Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hii na kibali cha kuweza kusimama na kuweza kuchangia hotuba hii. Nawashukuru sana Waziri, Naibu Waziri, watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, nawapongeza wafanyakazi wote wakiwemo walimu katika nchi yetu ya Tanzania kwa kazi kubwa ambayo wanakuwa wanaifanya kuhakikisha kwamba elimu inaboreka katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa bajeti hii na moja kwa moja ninaiunga mkono. Kwa nini ninaiunga mkono? Ni kwa sababu Wizara hii imekuwa ikitekeleza majukumu yake. Kwa mwaka wa fedha 2023/2024, imeweza kutekeleza miradi ya maendeleo kwa 68% na fedha ambayo iliidhinishwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ilikuwa 68%. Kwa hiyo, naweza kusema kwamba wametekeleza kwa jinsi ambavyo waliweza kupatiwa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa bajeti ya mwaka huu tumeona ongezeko kubwa la Bajeti ya Wizara hii ya Elimu. Zaidi ya 13.74% imeweza kuongezeka. Ukiangalia kwa mtiririko, kwa miaka mitatu zaidi, Wizara hii imekuwa ikiongezewa fedha. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuona umuhimu wa sekta hii ya elimu.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, mwaka 2021/2022 Wizara hii ilitengewa shilingi trilioni 1.446 lakini mwaka 2022/2023 ilikuwa shilingi trilioni 1.493, mwaka 2023/2024 ilikuwa shilingi trilioni 1.675 na mwaka huu 2024/2025 wameweza kutengewa bajeti ya shilingi trilioni 1.905. Kwa kweli haya ni maendeleo makubwa sana kwenye sekta yetu ya elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumeona katika bajeti hii Wizara imekuwa na vipaumbele. Katika mojawapo ya vipaumbele ambavyo wamevitaja ambavyo wanavifanyia kazi ni huduma ya maji na usafi wa mazingira. Katika kipaumbele hiki, cha kushangaza ni kwamba, fedha za ndani hawakupanga fedha yoyote isipokuwa kwa fedha za nje wamepanga shilingi bilioni 1.2. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa najiuliza, kipaumbele hiki cha huduma ya maji na usafi wa mazingira ndicho kipaumbele ambacho kwa asilimia kubwa shule zetu hasa za msingi na sekondari zinaguswa moja kwa moja. Sasa kama fedha ya ndani hatuoni umuhimu wa kutenga bajeti, tunategemea vyoo wanavyotumia watoto wetu tupate msaada, je, tutafika?
Mheshimwia Spika, napenda Mheshimiwa Waziri aje aniambie hapa atakapohitimisha, ni kwa nini katika kipaumbele ambacho ninyi wenyewe kama Wizara mmekiainisha lakini hamkupanga fedha za ndani, mnategemea fedha za nje? Je, ni kweli tutakidhi takwa la kuhakikisha kwamba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanapata vyoo safi na salama kwa fedha hii ambayo wamepanga kwa kutegemea wafadhili? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ina maana mfadhili asipotoa hii fedha watoto wetu hawatakuwa na vyoo, wala hawatakuwa na maji salama. Naomba Mheshimiwa Waziri anieleze ni kwa nini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna kipaumbele kingine ambacho mmesema mtaimarisha uwiano wa kitabu kwa mwanafunzi ngazi ya msingi, sekondari na huduma za maktaba. Katika kipengele hiki mmetenga fedha za ndani shilingi bilioni 1.5. Tunashukuru kwa kutenga hiyo fedha, lakini najiuliza, hii shilingi bilioni 1.5 kwa mikoa tuliyonayo Tanzania na kwa maktaba ambazo tunazo na mna-plan kujenga maktaba nyingine, hii maktaba itakuwa Makao Makuu ya Mkoa; yule mtoto anayetoka Mwashilugula kule Shinyanga, anayetoka Mwakitolyo, ataweza ku-afford kuja mkoani hapa kwa ajili ya kutafuta huduma ya maktaba? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa huyu mtoto atahitaji rasilimali fedha, je, mzazi ataweza kumpa mtoto wake fedha atoke kijijini aje mjini kwa ajili ya kufuata maktaba? Kwa nini fedha hizi msizielekeze kwenye suala zima la kuchapisha vitabu ili kila shule iweze kuwa na vitabu vya kutosha kwa ajili ya wanafunzi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo, kwenye taarifa yenu mmesema kwamba mmeshaanza uchapishaji wa vitabu na kuna baadhi ya vitabu takribani kama 9,000 ambavyo vimeshaanza kusambazwa, lakini kuna vitabu ambavyo kwa taarifa ambazo ninazo mnavituma online, mnatuma kwa softcopy. Sawa, mmewapa walimu vishikwambi, je, ni walimu wangapi ambao wanaishi kwenye mitandao ya internet? Ni walimu wangapi ambao wanaweza waka-afford ku-download hivyo vitabu na kuweza kuvi-distribute kwa wanafunzi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali haioni kwamba inazidi kuongeza mzigo kwa walimu hawa ambao wanaishi katika mazingira magumu ambao kwa kweli hawana hata motisha ya kazi ngumu wanayoifanya ya kuelimisha watoto wetu? Kwa nini tusichapishe vitabu vya kutosha badala ya kufikiria kujenga?
Mheshimiwa Spika, maktaba siyo mbaya, siyo mbaya kabisa, tunahitaji watoto wetu waweze kusoma, lakini mazingira ya hizo maktaba ndiyo shida. Unakuta maktaba iko mkoani, sidhani kama kuna wilaya ambazo zina maktaba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa, kama maktaba mnajengea mkoani, hao watoto wa vijijini watafanya nini? Kwa nini msije na mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba mnachapisha vitabu vingi vya kutosha halafu mnavisambaza kwenye shule? Kwa sababu, mkiendelea kusema mjenge maktaba, sawa ni wazo zuri lakini mwatumie walimu vitabu kwenye vishikwambi vyao ili wao wavizalishe, tunawapa kazi ambazo sidhani kama wataweza kuzitekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine tumeona kuna sheria ambayo inasimamiwa na Wizara hii, Sheria Na. 25 ya Mwaka 1978 imekuwa ikifanyiwa marekebisho madogo madogo mara kwa mara. Mimi ninachokiona, kwa sababu sheria hii na kanuni na miongozo imekuwa ikikinzana na matakwa ya Sera ya Elimu ya Mwaka 2014, Toleo la Mwaka 2023, unakuta kwamba anayesimamia mipango, hata fedha ambayo tutaipitisha leo, fedha nyingi itaenda TAMISEMI, haitabaki Wizara ya Elimu. Itakwenda TAMISEMI ambako ndiyo wana elimu za sekondari, wana elimu za msingi na VETA sasa hivi ziko huko, na kuna vyuo ambavyo viko kule. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nafikiri kuna umuhimu wa kufanya marekebisho na mapitio ya sheria hii ili sasa kusiwe na mkanganyiko, kusiwe na sera ambazo zinakinzana, kwa sababu kumekuwa na miongozo mbalimbali ambayo inatolewa. Unajikuta wakati mwingine hiyo miongozo ambayo inatolewa inakinzana na sheria iliyopo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mtekelezaji ni TAMISEMI, lakini elimu anasimamia ubora wa elimu, anahakikisha kuna vitabu, anahakikisha mitaala ipo, inafuatwa vizuri, lakini REO na DEO wako chini ya TAMISEMI. Yaani pale mkoani anasomeka kama mwakilishi wa Kamishna ambaye Kamishna yuko Wizara ya Elimu. Mimi ninaona kama kuna mkanganyiko, kuna vitu ambavyo vinaingiliana.
Mheshimiwa Spika, basi ni wakati mzuri wakae chini; najua wamejaa maprofesa na madaktari, nafikiri kuna umuhimu sana wa kuboresha hii Miongozo, Kanuni na Sheria ili kusiwe na mwingiliano. Shule nyingi ziko kule; shule za msingi, sekondari, vyuo, kusiwe na mwingiliano ili basi mipango hii mizuri ambayo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaipanga, iweze kutekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Ooh!
Mheshimiwa Spika, nimeshaunga mkono hoja. Naomba sana, sana, sana kufuatilia. (Makofi)