Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Jumanne Kibera Kishimba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kahama Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naungana na Wabunge wenzangu, kuipongeza Wizara hii ya elimu ya juu. Pia, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa suala zima la maboresho ya elimu pamoja na Mheshimiwa Waziri na timu yake nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wabunge kazi yetu ni kuangalia maeneo ambayo bado yana matatizo mengi sana. Suala hili la elimu naona kila anayeamka anaendelea kulizunguka sana. Naweza kuungana na mchangiaji aliyemaliza, Mbunge wa Tarime, hapa tunayemkwepa ni mtu wa muhimu sana, huyu anayetutayarishia kitabu watoto wetu wakasome huwa anapatikanaje na ni nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiondoa suala kwamba amesoma, ana kitu gani kingine cha umaarufu alichonacho ili tumpe huyu akatuzalishie kitabu watoto wetu wajifunze? Kwa nini nasema hivyo? Nimepitia vitabu viwili vitatu vya shule za msingi, kipengele kimoja tu ambacho kimeniuma sana, lakini ukikiangalia kipengele hicho ndicho hata Wizara inachofanya. Mwalimu kwenye maelezo yake anaeleza kwamba mwanafunzi ukiwa unasoma, ameandika vizuri sana, ukimaliza shule acha kujenga nyumba yako hii ya wazazi wako ya tope na nyasi, utajenga nyumba ya bati nzuri ya block, siyo vizuri kuwa na ng’ombe uza ng’ombe jenga nyumba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, huyu mtoto mimi nakaa naye, tunakaa nyumba ya nyasi, nyumba ya tope, tumejenga na tunao hao ng’ombe, wewe unaanza mwanzoni kumfundisha mwanangu kwamba hii nyumba yangu siyo sahihi na ni vizuri tuuze mifugo ili tujenge nyumba, automatically, mgogoro unaanzia hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tupo makabila 125, hatuwezi kuishi haya maisha wanayoyasema humu ndani ya Ulaya, nani ataweza kwenda kuishi maisha ya kizungu? Haiwezekani! Mwanafunzi aelezwe maisha ya wazazi wake, kwamba hii nyumba ya nyasi na tope na ng’ombe mlizonazo nyumbani ni mali halali; ni sahihi; ni nyumba sawasawa kabisa na nyumba nyingine, kwa sababu hata kama tutabisha, nyumba za nyasi au nyumba za tope tukasema hazifai, hizo nyumba za watalii kule National Park si za nyasi? Si wanalipa shilingi milioni moja kwa siku? Unamwambiaje mtoto wangu kwamba ni haramu hizo nyumba na unataka sisi tuuze ng’ombe tukajenge nyumba, inawezekana kweli? Mimi niuze ng’ombe nikajenge nyumba, usingizi unaletwa na nyumba? Inawezekana kweli? Mimi usingizi wangu na maisha yangu yanapatikana kwa ajili ya ng’ombe siyo kwa ajili ya nyumba. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najaribu tu kulipima na kuliona kwamba, inawezekana tunazunguka kote, tatizo kubwa liko hapa. Huyu anayeandika vitabu lazima awe mtu ambaye anayajua maisha ya Watanzania ili mimi mtu wa Kahama ninaposoma kile kitabu nikiwa mdogo niyaheshimu maisha ya nyumbani; kwamba haya maisha hata nikishindwa kumbe naweza kuishi, kuliko sasa hivi inavyoonyesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekwenda kwenye maonyesho ya Mheshimiwa Waziri ya watoto wenye vipaji. Kilichonishangaza, Mheshimiwa Waziri bahati nzuri alikuwepo, kila unapokwenda lile banda la watoto wenye vipaji, unakuta ametengeneza redio hajakamilisha, katengeneza mita ya maji anahitaji msaada, haijafanya kazi. Sasa Mheshimiwa Waziri ina maana kipaji cha binadamu, kwa nini kusiwe na kipaji cha kulima? Kipaji cha kukamua maziwa, wenyewe hawaruhusiwi? Kipaji cha kuchunga hakiruhusiwi? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Waziri kwenye kipaji cha kulima kama mtu ana kipaji cha kulima akalima heka moja kwa siku moja si ni shilingi laki moja? Siyo kipaji? Shilingi laki moja maana yake kwa mwezi si shilingi milioni tatu? Je, ni sahihi kuwafundisha judo, sarakasi, mabaunsa, mwisho wa yote watakuwa nani sasa? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake tunaongea hapa kwamba je, tunatarajia kuwa wazungu? Yaani inawezekana Tanzania nzima watu milioni 70 tutakuja kuwa wazungu na tuishi kabisa kweli yaani tuondokane kabisa iwezekane? Ingawa pamoja na yote nimefuatana na Waheshimiwa maprofesa kwenye michango lakini sioni kwa nini hatutaki kabisa yale maisha original? Hatuwezi kuwa na elimu ya Kiafrika na yenyewe ikafundishwa darasani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna somo la kutafuta pesa na kutunza pesa, kwa nini kwenye mitaala ya elimu halimo? Mheshimiwa Waziri wote hapa wanaeleza kwamba nataka mwanangu asome akawe daktari, akawe nani ili afanye nini? Si apokee mshahara? Sasa kwa nini tunakataa somo la kutafuta pesa? Lifundishwe kutoka darasa la kwanza. Mheshimiwa Waziri litakuwa kosa gani na madhara yake yatakuwa nini? Yaani kutafuta pesa na kutunza pesa madhara yake yatakuwa nini? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana wenzetu wa mitaala lazima wakubaliane kwamba suala la pesa liongelewe wazi kwa sababu ndiyo suala la mwisho. Kote huko kusoma, kufanya nini, mwisho wa yote tunaenda kuangukia kwenye fedha, sasa kama hatutaki hela tufanyeje? Profesa Muhongo ameongea vizuri sana, lakini je, tutafanya nini bila hela? Huyu mtu ana ng’ombe kumi anaweza akasoma mpaka Ujerumani, anafanyaje sasa hebu watuambie. Je, wote wataondoka kweli Watanzania wote wataondoka huko vijijini? Haiwezekani! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, najaribu tu kumweleza Mheshimiwa Waziri afikirie kwa mapana sana. Leo hapa biashara inayoongoza na bahati nzuri yeye ni mwenyeji wa Moshi, biashara inayoongoza Tanzania nzima ya kwanza ni ya maduka. Je, tunao mtaala wa maduka kwenye vyuo vyetu na kwenye VETA? Mnataka tuwe na mabilionea, haya, bilionea anatokea wapi? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya maduka yote yaliyopo hapa Dodoma waliyolipia ni hawa wafanyakazi wa Serikali. Wamelipia kodi shilingi milioni moja, si wameyaweka nguo hapo, wamelipa shilingi milioni moja, wanataka nini? Si biashara ya maduka? Sasa biashara ya maduka wanakaataje isiende kwenye mitaala ya shule? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu watu wote huanzia kwenye magenge wakaenda kwenye maduka, kwenye maduka ndiyo wakaenda kwenye viwanda. Akishakuwa anakiuza kitu ndiyo anajua kumbe hiki ninachokiuza naweza kukitengeneza, kinatengenezwaje? Ndiyo anaanza kufikiria. Sasa huku kwingine tunazungukaje kwenye sehemu ambazo ni za msingi. Nataka tu nilieleze ili kusudi kulitolea mwanga zaidi maana yake naona bado linaendelea kutusumbua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeongea hapa suala la matatizo ya sekondari na university, mimi sina tatizo, lakini labda nimuulize Mheshimiwa Waziri, mimi mtoto wangu anatakiwa kupata degree kwa miaka minne, ameishia miaka miwili, mimi nimekosa hela ameshindwa amerudi, huyu tunamwitaje? Kwa nini asipewe nusu degree, wamwandikie nusu degree kwa sababu anayeamua degree siyo Waziri, anayeamua degree ni mwajiri. (Makofi/Kicheko)

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Engineer Mwanaisha.




TAARIFA

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa Taarifa Mheshimiwa Kishimba kwamba, katika Competence Based Education Type, mwanafunzi anaposoma akishindwa kufika mwisho, pale katikati anapewa ile NTA Level 7. Inakuwa siyo degree kamili, bali hapa nyuma kuna cheti ambacho anapewa kabla hajakamilisha ile degree yake. Hiyo iko hapahapa Tanzania, ukienda DIT wanatoa competence based, unasoma unapewa kitu kinaitwa Higher National Diploma ambayo una…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Engineer, natamani Mheshimiwa Kishimba akuelewe unachokisema. Mheshimiwa Kishimba unaipokea hiyo Taarifa?

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei kwa sababu, huyu mwajiri siyo Mheshimiwa Eng. Ulenge, ni mtu wa Kariakoo. Unamwambia mimi nilikuwa nasoma miaka minne, nikakosa hela nikaishia miwili, anakuulizaje? Hayo maneno ya competence hayajui, anakwambia unayo nusu degree, si ndiyo? Wewe niandikie mimi hayo maneno yote yalete, hapa chini andika nusu degree, ili tajiri ndiyo atoe maamuzi. Maana haya mengine yote mnayoongea ni utapeli, eleza kabisa kwamba, mimi nina nusu degree. Najaribu kueleza kitu ambacho kiko kwenye field ya maisha kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja tu nimalizie. Mheshimiwa Waziri, kulikuwa na suala hili zuri sana la watoto kula shuleni. Sasa hivi limetuletea mgogoro sana kati ya sisi na walimu, linatuchonganisha. Tunaomba Wizara itoe tamko kwamba, kiwango cha chakula ambacho wazazi wanatakiwa kuchangia pale shuleni kiwe ni chakula gani na kwa kiasi gani? Kwa sababu, sasa hivi unaambiwa mtu alete kilo nne za mchele kwa mwezi na kilo tatu za maharage, lakini ni shule gani inayokataa mchicha? Hawataki mchicha wala matembele, itawezekana namna gani? Si ndiyo? Sasa maharage ni shilingi 4,000 si ndiyo? Shilingi 12,000, wewe una watoto sita, utaweza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuandikieni hapahapa, Serikali itoe waraka kwamba, chakula kinachotakiwa ni hiki. Kama tajiri ana hela zaidi, yeye hahusiani na tatizo hata nyama atatoa ili hawa maskini tuwatendee haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huo, nakushukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)