Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara ya Elimu. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa kutujalia uhai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha elimu kwa Watanzania. Napenda pia kuchukua nafasi hii kumpongeza Waziri wa Elimu Mheshimiwa Profesa Mkenda na Naibu wake Mheshimiwa Kipanga pamoja na watendaji wote wa Wizara hii. Pia, natumia fursa hii kuwapongeza walimu wote wa shule za msingi, shule za sekondari, shule za awali pamoja na wa vyuo vikuu nchini Tanzania, wanafanya kazi kubwa sana ya kuwaelimisha watoto wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nakwenda kuchangia kadiri ya wasilisho la Mheshimiwa Waziri. Kwanza kabisa napenda kuipongeza Serikali kwa kuja na mtaala mpya. Mtaala mpya ni mzuri na wazo ni zuri, lakini una mapungufu. Mapungufu hayo napenda kuyataja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaala tumeupokea, lakini katika upokeaji wa mtaala, hatukuwa tumejiandaa. Kwa nini nasema hatukuwa tumejiandaa? Nasema hivi kwa sababu, walimu wanaokwenda kufundisha ule mtaala, hawajaandaliwa. Wizara ya Elimu inasema imeandaa walimu, lakini walimu iliowaandaa ni imechukua walimu wawili kutoka kwenye shule; nafanya kama sampling, kwa mfano, Shule ya Nsemulwa, Mpanda, wamechukua walimu wawili wakaenda kufundishwa, lakini zipo shule nyingi ambazo wamechukuliwa walimu wawili wamefundishwa ili na wao wakawafundishe walimu wenzao. Nini maana yake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa walimu wawili waliochukuliwa kwenda kufundisha walimu wenzao, ina maana kama hawajaelewa kile kitu, basi na wao watakwenda kukifundisha vilevile. Hilo naona ni pungufu. Ni nini ushauri wangu? Ushauri wangu ni kwamba, ni kwa nini wasifundishe wakufunzi, wakawaita let say wakaenda pale Wilaya ya Mpanda, wakawaita walimu wote wakawafanyia hayo mafunzo? Suala la kuchukua walimu wawili kwenye kila shule na kwenda kuwafundisha, kuwafanya ndiyo wakufunzi, naona kama bado hapo kuna tatizo kwa sababu, wale ni walimu, hawawezi wakaenda kuwa wakufunzi, japokuwa wamewafundisha. Pia, wale walimu wengine wangependa wafundishwe kwa utaratibu unaofaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pungufu lingine ni vitabu na vitendeakazi. Kweli, mtaala umekuja, lakini vitendeakazi hakuna. Unakuta shule ina kitabu kimoja wanaambiwa watoe photocopy, lakini ukiangalia maisha ya vijijini hizo photocopy hakuna. Je, hizi shule za vijijini zitatoaje photocopy kwa ajili ya mtaala huu? Naona hilo nalo ni pungufu kwenye kutekeleza mtaala huu vizuri. Suala ambalo naliona hapa ni tulitakiwa twende taratibu, ili kutekeleza huu mtaala uweze kuwa vizuri. Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu huwezi kufanya test kwa wanafunzi. Unafanya majaribio ya mtaala wakati hujaandaa vifaa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo siyo sahihi. Ilitakiwa vifaa, kwa maana ya vitabu na kila kitu viandaliwe na walimu waandaliwe ili mtaala uanze. Hakuna mtu ambaye anakataza mtaala usianze, yote haya tunayapongeza ni juhudi nzuri, lakini tatizo ni ule utekelezaji, tulitakiwa twende taratibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kulizungumza hapa ni hizi shule za amali. Shule za amali hakuna kilichobadilika ni zile shule za ufundi za zamani ni kwamba, zimebadilishwa jina tu. Hizi shule za ufundi zilikuwepo na vitendeakazi vilikuwepo. Je, tumejiuliza kitu kilichoua zile shule za amali ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kilichoua zile shule za amali ambazo sisi tulisoma zamani ilikuwa ukifika, ukienda darasa la needle work, unakuta vyerehani vimekaa pale, ukienda darasa la cookery room unakuta majiko yamekaa pale, majiko ya gesi; kule mnafundishwa kupika, mnafundishwa usafi. Je, mnapoanzisha hizi shule za amali ni kitu gani kimebadilika? Vitendeakazi vimenunuliwa kwenye hizi shule za amali? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo shida ninayoiona hapa kwa sababu, hizo shule zipo ni jina tu limebadilika, badala ya kuita shule za ufundi zimeitwa shule za amali. Tukienda kwenye shule za technical college, tulikuwa na shule nyingi za technical college, kuna Moshi Technical, kuna Mkwawa, nyingi tu, lakini kitu kilichofanya zile shule zikafifia, ni vitendeakazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala ninalojiuliza ni tumeanza mtaala huu tangu Januari, je, hivi vitendeakazi vimeshafika hukou kwenye hizi shule? Jibu litakuja ni hapana. Hili naona kama ni suala ambalo tunakwenda kufanya test, kuwa-test watoto wakati tayari tukiwa tumeanza mtaala tangu Januari. Napenda Wizara ya Elimu kama ingelichukua hili jambo taratibu, liende taratibu, ifundishe walimu na pia iandae hivyo vifaa ili mtaala huu uweze kukamilika vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kulizungumzia hapa ni lugha ya kufundishia. Wazungumzaji waliopita hapa wamezungumza suala la lugha kwamba, huwezi kuachanisha Kiingereza na Kiswahili, ni lazima viende sambamba. Ili mwanafunzi au mtu aende kufundisha Kiswahili Marekani ni wajibu wake ajue Kiingereza, ili aende kufundisha Kiswahili China, sijui Japan, Australia, ni lazima ajue Kingereza. Sisi tuna matatizo ya walimu wa Kiingereza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, sijui hili umejipanga vipi ili kutoa hili tatizo la elimu kwa watoto wetu, hasa kwenye hizi lugha mbili, Kiswahili na Kiingereza kwa sababu, ndiyo lugha international ambazo zinaenda kwa pamoja. Hizo lugha nyingine ndiyo zipo, lakini tunaangalia Kiingereza kinazungumzwa kwenye nchi ngapi? Kinazungumzwa almost duniani kote kwa sababu, Kiingereza ndiyo lugha ya dunia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watoto wetu wengi wamekuwa wakienda kwenye interview, siyo kwamba watoto hawana akili, wanaelewa hayo mambo, lakini wanavyoenda ku-compete kwa sababu, hatujawaandaa vizuri, tunaonekana kwamba hatuna vijana wengi ambao wanafanya kazi kwenye hizo international organizations sababu ya lugha. Ningeomba Mheshimiwa Waziri suala la walimu wanaoenda kufundisha Kiingereza lichukuliwe kwa umuhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni marupurupu na stahiki za walimu. Walimu hawa ndio tunawategemea, kuna mwalimu unakuta anafundisha zaidi ya masomo matatu, lakini mwalimu huyu mshahara ni ule ule, anavunjika moyo wa kufundisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie madai ya walimu walipwe, lakini tuangalie ni jinsi gani tunawaongezea incentives wale walimu ambao wanafundisha zaidi ya masomo matatu. Kwa sababu haiwezekani mwalimu anachukua masomo matatu au manne, lakini bado mshahara ni ule ule, hamna anachoongezewa, anavunjika moyo. Nilitaka hili Wizara ya Elimu iliangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine Wizara ya Elimu ndiyo msimamizi wa Sera ya Elimu hapa nchini Tanzania. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri, leo wakati anakuja kuhitimisha hoja yake ya Wizara ya Elimu, atupe msimamo wake juu ya hawa walimu ambao wanalipwa na Serikali halafu wanakwenda kufundisha shule za private ambazo zimejengwa na Halmashauri zetu nchini, kwenye baadhi ya halmashauri na manispaa, ili tuelewe tunaendaje? Je, ni sahihi huyu mwalimu ambaye analipwa na Serikali kwenda kutumika kwenye shule ya private halafu ionekane kwamba mapato yametengenezwa na halmashauri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja. (Makofi)