunzo kwa vitendo, nashukuru kwamba kuna vyuo vingine ambavyo vinafanya mafunzo kwa vitendo hapo hapo kwenye kampasi zao; kwa mfano pale SUA. Namshukuru Mkuu wa Chuo cha SUA ameweza kuwawezesha wanafunzi wanafanya vitendo pale pale, wanalima pale pale na watoto wengine wanakuja chuoni hata jembe hawalijui; lakini angalau sasa hivi wanaweza wakafanya. Kwa hiyo mafunzo kwa vitendo (field practicals) yaweze kuongezewa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na ajira; vyuo vikuu vina maprofesa, madokta na wahadhiri. Wahadhiri wana-retire (wanastaafu) maprofesa wengi wamestaafu. Kwa mfano Chuo Kikuu cha SUA wastaafu wengi ni maprofesa. Kwa hiyo ionekane jinsi ya kuajiri wahadhiri wapya ambao wataweza kuchukua nafasi ya hawa wanaostaafu, kwa sababu wakistaafu hakuna mwingine ambaye anaweza akafundisha hayo mambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja upande wa stahiki za wahadhiri na hasa maprofesa; kama alivyosema Mheshimiwa Shally, kwamba kuna maprofesa wengi wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) wanadai stahiki zao baada ya kustaafu. List ni kubwa sana. Wameshaleta maombi yao mpaka utumishi. Naomba sana waweze kuangaliwa kwa sababu wanadai. Ni kweli kwamba mtu ukidai stahiki yako ni vizuri ukalipwa na si kudai mara kwa mara. Kwa hiyo, naomba hiyo ya kuhusu vyuo vikuu iweze kuangaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ubora wa elimu ni miundombinu pamoja na walimu. Ukweli ni kwamba kuna upungufu wa walimu, hasa walimu wa sekondari. Sekondari nyingi hasa za pembezoni utakuta kuna walimu wawili na wana wanafunzi kuanzia darasa la kwanza mpaka la saba. Hebu fikiria kwamba sasa la saba huendelea mpaka form four lakini unadhani kuwa ni nani atawafanya wafaulu vizuri? Ni vyema wapate walimu wa kutosha hasa walimu wa sayansi, Wizara itafute mfumo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu wako wengi ambao nawajua, ambao Waheshimiwa Wabunge wanawajua, ni wengi. Wamechukua mafunzo ya sayansi na wako mitaani hawajapata ajira. Wanaomba mara kwa mara, vigezo wanavyo lakini bado hawajaajiriwa ilhali shule zetu hazina walimu wa kutosha. Muda bado, hivyo, naomba niendelee kidogo. Kwa hiyo naomba Wizara wawaajiri hao walimu ili waweze kufundisha watoto wetu; kwa kweli walimu wa sayansi wanahitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na mafunzo ya amali, nimalizie hapo hapo. Naunga mkono kuhusu mafunzo ya amali na mtaala mpya; hasa mafunzo ya amali. Wakipata vitendea kazi na ujuzi ambao zamani ulikuwepo; kulikuwa na needle work, yalikuwepo mambo ya domestic science; hayo mafunzo ya amali yatawafanya wanafunzi hawa waweze kujiajiri wenyewe na hivyo kupunguza matatizo ya ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa hayo machache niliyochangia na Mwenyezi Mungu akubariki na aibariki Wizara ya Elimu, fedha ziongezeke na bajeti iweze kuongezeka na waweze kuwapatia walimu, wahadhiri waweze kupata stahiki zao na madai yao kwa sababu wamedai kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)