Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Jambo la kwanza, natumia nafasi hii kuipongeza sana Serikali pamoja na Wizara kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya. Pia, natumia nafasi hii kuzipongeza taasisi na vyuo vilivyo chini ya Wizara kwa kazi nzuri ambazo vinafanya, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo Wizara imekuja nalo, la mabadiliko ya mitaala, ni katika kutekeleza Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu, suala la elimu ni suala la Kikatiba. Ukichukua Ibara ya 11(1) inazungumza kwamba, kila Mtanzania, kila mtu ana haki ya kufanya kazi na kila mtu ana haki ya kujipatia elimu. Ibara Ndogo ya (2) inasema, “Kila mtu anayo haki ya kujielimisha na kila raia atakuwa huru kutafuta elimu katika fani anayopenda hadi kufikia upeo wowote kulingana na stahili na uwezo wake”. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, elimu ni suala la Kikatiba ndiyo maana hata tulipotayarisha Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2000 – 2025, katika malengo matano tuliyoyaweka, mojawapo ya lengo ilikuwa ni kuwepo kwa jamii iliyoelimika vyema na inayoendelea kujifunza. Ipo kwenye Dira ya Nchi yetu, lakini kama hiyo haitoshi, mwaka 1961 wakati tulipopata uhuru, Baba wa Taifa alitambua na alitangaza kwamba, wapo maadui watatu wa nchi yetu, maadui hao ni ujinga, umaskini na maradhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo yote tangu tumetoka huko mpaka leo na hawa maadui watatu bado wanaendelea kutusumbua katika Taifa letu. Ndiyo maana hata viongozi mbalimbali, wadau wa elimu na wadau wa Maendeleo wa Afrika walipokutana Kampala, Uganda mwaka 1991, walikuja na kitu kinaitwa “The Kampala Document” ambayo walikubaliana maazimio kadhaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya mambo waliyokubaliana ni umuhimu wa elimu kwa Vijana wa Afrika. Wakasema, Vijana wa Kiafrika wafundishwe juu ya elimu, juu ya Maadili ya Kiafrika, juu ya Utamaduni wa Kiafrika na wajifunze teknolojia itakayolisaidia Bara la Afrika katika kuleta maendeleo. Kwa hiyo, utaona haya yote ni masuala ambayo tumeanzia kwenye Katiba, tumekuja kwenye Dira na tumekuja kwenye Sera, yote yanazungumzia elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Waziri na pia, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuja na mabadiliko makubwa kwenye Sera ya Elimu. Hayo wanayotekeleza ni Katiba na ukiangalia Mheshimiwa Rais amekuja na mabadiliko makubwa, lakini pia ameongeza rasilimali fedha kwenye Wizara na kwenye taasisi, tunampa hongera sana. Sasa, tulikotoka kumetufikisha hapa tulipofika, hali ikoje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2023, FinScope wamefanya utafiti. Walipofanya utafiti wamekuja na matokeo ambayo yanatuambia hivi, kwa mwaka 2023 Watanzania ambao wana umri wa miaka 16 na kwenda juu, ambao wana elimu ya kuanzia tertiary na kupanda juu, ni asilimia tano tu ya Watanzania wote, lakini 26% ya Watanzania ni wale ambao wana elimu ya sekondari. Hii ndiyo elimu ambayo wameifikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu hizo zinatuambia, Watanzania ambao wamefikia kwenye elimu ya msingi tu peke yake mpaka sasa hivi ni 56%, lakini kuna Watanzania ambao hawana elimu kabisa, hao sasa hivi wamekuwa ni 13%. Hizi takwimu na huu utafiti unatupeleka wapi? Ukiangalia haya matokeo yanatupeleka mwaka 2023 ambapo Watanzania wenye uwezo wa kuongea na kuandika Kiswahili ni 79% tu, maana yake ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kama ni 79%, hao wengine hawana uwezo wa kusoma wala hawana uwezo wa kuandika Kiswahili. Ukienda kwenye lugha ya Kiingereza, utafiti unaonesha Watanzania wenye uwezo wa kuongea na kuandika Kiingereza vizuri ni 30%, lakini Watanzania 61% na kuendelea, hawana uwezo wa kusoma wala kuandika Kiingereza. Sasa, hii inatupelekea wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tunahitaji kufanya mabadiliko makubwa kwenye elimu yetu ili kuwaandaa Watanzania na hili ndiyo Wizara inakuja nalo na ndilo linalofanya kazi na ndiyo maana tunawapongeza, lakini ili tuweze kufanikiwa kwenye mabadiliko tunahitaji walimu ambao ni mahiri, tunahitaji wahadhiri ambao ni mahiri, ambao ni competent, watakaoweza kutupeleka huko tunakotaka. Ili tufikie hayo ni lazima maslahi ya walimu yaangaliwe na motisha iwepo. Mwalimu hawezi kuwa anasononeka halafu ukategemea kwamba, atatoa maarifa mazuri kwa Watanzania. Kwa hiyo, maslahi yao yaangaliwe na utaratibu wao uangaliwe vizuri, hii itawasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni utafiti kwenye vyuo vikuu na ushauri wa kitaalam ni muhimu mno katika maendeleo ya nchi yetu. Tunahitaji watafiti waisaidie nchi, sasa tunahitaji uwekezaji wa kutosha katika eneo hilo ili tuweze kufikia hapo, lakini zaidi ya hapo, tumesema na watu wamechangia kuanzia jana, taasisi inayosimamia ubora wa elimu ya shule za msingi na sekondari tunafikiri sasa umefika wakati iwe ni taasisi au awe wakala anayejitegemea, ili aweze kusimamia ubora ule unaotakiwa. Hili ni la muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo kwa sababu, elimu ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi ndiyo maana kule Mbozi, Vwawa, tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri anatujengea Chuo cha VETA, lakini bado hakijakamilika. Tunamwomba aongeze kasi, ili kile chuo kikamilike, tupate wataalam, tupate vijana ambao watakuwa wamesomea aina mbalimbali za ufundi. Pia, tunahitaji tawi la chuo kikuu angalau kimoja, Mkoa wa Songwe hauna tawi hata moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa pale tuko mpakani, tunataka Wazambia, Wamalawi, Wazimbabwe na watu wengine waje kusoma Tanzania watatuletea fedha za kigeni. Kwa hiyo, tunahitaji kujenga matawi na kuwatengeneza walimu wetu watoe elimu iliyo bora ili tuvute watu wa nje, tupate fedha nyingi, hii itatusaidia sana Mheshimiwa Waziri. Sasa katika hali hii tuliyonayo, tunapohitaji walimu wenye maadili, walimu ambao wamesomeshwa, pia, tunahitaji wapate elimu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi ukasoma mwaka 1980 ukaendelea kufundisha ukasema inatosha, ni lazima uendelee kujifunza kama Katiba inavyosema. Kwa hiyo, wawe na programu za kuwaendeleza walimu, si tu wa vyuo bali hata walimu wa shule za msingi na sekondari. Iwe kila mwaka, kila mwalimu akafundishwe, apate semina kidogo, angalau anazaliwa upya, anakuwa na uwezo wa ku-deliver na kuweza kutoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, tunahitaji vifaa vya kisasa vya kufundishia ili haya mabadiliko ya taaluma yatuwezeshe kuwaandaa Watanzania, tuondokane na hizi takwimu ambazo zinaonesha Watanzania wengi bado hatuna uwezo. Nchi inahitaji wataalam, tunahitaji watu wenye fani mbalimbali, wanahitaji kujielimisha, wakomae, wawe mahiri, wawe ni competent katika maeneo yote kwa kuwa na elimu, kwa kuwa na maarifa na kwa kuwa na ujuzi wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)