Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango wangu katika elimu ambayo ndiyo msingi wa ukuaji wa uchumi katika Taifa letu la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu, Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amefanya kazi kubwa katika Jimbo letu la Tarime Mjini na ametuwezesha kupata zaidi ya shule nne katika Jimbo letu la Tarime Mjini ambazo ni; Shule ya Sekondari Nyakisese, iliyoko Nyandoto; Ikohi sekondari iliyoko Turwa; Regicheri iliyoko Nkende. Ameboresha sana Shule ya Sekondari ya Tarime. Naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Wanatarime naomba nichukue nafasi hii kuelezea umuhimu wa elimu katika Taifa letu la Tanzania. Elimu ni zaidi ya kusoma, kuandika na kuhesabu, elimu ni muhimu katika nyanja zote katika maisha ya binadamu, elimu ni mojawapo ya uwekezaji mkubwa ambao Serikali inaweza kuwekeza kuhakikisha kwamba uchumi wa nchi unakua, elimu husaidia watu kufanya kazi vizuri na unaweza kuunda fursa za ukuaji endelevu wa uchumi wao wenyewe pamoja na watoto wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, elimu imeonekana kuwapa watu ujuzi muhimu na zana za kuwasaidia kujikimu wao wenyewe katika maisha yao. Utafiti uliofanyika umeonyesha kwamba nchi za Australia, Marekani na Japan ni mojawapo ya nchi ambazo zina elimu nzuri sana na watu walioelimika. Watu binafsi, mtu mmoja mmoja, katika nchi hizo wanaishi juu ya mstari wa umaskini. Kwa takwimu hizo tunaweza kujifunza kwamba elimu ni sehemu ya ukuaji au ustawi wa uchumi katika nchi yoyote ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ikoje katika nchi yetu ya Tanzania? Yametokea mabadiliko ya mitaala ya mara kwa mara ambayo yamesababisha ukosefu wa utulivu wa mitaala katika Taifa letu la Tanzania na hivyo kusababisha elimu inayotolewa katika nchi yetu isikidhi mahitaji yanayohitajika katika kukuza uchumi wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano katika miaka ya 90, mtaala ulibadilika ambapo toka wakati huo elimu yetu imekuwa siyo nzuri sana. Haiwajengi wahitimu kujiajiri wenyewe au kujisimamia wenyewe, wamekuwa ni watu wa kutegemea kuajiriwa peke yake. Mwaka 2004 yalifanyika mabadiliko ya mtaala, miaka ya 2010 pia yalifanyika mabadiliko ya mitaala, tena mwaka huu 2024 yamefanyika mabadiliko ya mitaala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa niseme, tayari mtaala mpya umeanza kufanya kazi na umeanza kazi Januari, lakini hakuna maandalizi yanayowezesha walimu kufundisha mtaala mpya. Wadhibiti ubora wanapita mashuleni kuhimiza walimu wafundishe mitaala mipya lakini hakuna maandalizi ya kutosha. Walimu hawa hawaujui huu mtaala mpya ni nini, hawaelewi mtaala mpya unafanyaje kazi kwa sababu waliopewa semina ni wachache kulingana na idadi ya walimu waliopo katika shule zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, isitoshe, mwanafunzi ambaye anafundishwa na mwalimu ambaye hajui kile anachokifundisha, tunatengeneza watoto wetu wawe wa aina gani? Hivi nikienda kufundisha mtu arushe ndege na mimi sijui kurusha ndege si unategemea ajali? Kwa hivyo, hii tunatengeneza ajali ya kielimu katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha ajabu zaidi vitabu ambavyo walimu wanategemea kufundishia havipo katika shule zetu, maana yake nini? Mwalimu atoe vitu kichwani afundishe huu mtaala mpya ambayo ni hatari sana katika kuelimisha watoto wetu ambao wanasoma katika shule zetu. Sisi wote hapa watoto wetu wanasoma katika shule zetu hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi wanategemea kwamba mtoto anapokwenda shuleni aweze kuwa mtu ambaye amepata ujuzi wa kujiendesha baadaye akiwa mtu mzima. Kwa miezi sita sasa toke Januari, mpaka leo mtaala mpya unafundishwa. Jana, katika jimbo langu ndiyo nilisikia walimu wakuu wanaenda kufundishwa juu ya mtaala mpya. Walimu wakuu hawa ndiyo wasimamizi wa mtaala mpya, sasa walikuwa wanasimamia nini katika shule zao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona hapa kuna mchezo ambao siyo mzuri, kulikuwa na dharura gani na haraka gani ya kupeleka mtaala huu uanze kabla ya maandalizi ya kutosha katika shule zetu ili watoto wetu wanapofundishwa waelewe kile wanachofundishwa. Mchezo huo ambao ulifanyika miaka ya 90 ndiyo unafanyika tena mwaka 2024, kweli? Haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge tuliangalie hili na watoto wetu wanafundishwa huko huko, wanafundishwa kitu gani kwa miezi hii sita ambayo wamefundishwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, vitabu vya mtaala mpya viko kwenye softcopy, hivi mshahara wa mwalimu ambao analipwa shilingi laki tatu, laki nne pamoja na mikopo hii ambayo tunasema hapa ya kichefuchefu, mwalimu atatoa wapi hela aweke kifurushi aweze ku-download kitabu aweze kufundisha? Mheshimiwa Waziri hii si sawa na hii ni kurudisha nyuma elimu yetu, haikubaliki kabisa kwamba mwalimu atumie fedha yake ku-download kitabu na siyo kwamba hawezi kuki-print kile kitabu, unasomea pale pale. Hii kwa kweli naona kwamba udharura huu uliofanyika haukuzingatia hali halisi ya nchi yetu na namna tunavyohitaji elimu iwe katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kuhusu upatikanaji wa vitabu katika Taifa letu, ukienda katika bookshops unatafuta kitabu kwa kweli vitabu havipatikani. Siyo sasa hivi, hata wakati uliopita bado vitabu havitoshelezi kwenye bookshops, pia, hata mchanganyiko uliopo unachanganya, Serikali inahimiza tutumie vitabu vya TIE na TIE ukiangalia vitabu vyao viko very shallow, haviendi deep sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Kiti chako kitoe maelekezo kwa Wizara iruhusu sasa vitabu…
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Michael Kembaki kuna taarifa, taarifa inatokea wapi?
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Hapa.
MWENYEKITI: Okay, Mheshimiwa Dkt. Thea.
TAARIFA
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika, napenda kumpa taarifa msemaji, vitabu vinavyotungwa, vinavyotengenezwa pale TIE vinatengenezwa na wataalam, wasomi wa kila somo. Kwa hiyo, vile vitabu haviko shallow kabisa, vitabu vinatengenezwa au vinaandikwa na walimu ambao ni wabobezi. Wataalam wote wanavipitia, kwa hiyo, vitabu vyetu vya TIE haviko shallow kama anavyosema msemaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Kembaki unaipokea hiyo taarifa?
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sipokei taarifa kwa sababu mlaji ndiyo anajua kama chakula ni kitamu au siyo kitamu. Kwa hivyo, kama yeye ni sehemu naomba niseme sijapokea taarifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhumuni langu ni hili, kwamba nchi yetu iruhusu wazalishaji wengine wa vitabu waweze kuingia sokoni washindane kwa ubora. Kusiwe na limitation ya kitabu, kama kitumike kitabu kimoja, hapana, kuwepo na uhuru kama zilivyo sekta nyingine ili vitabu vipatikane kwa wingi, walimu waweze kuwa na machaguo kadha wa kadha kwa ajili ya kuongeza uelewa wa ufundishaji. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)