Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii ya Elimu. Namshukuru Mheshimiwa Rais kwamba ameendelea kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu, hasa kuanzisha mitaala mipya ambayo ninaamini kwamba Watanzania wote wanaunga mkono maboresho haya ambayo Mheshimiwa Rais ameruhusu yafanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Profesa na wenzanke wanafanya kazi nzuri, akiwepo mwalimu wangu wa Chemistry, first year, University of Dar es Salaam, Prof. Mdoe, CH 100. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii ni Wizara muhimu sana, ni software. Tunatengeneza Watanzania wa miaka 100 ijayo. Kwa hiyo, nafikiri Mheshimiwa Waziri hata anapokuja kujibu na kuhitimisha hoja, yaani inabidi achukue hoja za Wabunge kwa umakini mkubwa. Kuna mengine yanahitaji majibu ya moja kwa moja akayafanyie kazi kwa maana ya kuboresha with time, kwa sababu, maboresho haya hayachukui muda mwingi, hapa huwezi kuimarisha leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, target ya Serikali hapa ni kwamba tuna changamoto kubwa sana ya ajira. Kwa hiyo, tunatarajia baada ya kuanzisha mitaala mipya tupunguze vijana wa Kitanzania ambao wamesoma na hawawezi kujiajiri. Kwa hiyo, aweze kuajiriwa, lakini pia aweze kujiajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapo kuna hoja nyingi sana. Kuna upinzani kwamba kwa nini leo unawaambia watu wakajiajiri wakati ninyi mmepata ajira ya Serikali? Kwa hiyo, unahitaji kufanya kazi kuwafanya watu waelewe tunalenga kitu gani? Lazima wakubali kwamba wakati ni ukuta, kwamba, kuna muda ambao Serikali iliweza kuajiri watu, kwa sasa wasomi wote hawawezi kuajiriwa na Serikali. Yaani wakubali hivyo, then tutengeneze namna bora ya kwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zimetangazwa hapa tahasusi 65, zimeongezeka mpya 49. Nikajaribu kuangalia hapa tunalenga nini? Kwa mfano, tahasusi ambazo zinahusika na mambo ya kijamii zipo tisa, zinazohusiana na lugha zipo 11, zinazohusiana na biashara zipo saba, sayansi zipo saba peke yake na dunia ya sasa inatawaliwa na sayansi, lakini michezo zipo saba, sanaa zipo 16 na dini zipo nane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ukimwuliza Profesa kwamba katika tahasusi hizi kwanza mlikuwa mnataka kulenga kitu gani? Pili, mna vitabu vya kutosha kwa haya masomo mapya ambayo mmeleta? Vimechapishwa tayari? Mna walimu wenye ubora wa kufundisha masomo haya ambayo yanaanzishwa sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo haya ili kuondoa wasiwasi wa Watanzania hasa vijana ambao wanaenda kusoma, ni vizuri tuwe na majibu sahihi na hili halihitaji siasa katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwamba kwa baadhi ya wilaya Serikali imepeleka fedha kuanza kujenga VETA, nami nimepata VETA kule Nyamongo – Nyabichune inaendelea vizuri. Sasa naomba, katika VETA hizi pia, unapotaka kutengeneza ajira kwa Watanzania walio wengi, lazima u-target. Wamesema Waheshimiwa Wabunge wengi kwamba, kama umepeleka kule Nyamongo VETA, kule kuna wachimbaji wadogo. Katika masomo mtakayofundisha pale, course hizo lazima uweze ku-consider uchimbaji mdogo kwa watu ambao wanazunguka eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pale kuna wafugaji na kuna wavuvi; pia kuna Mto Mara pale. Kwa hiyo, tunatarajia walimu ambao wataenda pale na vitendea kazi viendane na mazingira ambayo VETA ipo katika eneo hilo. Ukijenga VETA katika maeneo ambayo watu wake ni wafugaji, maana yake utakuta wote wanapata taaluma na watapata ajira. Kwa hiyo, malalamiko mengi yatakuwa yamepungua katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna hii elimu ya amali ambayo inaanza kwa primary, kwa maana ya kote, lakini na baadhi kwa sekondari. Pia kumekuwa na maswali katika eneo hili. Hivi Mheshimiwa Profesa anaweza kutuambia leo kwamba ameshakarabati karakana ngapi zilizokuwa za zamani kwa teknolojia ya kisasa ya dunia? Amejenga karakana zipi mpya za kisasa katika maeneo yetu? Pia ni maeneo ambayo anatakiwa utueleze. Kwa mfano, kuna course ya ushonaji, hivi una mashine mpya za kisasa za ushonaji? Kama ni useremala, hivi vitu vipo? Haya maswali pia na mengine yatafakariwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama ni sayansi ipo ya eneo fulani, kwa mfano kwenye hizi VETA na vyuo mbalimbali vya kijamii, kuna maabara za kisasa zimejengwa katika eneo hilo? Kuna maji ya kutumia kwenye chemicals? Kuna umeme wa kutosha? Kuna standby generator in case umeme umekatika? Umeandaa walimu wa kutosha? Je, waliopo sasa ni wa zamani? Wamefundishwa hii taaluma ya sasa ili wakaboreshe ufundishaji kwa vijana wetu? Hayo pia ni maeneo ambayo ni muhimu sana yakazingatiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo nataka nichangie, kwenye taarifa ya Kamati yenyewe wameonesha wasiwasi. Kwa hiyo, nafikiri Mheshimiwa Waziri anapokuja kuhitimisha hoja yake ni vizuri atueleze, Kamati wanasema wana wasiwasi na miundombinu pungufu iliyopo kwa ujumla wake, wametaja hapa kwenye ukurasa wa 14. Wanazungumza kwamba vitabu havitoshi vya mitaala mipya na huenda baadhi ya maeneo ni vichache sana. Pia wamesema hata fedha za mikopo ambazo ziliwezesha, na hii lazima litolewe maelezo.

Mheshimiwa Spika, ukiwaambia hawa watoto waliopo shuleni na wazazi, Mheshimiwa Rais ameshatamka kwamba ameongeza fedha ya mikopo halafu wanasema humu zimepungua. Lazima uonyeshe umepunguza eneo lipi katika mazingira hayo ili pia isilete taharuki.

Mheshimiwa Spika, katika tathmini, mmekuwa mkitoa mikopo 20%, 40%, 60% mpaka 100%. Hivi tathmini imefanyika? Wale watoto ambao walipata 20%, 40% halafu wazazi na wadau wakashindwa kuwasomesha wakaacha vyuo, hivi wako wapi? Hii fedha ina maslahi gani kwa Watanzania? Kuna mtu umempa 40%, mzazi au mlezi hawezi kumsomesha, ameenda ameripoti chuoni na wengine kimsingi wamechanganyikiwa mtaani. Je, umefuatilia katika maeneo hayo? Kwa hiyo, haya mambo ni muhimu sana kwenda kuangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nilikuwa Rais wa Chuo pale Mlimani mwaka 2005/2006. Katika migomo ambayo niliwahi kuendesha pale, watu ambao niliwaongoza humu ndani wapo ninawaona, wapigakura wangu wa zamani wa Mlimani wapo hapa. Tuligoma pale Mlimani Chuo kikafungwa mara mbili, mara tatu kwa sababu ya boom. Kwa hiyo, boom hii ilikuwa shilingi 2,500/= ikaongezwa shilingi 2,500 ikawa 5,000. Nilipambana nikakuta, sikuitumia ile shilingi 5,000, ikaja mwaka 2009/2010 ikaenda shilingi 7,500, shilingi 8,500, leo ni shilingi 10,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maisha ya kawaida tungetarajia Mheshimiwa Rais ikimpendeza na kama hali itaruhusu, hawa vijana wapewe hata shilingi 20,000, itawasaidia sana kuboresha maisha yao kwa sababu mahitaji ni makubwa sana. Sasa kama kuna lugha nyingine zimetumika, na nimeona vijana wamepokea very negative, mimi nasema hao vijana kuwapa boom, mimi mwenyewe limenisaidia sana wakati ninasoma. Unaweza ukawa umekwama ukanunua vitabu. Umezungumza hapa maktaba vitabu havitoshi, kwa hiyo, tulikuwa tunachangisha kwenye chumba ili mtu anunue kitabu na vitendea kazi vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kuna matumizi mengi sana ambayo fedha hii inaweza kuwasaidia vijana wakawa comfortable. Tunachotaka ni kwamba Mheshimiwa Rais apeleke mikopo, watoto wapewe boom wasome. Jambo la muhimu ni kwamba waweze kufanikiwa vizuri wakaboreshe jamii zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilitaka nimwulize Mheshimiwa Waziri swali, hivi kwa elimu ya Tanzania tangu tumepata uhuru mpaka leo, ni sahihi Wabunge humu ndani kuwa na kigezo cha kujua tu kusoma na kuandika na ikatamkwa kwenye vitabu! Ni sahihi? Yaani mpaka leo kwa nchi hii ni wasomi wengi na wataalamu, lakini kwenye vitabu inasoma kwamba sifa ya Mbunge ni kujua kusoma na kuandika. Kama kuna hoja ya mtu kujua kusoma na kuandika, lakini anajua nini cha ziada? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kishimba hapa mpaka amepewa jina la Profesa, siyo msomi, lakini ukimsikiliza mambo yale ni makubwa kweli kweli kuliko hata ya ma-doctor wengi nchi hii. Sasa nadhani hii pia ni muhimu, maana yake ukiongea Mbunge wanafikiri wote humu darasa la saba au la saba siyo chochote. Hapana, kafanyeni tathmini, kuna mtu aliishia darasa la saba, ana nini? Kuna ile wanaita extra curriculum. Ni kitu gani cha ziada anakijua? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huyu mtu ni mtaalamu kuliko hata maprofesa wengi, lakini kwa sababu tu anatakiwa vyeti, anakuwa labelled kwamba kujua kusoma na kuandika. Kwa hiyo, nadhani Wizara ya Elimu mambo haya ya msingi mtusaidie kubadilisha ile mentality ya Watanzania ili Wabunge pia wapate heshima kwamba unaweza ukawa darasa la saba lakini unajua vitu vingi.

Mheshimiwa Spika, wengine hapa wanamiliki mitaji mikubwa, wanafanya biashara, wametembea nchi mbalimbali, wana mambo makubwa ambayo wanafanya na huku wanaweza wakachangia michango mikubwa sana kuliko hata wasomi, ili tuone kwamba kumbe kusoma siyo kuwa na vyeti tu. Unaweza ukawa na elimu nzuri na bado hauna vyeti na ukafanikiwa katika maisha na ukaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaangalia hata duniani, viongozi wengi wa nchi kubwa ambazo zimeendelea wala siyo wasomi sana. Wasomi wamebaki ofisini kufikiria, kutunga vitabu na kuandika, wale watu ambao wanaweza kusimamia, wanafanya kazi hiyo vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ningetamani kwamba Wizara hii kwa maswali mengi ambayo Waheshimiwa Wabunge wametoa na kuuliza na wamezungumza, kwa mfano tulikuwa na upungufu wa walimu hasa wa sayansi katika shule zetu. Unapoongeza wigo wa tahasusi na elimu ya amali, hivi Watanzania wajipange katika lipi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, naomba niunge mkono hoja. Nakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Waitara, kuna hoja yako umeianza lakini hujaihitimisha. Umesema kwamba kuna haja ya kuandika kigezo cha Ubunge kama ni kusoma na kuandika. Wewe unamshauri nini Mheshimiwa Waziri?

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, namshauri Mheshimiwa Waziri kwamba ikibaki tu kwamba Waheshimiwa Wabunge humu uwezo wetu uwe ni kujua kusoma na kuandika tutakuwa undermined. Maana yake kama kuna mtu amesoma elimu fulani itamkwe, hata kama ni darasa la saba, anajua kusoma na kuandika lakini anajua vitu vya ziada. Hivyo, iwepo kwenye CV yake, na waelezwe kwamba hiyo ni ya ziada tu, lakini unaweza ukauliza vitu vingine vya msingi sana, ndiyo hoja yangu hapo.

Mheshimiwa Spika, ukienda hata Kenya hapo wameweka masharti kwenye Bunge...