Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Eng. Mwanaisha Ng'anzi Ulenge

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi. Awali ya yote, namshukuru Mungu kusimama mahali hapa jioni ya leo. Kipekee kabisa nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye suala zima la elimu nchini. Sitaki kurudia kusema yapi yamefanyika, siyo tu katika miundombinu, Mheshimiwa Rais ameonesha dhamira kuhakikisha tunakwenda katika elimu ambayo inaitika katika mahitaji ya jamii, mahitaji ya mazingira na mahitaji ya wakati wa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha elimu inakuwa bora kuendana na Mipango ya Taifa na mahitaji ya kitaaluma, nawapongeza sana Mawaziri mnaofanya kazi katika Wizara hii. Naomba niwatie moyo, wakati ni sasa, wala tusisubiri kufanya baadaye eti ili tuwe tunafanya kwa ukamilifu. Kwa hakika tumeshachelewa, tuanze kufanya sasa hata kama hatujakamilisha, along the way tunapunguza upungufu wetu na mwisho wa siku tutafikia ukamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa naomba niseme kwamba, nimeisikiliza hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ameeleza vizuri hatua mbalimbali iliyochukuliwa na Serikali katika kuimarisha ubora wa mafunzo ya amali na mafunzo ya ufundi stadi, amezungumza vizuri ongezeko la vyuo vetu vya VETA, pia amezungumza suala zima la ongezeko la wanafunzi wa VETA, vilevile amezungumza suala zima la INTEP program (Integrated Training for Entrepreneurship Promotion). (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naiona dhamira na mwelekeo, naona tunapokwenda. Niwatie moyo, nimeona suala zima la VETA kwa kushirikiana na vyuo vya nje, vilevile naona zile VETA 64 ambazo zimeanzishwa, yote haya yanaonesha dhamira ya Wizara hii ya kuhakikisha elimu yetu inaitika katika mahitaji ya jamii ya mazingira na wakati wa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha uwezo wa nchi katika tafiti, matumizi ya sayansi na teknolojia na ubunifu ili kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda, ninashauri Serikali ifanye yafuatayo: -

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ambalo ninaishauri Serikali, wenzangu wengine wamesema hapa, VETA iweze kufanya tafiti katika Wilaya zetu na maeneo yetu, kubaini rasilimali tulizonazo na itengeneze mitaala kulingana na rasilimali zilizopo katika maeneo yetu ili kuongeza thamani ya vitu vilivyopo na kuibua ubunifu na ajira kwa vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, pale kwetu Mkinga tumeanzishiwa VETA. Pale Mkinga kuna madini ya kutosha ya Tanga Stone, tunaomba VETA ihakikishe inashirikiana na vile vyuo vya kuongeza ubora na thamani ya madini, kuhakikisha tunapata mitambo kuwezesha vijana wa pale, kuhakikisha tunazalisha ajira na ubunifu na ku-add value katika madini yale kwa mustakabali mpana wa vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile, ninaishauri Serikali ione namna ya kuhamasisha kuanzishwa kwa professional bodies ili tuweze kupunguza mianya kati ya wanachuo wanaotoka shuleni na waliopo mtaani. Lazima isimamiwe professional bodies zianzishwe. Tunajua mtaani kuna wanataaluma wazoefu na wenye viwanda waweze kuunganisha nguvu kwa pamoja kuondoa gap (academic gap) kwa wanafunzi wanaotoka vyuoni ili jamii iweze kupata tija kwa haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, mwanafunzi yeyote, awe ni mechanical engineer au electrical engineer, anapoingia chuoni, akisajiliwa kama mwanafunzi au mjumbe wa bodi ya mechanical engineers Tanzania, itawezesha mwanafunzi yule anapofanya tafiti zake, kwenda kutengeneza makongamano kwenye hizi bodi huku mtaani na kuweza ku-share kile anachokifanya na hawa huku wazoefu mtaani ili kuondoa lile gap na ku-share maarifa yale. Hii itasaidia kuibua the state of art technology. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumesema, ili elimu yetu iwe bora kuendana na mipango ya Taifa, maana yake elimu ni cross cutting issue. Kwa hiyo, ni lazima tuone ni kiasi gani Wizara hii inakuwa pro-active enough kugundua gaps zilizopo mtaani na namna ya kuhakikisha zinazibwa haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile najua bodi hizi huwa zinakuwa ni bodi binafsi, kama vile Taasisi ya Wahandisi Nchini ni bodi binafsi, lakini kwenye taasisi ile utakuta wahandisi wote tuko ndani ya umbrella moja, lakini tukigawanywa kwa mujibu wa taaluma zetu na tukishirikiana na vyuo vikuu vyetu na Maprofesa wale wakiweka kwa pamoja mipango ya kuanzishwa makongamano ambayo yatasababisha kufanya tafiti, tafiti zao zinakuja huku mtaani kwa wataalamu na baadaye zinakuwa published. Itasaidia sana kupata the state of art technology ambayo inakuja kusaidia ukuaji wa taaluma, ajira na ubunifu katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo wameweza kushirikisha VETA na nchi nyingine tano kwa mujibu wa taarifa ya Mheshimiwa Waziri, vilevile tunaweza kupata uzoefu kutoka kwenye nchi mbalimbali ambazo zina hizi professional bodies. Zipo nchi ambazo mpaka sasa zinafanya makongamano ya miaka 60 ya Technical Engineers labda, au miaka 60 ya Electrical Engineers. Muda wote huo wamekuwa wakikusanya taaluma mbalimbali kwa kushirikiana na vyuo na zile professional bodies.

Mheshimiwa Spika, nafikiri nasi tukajifunze pia kutoka kwenye nchi za wenzetu ili tuweze kuanzisha hizi bodi kupunguza gap la elimu nchini kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile ili kuchochea tafiti ni lazima tuanze na maktaba kwenye maeneo yetu. Hebu tujiulize huko kwenye Wilaya zetu, maktaba zetu zipo katika hali gani? Utakuta maktaba hazipo. Kuna majengo tu yamewekwa hayana vitabu. Hatuwezi kuhakikisha tunafanya tafiti za maendeleo kama watoto huku chini hawajengewi utamaduni wa kujisomea katika maktaba zetu ambazo zipo.

Mheshimiwa Spika, maktaba ya Tanga imeanzishwa mwaka 1958, lakini ni chakavu kupitiliza, na ipo Tanga Mjini. Hapo tunaibua vipi mambo ya kufanya tafiti. Hata walimu waliopo kwenye Mkoa ule hawaoni haja ya kuwasogeza watoto kwenye maktaba zile ili kujenga utamaduni wa kujisomea na kuweza kuibua tafiti. Tafiti unazipataje kama hufanyi literature review? Unazipataje tafiti kama hujui wengine wamefanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru Makamu wa Rais wetu, alipokuja Tanga nililiibua hili na ninashukuru sana Prof. Franklin, nimeambiwa hatua ambazo amezichukua kuhakikisha kwamba vitabu vya kiada vimekwenda na Maktaba yetu ya Tanga inarekebishwa. Naomba sana maktaba zote katika Wilaya zetu ziweze kutengenezewa uwezo wa kuwa na vitabu vya kutosha na walimu waone dhamira ya dhati kuwapeleka vijana karibu na maktaba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maktaba siyo magofu ya kumbukumbu, maktaba ni mahali ambapo wanafunzi wanapaswa kwenda kuwekwa karibu na kujisomea. Walimu wanapaswa kuwa na hamu hiyo kuwajengea uwezo, la sivyo kama huku chini hawajapata hayo, hawezi kwenda chuo akasoma reference books. Atakuwa anatoka kwenye vitini vya walimu mle, mwisho wa siku anakuja mtaani mnasema wanafunzi wa vyuo vikuu wapo shallow, kumbe kule chini hawajajengewa utamaduni wa kuanza kusoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile naomba kusema yafuatayo: Naomba nizungumzie kuhusiana na Tume ya Mionzi Tanzania (TAEC). Kuna mradi wa Multipurpose Food Radiator ambao uko pale Msakuzi. Mradi huu utatugharimu almost eight billion.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, naona umekaa sawasawa. Ahsante sana. (Makofi)