Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii ya Wizara ya Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake na kwa kuielekeza Wizara ya Elimu ili iweze kurejea na kuweza kuleta mfumo mzuri wa mitaala ambayo itakuja kuwasaidia vijana wa Tanzania kuweza kujikwamua kimaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto kubwa sana kwa vijana. Wanashindwa kwenda kuyakabili maisha kwa sababu ya kukosa ujuzi, maarifa na elimu. Ukianglia kwanza demografia ya Tanzania ya idadi ya watu utaona kwamba imekaa kama pyramid. Kwa maana hiyo vijana wengi wa Tanzania au idadi kubwa ya Watanzania ni tegemezi. Kwa nini tegemezi? Nguvu kazi ya vijana wa Tanzania miaka 15 mpaka 40 zaidi ya 50% ni wategemezi kwa sababu hawajaandaliwa kwenda kujiajiri wenyewe kwa sababu ya kukosa ujuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana kuna wimbi kubwa sana sasa hivi la Watanzania wenzangu kwenda kuwapeleka pengine watoto shule hizi za english medium na international schools ambapo ukiangalia vijana hao wanaandaliwa kwenda kuwa watawala lakini pengine kwenye white colour jobs ambazo kiukweli hazipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona kwamba kwa Tanzania karibu kila mwaka kuna watu takriban 800,000 hivi ambao wameshahitimu na wanatakiwa waingie kwenye ajira. Kwa hiyo kwa hili nampongeza Mama Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na namshukuru sana kwa kuja na wazo hili, kwamba sasa tuweke mtaala mzuri. Kwa upande wa amali tuna hakika kabisa kwamba wanafunzi wakifikia sehemu fulani wanaweza kujiajiri wenyewe, watakuwa na ujuzi wa kutosha na wanaweza kujikimu kimaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiukweli tumeona jitihada nyingi sana za Wizara na mwelekeo ni mzuri kwenye jitihada hizo, kwamba tunaweza kwenda na mifumo hiyo ya mkondo wa amali, lakini bado tutaendelea na mkondo mwingine wa taaluma; na jitihada zao wamezieleza kwenye bajeti. Wana mpango wa kujenga miundombinu kwenye shule 100 za sekondari kuanzia mwakani na 26 zitaanza kudahili. Kuna vyuo 65 vinakwenda kuanzishwa. Kuna wanaoendelea kusajili hizi vocational training schools; wanaendelea kusajili technical schools hizi ili kwamba angalau mwakani basi wachukue idadi kubwa ya wanafunzi wajaribu kwenda na hiyo mikondo miwili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tuna nia thabiti kweli kwamba hizi sasa ndizo solution kwa ajili ya Taifa letu na vijana wetu, hatuna budi kukubaliana kwamba Wizara hii ipewe fedha nyingi za kwenda kuwekeza huko. Tumeona kweli, hata mwaka jana nilisema, kwamba bajeti kubwa ya development ya Wizara ya Elimu kila mtu amesema 60.3% inakwenda kwenye mikopo. Ni jambo jema, lakini nashauri tu kabisa, kwamba huko kwenye mikopo sijui kwa nini inaitwa development; kwa sababu tunaweza tukafikiria Wizara ina fedha nyingi. Tumeona bajeti yao ya 1.9 trillion shillings tukafikiri zote ndiyo zinakwenda sasa kwenye miamala na kwenda kuboresha elimu; kumbe nyingi zinakwenda huko kwenye mikopo ambayo kwa vyovyote vile ingekuwa ni revolving fund; kwa sababu inakopwa na kurejeshwa, au ingekuwa kwenye capacity building kiasi kwamba kama haitarudi kwenye marejesho, basi iwasaidie Watanzania kwenye capacity building.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo tunaona kwamba fedha zinazokwenda sasa kwenye kuboresha elimu na miundombinu ya kwenda kupambana kuwezesha hii mikondo ya amali itakuwa ni kidogo. Kwa sababu hiyo sasa, hofu yangu ni kwamba kwa huu utaratibu coverage itachukua hata zaidi ya miaka 10 ili kuona kwamba sasa Tanzania nzima tume-stable kwenye mikondo miwili kwa sababu sasa tunakwenda taratibu kutokana na bajeti. Hili lazima kama Taifa tulione.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwijage mwaka jana alisema kwamba tunawafanyia majaribio watoto wa Tanzania. Mimi pia nasema, kweli kwenye hili tuwe makini; kwa sababu naona tu kwamba, tunawaweka wanafunzi waingie mikataba ya maisha na hii mikondo. Hivi ukimchukua mtoto wa miaka sita ukamweka kwenye mkondo wa amali ambao atakwenda nao na elimu ya lazima ni mpaka form four. Miaka kumi amesoma amali akitoka hapo kwenda chuo au kwenda form five bado anaendelea na mkondo wa amali mpaka chuo kikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kwa mfano hapa katikati pengine hatukumjengea mazingira mazuri, amesoma kwenye sehemu ambayo hapakuwa na karakana nzuri ya kumfundisha na hapakuwa na walimu wazuri; hivi kum-correct huyu mtoto unafanyaje? Anakwenda kuanza darasa la kwanza au anakwenda kuanza form one? Kwamba sasa pengine upande huu amefeli, hakufanya vizuri sasa aanze kusoma upande wa taaluma. Hiki kitu lazima tuwe makini sana, vinginevyo wazazi na walimu waelimishwe kuhusu namna ya kuwachagua hawa Watoto, kwamba ni nani anatakiwa kwenda upande wa amali na nani anatakiwa kwenda upande wa taaluma; vinginevyo commitment ya Serikali iwe kubwa sana, ama sivyo tunakwenda kuzima ndoto za hawa watoto. Watafika mahali watakuwa useless mitaani. Kwa hiyo hili lazima tuliangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri, kwa sababu hiyo basi maandalizi ya walimu na karakana ni muhimu sana. Mtoto asije akaenda tu kufundishwa habari ya automobile engineering akaenda labda kwenye mambo ya carpentry au usanii na hana namna ya kujifunza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mwanzo ni mgumu, kuna karakana za mitaani zina mafundi, local artisans, mafundi uashi wazuri sana. Serikali labda ingeanza basi kwenye karakana zetu na iwaajiri wale wa mitaani wanao-perform vizuri. Kuna fundi wa mtaani akikufungia injini ya gari wala huwezi kuona shida na hajasoma hata kidogo. Tena wako vizuri kuliko hawa wakwetu wanaosoma vocational training na wengine. Kwa hiyo basi, Serikali ianze nao wale waliobobea. Kuna mafundi cherehani wa mitaani wanaoweza ku-design vizuri, wachukuliwe na kama tayari tutakuwa tumeshajenga karakana na miundombinu ya kutosha, waanze kuwafundisha vijana wetu. Kwa hiyo, kwenye hilo la amali naliunga mkono, naona linaweza kuwa ni muarobaini kwa watoto wetu, wakimaliza kusoma wajue tu kwamba kuna kujiajiri. Kwa sababu hiyo, Serikali iangalie na iwezekeze fedha za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine unaenda kwa walimu, kuna changamoto za aina mbili kwa walimu; kwanza, kuna upungufu mkubwa wa walimu, lakini kuna ubora, umahiri na ubobezi kwa walimu. Indicator ya kuona kwamba tunafanyaje ni performance ya wanafunzi, jana ameeleza Mheshimiwa Getere hapo, alikuwa anaangalia skillness ya wanafunzi wanaoishia pengine Division Four na Division Zero, ile ni image na indicator ya walimu wanaowafundisha wanafunzi. Kama walimu hawata-perform vizuri tusitegemee kwamba wanafunzi wetu watafanya vizuri na wataenda ku-compete kwenye soko la dunia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana wanafunzi wengi wanaofeli ni wanaochukua masomo ya sayansi na ndiyo maana wanakwepa. Yaani, mwanafunzi anaona kuliko umpeleke darasa la Physics, Chemistry, Hesabu akaenda kupata sifuri ni afadhali aende kwenye upande wa arts pengine Historia na Jiografia ambayo anaweza akajisomea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kwenye dunia inayoenda kwenye sayansi na teknolojia, lazima tuwe na walimu wa sayansi, kwa sababu kuna gap kubwa ya walimu wa sayansi, tuwekeze kwenye ualimu, tuajiri walimu wa kutosha kwenye sayansi. Kwa sababu sasa tumeenda kwenye mtaala mpya, tuhakikishe kwamba tuna walimu wa kutosha wanaoenda huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna kusajili walimu kwenye bodi ya taaluma ya ualimu, hili jambo ni jema sana, walimu watambuliwe na waone training needs, waone gap za walimu ziko wapi…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. YUSTINA A. RAHHI:…ili siku hizi TRC ambazo tumezijenga walimu wafundishwe mara kwa mara, training na nini, kuwakumbushia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile udhibiti na ubora wa elimu…
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Yustina Rahhi, naona huweki full stop, ahsante sana. (Makofi, Kicheko)