Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze mchango wangu kwanza kwa kumshukuru Mungu kwa fursa ambayo nimeipata. Kulingana na muda, naomba niwapongeze sana Wizara ya Elimu, Mheshimiwa Prof. Mkenda na timu yake pamoja na watendaji kwa kazi nzuri ambazo wanafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitajikita katika point mbili tu kwenye yale majukumu ya Wizara. Jukumu la kwanza, naomba ni-quote: “Kutunga na kutekeleza Sera ya Elimu, Utafiti, Huduma, Maktaba, Sayansi, Teknolojia, Ubunifu na Uendelezaji Mafunzo na Ujuzi.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile ya pili ya Kusimamia Elimu ya Msingi, katika Sera ya Elimu Na. 25 ya Mwaka 1978 inaruhusu watoto wa elimu ya msingi kwa shule binafsi kuweza kuhamia katika shule za Serikali, lakini sera hiyo hiyo hairuhusu watoto wa sekondari kuhamia kutoka private kwenda shule ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilichokuwa nataka kuomba, kuna mazingira ambayo yanachangia mpaka wazazi kutaka waombe watoto wao watoke kwenye private school kurudi kwenye shule za Serikali. Unaweza ukakuta ni wazazi kutengana, wazazi kufa, walezi kuishiwa uwezo wa kumwendeleza mtoto. Awali alifikiri atamsomesha katika shule ya private, lakini amejikuta mahali fulani hawezi tena kuendelea. Sasa kwa sababu sera yetu ya elimu inayazungumzia masuala haya, basi tuone namna bora ya kuweza kubadilisha. Kama tunaruhusu primary, basi na kwa sekondari turuhusu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la mafunzo na ujuzi. Moja ya vipaumbele ambavyo Wizara imeelezea ni suala la Wizara kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa mafunzo ya amali kwa shule zetu za sekondari na vyuo vya ufundi. Sasa changamoto ninayoiona hapa, katika elimu ambayo tayari wameshaitoa kwa maana ya walimu kuwapa elimu ya hii mitaala mipya wamekwenda katika shule 181,777. Kati ya hawa, shule za msingi ni 155,476, lakini wale walimu wa shule za awali ambao wamepata haya mafunzo ni walimu 7,454, sawa na asilimia nne, ukilinganisha na wale wengine wa darasa la kwanza mpaka la saba 148,019 sawa na 86% na hawa wengine ni asilimia nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa changamoto ninayoipata hapa, msingi wa mtoto unajengwa akianzia kwenye shule ya awali, lakini ukiangalia idadi ya walimu waliopata mafunzo hayo ni wachache, lakini ukienda pia hata kwenye suala la uandikishaji ambalo linafanywa mara nyingi na TAMISEMI, wanaoandikishwa kwenye shule za awali ni wachache ukilinganisha na wanaondikishwa katika darasa la kwanza. Maana yake ni kwamba kuna watoto wengi wanaingia darasa la kwanza bila kupitia shule za awali ambako ndiko upo msingi mtoto anatakiwa kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali, nilikuwa naona, kwa sababu tunahitaji kila mtoto apitie katika shule ya awali, uandikishaji uwe kwenye shule ya awali tu na wataendelea hivyo, kusiwe na uandikishaji mwingine kwenye darasa la kwanza, kwa sababu lengo letu ni kuona mtoto anajengewa mazingira mazuri akiwa bado mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukimwandikisha awali, unaandikisha tuseme 100,000; darasa la kwanza unaandikisha 200,000. Maana yake ni kwamba kuna 100,000 pale hawakupitia yale mafunzo ya awali ambayo wanatakiwa kujengewa msingi watoto wadogo. Kwa hiyo, niliona hili tuone namna bora ya kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la watoto wenye ulemavu (wenye mahitaji maalum), tunazo shule zetu ambazo walimu 920 wamepata mafunzo na shule tulizonazo ni nyingi. Bado wasiwasi wangu ni ule ule, je, walimu hao watakidhi mahitaji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua mfano tu, kwenye Jimbo langu la Ilemela tunazo shule 10 na ni shule nyingi, lakini walimu waliopo ni 15. Ni wastani wa walimu wawili kwa shule moja labda, maana huwezi kusema mwalimu na nusu. Sasa nashauri hapa kwamba tuone namna bora ya kuwajengea mabweni na kupunguza utitiri wa hizo shule ili waweze kupata mazingira mazuri ya kujifunzia na kufundishwa kwa maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kufanya hivyo, tutakuwa na shule nyingi, lakini walimu hawatoshelezi. Waliopata mafunzo katika huu mtaala mpya ni wachache, matokeo yake bado watoto wale watakuwa wanakwenda bila kufikia hatma ambayo pengine tunahitaji katika kuwajengea ujuzi tunaotaka kuufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali katika ujenzi wa shule 100 za ufundi. Tunakwenda kuwajengea watoto wetu mazingira mazuri. Rai yangu kwa Serikali, kwa sababu tumeelekea uelekeo huo, naomba sana watoto wale wanapomaliza shule, kwa sababu ni shule za sekondari za ufundi, basi wanapomaliza wapewe mitaji ya vifaa vya kutendea kazi. Kwa kuwa wamepata ujuzi, wanatakiwa pia kama hawataendelea na chuo kikuu na mambo mengine, wanatakiwa kwenda kujiajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuta mtoto amemaliza sekondari, kapata ujuzi, lakini ujuzi ule hawezi kuutumia, nasi tunataka kupunguza tatizo la ajira katika nchi yetu. Kwa hiyo, lazima tuangalie namna bora ya kuwawezesha vitendea kazi ili wanapomaliza shule waweze kuendelea na maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili naishukuru sana Serikali kwa sababu, moja ya shule za ufundi zitakazokwenda kujengwa na Wilaya ya Ilemela imebahatika. Namshukuru sana Waziri kwa sababu wananchi waliamua kutoa eneo lao la ekari 50 ili waweze kupata fursa hii. Nashukuru katika orodha ambayo iko katika watakaopata, na wilaya yangu itapata. Mheshimiwa Waziri, nakushukuru sana pamoja na timu yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kushauri, vyuo vyetu vingi vya kati vilipandishwa hadhi na kuwa vyuo vikuu. Tunapokwenda maofisini, kule kuna changamoto na matatizo ya kiutendaji, watu wengi pale wamekaa kama mabosi kwa sababu kila mmoja ana degree, ana masters, ana Ph.D. Hakuna wale watendaji ambao tunaweza kuona kwamba wanaweza kuwa ni technical clerk katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, katika suala zima la urejeshwaji pengine kwenye vyuo vyetu vya kati vya ufundi tuweze kuona vilivyopo visipandishwe tena hadhi, lakini tuendelee kuongeza vingine ili tuweze kupata wananchi au wanachuo wenye ujuzi ambao wataweza kufanya kazi hii vizuri katika utendaji na katika shughuli zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine pia katika uwezeshwaji wanafunzi ni kwenye chakula. Sasa hapo kuna changamoto moja ambayo pengine naomba Serikali itusaidie kwa maana ya Wizara. Ukiangalia fedha zinazotengwa kwa ajili ya watoto walioko shule ya bweni, kwa chakula wanatengewa shiling 1,500/=, lakini aliyeko chuo cha ualimu chakula anatengewa shilingi 5,000/=, aliyeko chuo kikuu chakula anatengewa shilingi 10,000/=. Sasa hawa ina maana na aina ya vyakula ni tofauti, kwa maana ya mahitaji, kwamba mwingine anahitaji labda chakula ambacho kina bei kubwa sana na mwingine bei ya kawaida! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifikiri pia tuangalie namna ya ku-review upya, pamoja na kwamba hii ya shule za bweni inawezekana ikawa TAMISEMI au namna gani, lakini ningeweza kuishauri Serikali hebu tu-review pia rate za vyakula ambazo tunawapa watoto walioko bweni na wale ambao wako vyuo vya Ualimu na Chuo Kikuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapokuwa wa mwisho mwisho, unakuta mambo mengi yamezungumzwa. Nizungumzie suala la mikopo wanayopewa wanafunzi wetu, kuna kuchelewa sana kupata na kunamfanya mwanafunzi pia achelewe kuwa registered katika shule yake. Matokeo yake sasa watoto wengi wanaanza kuhangaika, na wengi wanakuwa kama ombaomba, maana hawana uhakika na future yao kwenye elimu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana katika hili, basi iwe inatoka mapema kama ambavyo Mheshimiwa Dkt. Paulina aliongelea. Maana kunakuwa na ucheleweshwaji sana; kuna awamu ya kwanza, ya pili sijui, kwa maana ya madirisha kidogo nayo yana changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuwa na bweni katika maeneo yao, mtoto wa mwaka wa kwanza anawekwa hosteli; akiingia mwaka wa pili anatakiwa atoke, kule mitaani ndiko wanakoharibikia. Naomba sana tuone namna bora ya kuongeza idadi ya hosteli katika vyuo vyetu. Mtoto wa mwaka wa kwanza na wa pili bado ni kijana mdogo, bado anahitaji pia kuwa katika maadili ndani ya chuo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana, badala ya kuwa-phase out kwamba huyu amemaliza mwaka wa kwanza aondoke aingie mwingine, bado kule anaenda kutangatanga. Ndiyo unakuta watu wanaolewa, yaani anatafuta kwa kila hali ili aweze kumudu maisha, lakini bado ni wadogo sana. Naomba sana hili, tuone namna bora ya kuwaweka watoto wetu chuoni na tusiwapeleke kwenda kupanga nje ya chuo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine naipongeza sana Serikali kwa namna ambavyo imeendelea kutenga fedha za maendeleo katika Wizara hii ya Elimu. Mwaka 2023/2024 walitengewa shilingi trilioni 1,137 na point lakini fedha ambazo wameweza kupewa mpaka Aprili 15 ni shilingi bilioni 979.1 sawa na 87%. Kwa hiyo, hii kidogo inatia moyo. Tuna imani ya kwamba mpaka kufikia Juni pengine zitakuwa zimekamilika ili vile viporo alivyokuwa anavisema Mheshimiwa Dkt. Ntara katika ujenzi wa mabweni vitaweza kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza pia kwa kuongeza hiyo bajeti ya shilingi trilioni 1.9, bado ni ndogo kwa elimu, lakini basi kama itatoka iweze kutoka yote. Hii Wizara ina mambo mengi ambayo yanajenga msingi wa maendeleo katika nchi yetu. Bila elimu ambayo imekaa vizuri, ambayo imewezeshwa tunaweza tukajikuta tunakwenda katika mambo ambayo siyo sahihi sana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali, kwa bajeti iliyotengwa, iweze kutoka yote na waweze kupanga na kutekeleza majukumu yao waliyoyapanga ili tuweze kwenda vizuri.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili ya muda, basi naunga mkono hoja na natoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais ambaye dira yake katika Hotuba yake ya Aprili hapa 2021 ndiyo imefanya pia Wizara ya Elimu waende vizuri. Hongera sana kwa Mheshimiwa Rais. (Makofi)