Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia Bajeti ya Wizara ya Elimu. Nawapongeza sana Maprofesa; Profesa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Mheshimiwa Prof. Adolf Mkenda ambaye ndiye Waziri wa Elimu na QS wetu; Naibu Waziri, Mheshimiwa Kipanga na wasaidizi wote wa ofisi yetu mahsusi ya masuala ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi pia ni Mjumbe wa Kamati, na kwa nukta hiyo, maana yake nakubaliana na mapendekezo ya Kamati. Nimeshiriki kujadili kwa pamoja na kwa kweli tumefanya kazi usiku na mchana kwa ajili ya kuhakikisha tunatoa ushauri ambao Serikali ikiufanyia kazi, tuta-move. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wizara ya Elimu nitachangia hoja mbili na nafasi ikibaki nitachangia hoja ya tatu. Kipekee kabisa nilikuwa napitia hapa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020/2025 Sura ya tatu. Ieleweke tu kwamba huwa tunapitia ilani pia kwa ajili ya kuhakikisha tunajipima tumetoka wapi? Tulipanga nini? Tunakwenda wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika ukurasa wa 124 hapa nilikuwa napitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi, wameeleza katika huduma za jamii Sura ya tatu, nitanukuu: “CCM inatambua kuwa rasilimali watu ndiyo nyenzo muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Aidha, CCM inaamini kuwa elimu bora ndiyo nyenzo muhimu ya kujenga, kulea, kuendeleza rasilimali watu.” Nami nakubali kwa sababu nilishawahi kusema mara moja na ninarudia tena mara ya pili leo na pengine tutaendelea kujadili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiizungumzia Tanzania katika mambo tunayozungumzia katika sekta za uzalishaji zote ambazo tunazijua: madini, viwanda, biashara, kuna masuala ya logistics, kuna masuala ya utalii, zote ni sehemu ya sekta za uzalishaji, lakini miongoni mwa vitu ambavyo ni nyenzo ya kufanikisha, hivyo vyote ni rasilimali watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiizungumzia Tanzania, ukapanga mikakati yako yote, ukatengeneza mipango ya maendeleo ya miaka kumi, mipango ya maendeleo ya miaka mitano, mipango wa maendeleo ya miaka 50, lakini usizungumze kipengele cha rasilimali watu, maana yake hakuna utayekuwa umempangia. Ndiyo maana lazima tuzungumzie rasilimali watu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nasema nafurahi kuona kwamba ilani imezungumza hivi na wameipa hadhi, kwa sababu ni ukurasa wa 24, 25, 26, 27 mpaka 30 kote wamezungumza elimu peke yake. Sasa tukienda kwenye details, huko kuna vitu vingi, bado tunaendelea, bado miaka haijaisha. Kwa kuzungumza tu hivi, kwa kuipa hadhi kubwa hivi, kwa sababu ilani ina mambo mengi, elimu maana yake tumeona wame-consider.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jambo langu la kwanza katika hili hapa na ndiyo maana nimenukuu ni ubora wa elimu, kwa sababu CCM wame-specify kabisa kwamba inaamini katika ubora wa elimu. Nitaanza kwa kuuliza, na leo natamani tutafakari kwa pamoja. Nimechukua vitabu cha history hiki hapa cha advance (History One na History Two) halafu nina vitabu vya geography na biology.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kufanya sampling. Kwa hiyo, nimechukuwa masomo matatu; biology, history na geography. Geography na biology nimechukua vitabu vya Taasisi ya Elimu na naomba niwaambie waliyosema, sijui wako shallow! Hawako shallow.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taasisi ya Elimu wamefanya kazi kubwa, inawezekana changamoto ikawa sehemu nyingine na ndiyo vitabu vyao ambavyo nitavifanyia reference leo na najua siyo kosa lao, kuna changamoto nyingine. Hivi vingine ni vya waandishi wengine, kwa sababu bahati mbaya TIE hawajatoa kitabu cha History Two. Kwa hiyo, kuna History One peke yake, wanajua sababu pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika ubora wa elimu, nataka kutafakari, hivi elimu yetu baada ya kuwa tumerekebisha mitaala, baada ya kuwa tumerekebisha sera, baada ya kusema sasa hivi tunashauriana hapa tutafute fedha tuandike upya sheria ya elimu kwa sababu imepigwa viraka sana; Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978 tuiandike upya na Wizara ipo tayari kufanya hivyo; na kuna miongozo, kuna taratibu, kuna maandishi na kadhalika. Ni kitu kizuri, lakini hivi tumejiuliza kwenye hivyo vitabu kuna nini nasi tunataka ku-achieve nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mpango wetu ni kutengeneza kizazi cha watoto ambao watakuwa wafanyakazi wa watu wengine ni sawa. Ila kama tunatengeneza kizazi ambacho tunajua Africa is taking over, na kama tunajua Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo kuna paradigm shift kubwa sana ya global history (historia ya dunia), watu wanaoamini katika spirituality na sizungumzii dini, watu wanaoamini katika imani, wanajua hiki ninachokielewa. Tuko katika mhamo (shift) mkubwa sana wa kihistoria na kiimani wa dunia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama tunaendelea kuwaandaa watoto wetu wawe wafanyakazi wa watu wengine, tafadhali nisikilizeni na tutafakari wote tunafanyaje? Kwa sababu hii picha ya nje tumeifanya vizuri na ninawapongeza mno Wizara, lakini the content, nimechambua, nitaanza hapa kwenye geography. Hiki ni kitabu cha Taasisi ya Elimu na kitabu cha Form Four, hiki hapa na watoto wanasoma, nimeweka hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna topic humu zipo nyingi sana, lakini topic ambayo nimeona ni relevant na ninaomba nianze kuwapongeza kwa hilo, ni topic inaitwa Environmental Issue and Managements. Wamezungumza vitu ambavyo kwa kweli wamefanya kazi na ni current. Kuna vitu vingi ambavyo ni current nitavi-challenge tu kidogo. Kuna baadhi ya vitu hawajaviweka, sijui tunaogopa kuwaambia nini watoto wetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kwenye climate change, kwa sababu mimi ni mdau wa climate, tumezungumza, lakini hatujasema kwamba sisi Afrika hata percentage ya emission ni ndogo, lakini the industrialized countries, nchi zilizoendelea ndiyo wanaosababisha athari ya climate ambapo sisi ni waathirika wakubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima watoto wetu wajue tangu wanasoma ili wawe wanajua tuna vita ya Global North and Global South. Ndiyo maana nauliza, au sisi ni viranja? Sisi nchi za Afrika ni viranja? Au kuna watu wengine ambao wametupa sisi kazi na wanatukagua tunaandika nini, ndiyo maana hatuandiki vya ukweli? Kwa hiyo, nawa-challenge hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine humu humu kwenye geography kuna sehemu nimepa-note kabisa pamenisikitisha. Hiki kitabu cha Tanzania wanasoma watoto wa Tanzania, lakini hapa kuna sehemu kwenye list huku ukisoma kitabu utaona nime-note, temperature and rainfall distribution for Bulawayo Zimbabwe; Temperature and rainfall distribution for Brazil; temperature and rainfall distribution for Manila Philippines; temperature and rainfall distribution for Salaa Algeria; temperature and the list goes on Lima Chile, Namibia, Chile, Greece, Tokyo – Japan, U.S.A the list goes on. Sijui tunataka tu-achieve nini? Bado tunaendelea kusoma haya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii ni sehemu moja. Hiki hapa pia cha biology ni cha Form Four. Sasa labda mtatusaidia ambao ni watalamu zaidi. Do we still need to label flower plant parts? Nini parts zile za ua? Hibscuss flower, tuna label pale juu tunakuwa tunataka ku-achieve nini? Samahani sana, mimi nilifikiri geography ilipaswa ituambie katika nishati, katika mifugo na uvuvi, content za Maafisa Ugani zilitakiwa ziwe kwenye vitabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifikiri watu wa Wizarani na sekta za uzalishaji, jambo la kunenepesha mifugo linatakiwa liwe kwenye geography ya Form Four kwa sababu watoto wengi tukiita hapa nje wako…
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa…
MWENYEKITI: Taarifa inatoka wapi?
TAARIFA
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe Taarifa…
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia hoja ya mwisho ya vitabu…
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe taarifa mzungumzaji…
MWENYEKITI: Ngoja nimpe hiyo Taarifa mara moja. Mheshimiwa Kembaki, taarifa.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba kumbe amekubaliana na hoja yangu kwamba TIE inatengeneza vitabu ambavyo viko shallow sana, havizingatii hali halisi ya Mtanzania na nchi yetu kwa ujumla.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Nusrat unaipokea hiyo taarifa?
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei, na mwanzo nilisema hivi, Mheshimiwa Waziri ni Profesa na yupo na jopo la wataalam. Tunapaswa tujadili, kwa sababu, ngoja nikwambie, TIE wamepewa terms of reference, wanaenda kuandika nini kwenye vitabu. Labda tunatakiwa sisi tujadili tunataka tusomeshe watoto wetu nini? Tunataka kua-achieve nini ili TIE wakaandike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TIE wanaweza kuandika chochote ambacho watapewa terms of reference. Kwa hiyo, siyo jambo la u-shallow wa TIE, na tafadhali, kwa sababu tunataka TIE waandike vitabu vyetu, tunataka uniformity kwa ajili ya watoto wetu waweze kusoma vitu vinavyoeleweka na siyo issue ya biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, nitazungumza sehemu moja kwenye History Two; katika hizi topic saba ambazo ziko hapa mbele, kuna The Raise of Capitalism in Europe, topic ya kwanza; ya pili, The Raise of Democracy in Europe; Imperialism and World Division; Raise of Socialism; na Super Power. Topic ya mwisho tu ndiyo relevant.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashauri kwamba hizi topic zote tuziweke kwenye vitabu vya ziada. Vitabu vya watoto wetu kusoma darasani, tuwafundishe watoto wetu Neo Colonialism and The Way Europe underdeveloped Africa. Tafadhali sana, hatutaki kuona watoto wetu wajinga. Samahani na with due respect, sizungumzi kwa ubaya kwa sababu mjinga ni mtu asiyefahamu na akifahamishwa ataelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatakiwa tufundishe watoto wetu jinsi ambavyo tulikuwa matajiri na something went wrong somehow somewhere, ndiyo maana leo tuko hapa. Kitabu kizima kilitakiwa kijae ukoloni mamboleo (Neocolonialism) na namna ambavyo nchi za Wazungu zilisababisha sisi tukawa maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huku kote tunajadili, nitasoma sehemu moja tu, kwa heshima yako na samahani sana, nataka tu niwatie hasira. Najua Mheshimiwa Waziri pia hafurahii. Kuna sehemu humu napata shida kupapata, lakini kumeandikwa Camp David. Tunafundishwa hapa tunaona Camp David Marekani, Jimmy Carter. “The Camp David Accord September 1978, Camp David in Military Camp in the U.S.A where President Jimmy Carter…”
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MJUMBE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wake umeisha anamalizia. Kwa hiyo, hamna taarifa.
MJUMBE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. NUSRAT S. HANJE: …History two, nitazungumza hili kwa ajili ya Muungano na ninaomba kama mna…
MJUMBE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanaongea ovyo kuhusu Muungano, ni kwa sababu inawezekana kuna vitu hatujavipa hadhi ya kutosha kuelezea faida za Muungano.
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Nusrat.
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hapa ni History One na mnavyojua History One huwa imeelezea historia ya nchi. Sisi hapa Tanzania kwa waliosoma history, topic ya saba karibia na mwisho mwisho ukurasa wa 264 ndiyo imezungumza political and economic development in Tanzania since independence. Karatasi moja na nusu ndiyo imezungumza kuhusu Muungano, wameweka mpaka picha ya Nyerere. Tafadhali andikeni, chukueni nyaraka za waasisi wa Muungano.
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Nusrat. (Kicheko)
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, tengenezeni vitabu watoto wajue, wasome, watu waache kudharau Muungano. (Makofi)