Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Eric James Shigongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kuwa hai na kuwa ndani ya Bunge hili. Nakushukuru sana wewe kwa kunipa nafasi ya kuzungumza. Vilevile namshukuru sana Mheshimiwa Prof. Mkenda na timu yote ya Wizara ya Elimu kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tangu mwanzo nimesema sijawahi hata siku moja kuwa na mashaka na Mheshimiwa Prof. Mkenda, tofauti yetu ilikuwa ni kwenye suala moja tu la RPL (Recognition of Prior Learning). Bado naendelea kuomba kwamba suala la Recognition of Prior Learning liweze kufanyiwa kazi ili Watanzania wenye ujuzi ambao hata kama hawana sifa kubwa sana waweze kupatiwa nafasi ya kuendelea na masomo ya chuo kikuu.
Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya. Amefanya kazi kubwa sana, madarasa mengi yamejengwa, vituo vya afya vingi na kazi kubwa inaendelea kufanyika katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jana nilipata nafasi ya kuzungumza na Mheshimiwa Prof. Mkumbo kwa muda, nikamwambia umepata bahati kubwa sana ya kuandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa, ya kwamba unachokifanya hakitakuwepo mpaka mwaka 2050. Jambo moja kubwa nililomwomba jana, anitengenezee watoto wenye akili, watoto wenye uwezo mkubwa, watoto wenye uwezo wa kushindana katika dunia inayokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya uhuru wa nchi yetu, wazee wetu walituandaa sisi na tumefika hapa tulipo leo, tunafanya tunayoyafanya, lakini ni ukweli ulio wazi kwamba sisi na watoto wetu tunashindwa kushindana kwenye ulimwengu wa sasa kwa sababu hatukuandaliwa vizuri.

Mheshimiwa Spika, sasa tunajadili Wizara ya Elimu, swali ninalojiuliza, tunamtengeneza mtoto wa aina gani? Tunamtengeneza mtoto wa aina gani mwaka 2050 ambapo tutakuwa na ulimwengu wa kidijiti zaidi, internet of things, cloud computing na mambo mengine mengi yatakuwa yanafanyika kwa kutumia artificial intelligence? Je, tunamwandaa mtoto wetu aweze kushindana vizuri kwenye ulimwengu huo wa mwaka 2050?

Mheshimiwa Spika, kwangu elimu ni kama fyatulio la tofali. Kule kijijini tuna mafyatuo ya tofali tunafyatua tofali, kwa hiyo, haiwezekani kupata tofali la duara kwenye fyatulio la mstatili. Je, mtaala huu tunaouandaa au mtaala tunaoutumia unatutengenezea watoto wa namna gani kesho? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini sana kwenye educated labour force, naamini sana na mpaka hivi sasa ninavyoongea naamini sana kwenye elimu kwamba ndicho kitu pekee kitakachomsaidia Mtanzania kutoka kwenye umaskini na kupeleka Taifa lake mbele. Mtu yeyote asitudanganye tukapuuza elimu. Hata kama mimi sikubahatika kuipata huko utotoni, lakini bado elimu inabaki kitu cha kwanza na cha msingi kwa maendele ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mnatumia fedha nyingi sana kusomesha watoto ili mtengeneze watoto ambao watakuwa faida kwa Taifa, familia na ulimwengu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Prof. Mkenda nataka utimize jukumu na wataalamu wote ulionao kututengenezea watoto wenye akili watakaoshindana kwenye ulimwengu ujao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina mambo matano tu ya kusema. Huo ndiyo utakaokuwa ushauri na mchango wangu kwa siku ya leo kwa Mheshimiwa Prof. Mkenda na Taifa zima. Tufanye nini ili tuweze kuboresha elimu ya Taifa letu? Mambo haya nimeyaandaa katika mfumo wa herufi tano ili iwe rahisi kwangu mimi kukumbuka na wanaonisikiliza kukumbuka. Herufi hizi tano zinamaanisha neno “Change”, C, H, A, N, G, E.

Mheshimiwa Spika, C – curriculum (Mtaala). Nampongeza sana Mheshimiwa Prof. Mkenda, amefanya jambo jema sana kushughulika na kubadilisha mtaala wetu. Mara ya mwisho nilipozungumza hapa niligombana kuhusu mtaala, nikasema mtaala huu unatuchelewesha kwenda mbele. Hivyo amechukua hatua na amebadilisha mtaala. Nimeusoma, nimeuona umezingatia mambo yote ya msingi. Anawaandaa watoto wetu kuweza kutimiza majukumu yao. Mtaala huu ninauunga mkono ukatekelezeke ili uweze kuboresha elimu ya watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natamani mtaala ambao utabadilisha mindset za watoto, natamani mtaala utakaowafundisha watoto wetu values za nchi yao, natamani mtaala ambao utafanya watoto wetu wawe practical zaidi badala ya theories. Huko nyuma tulikuwa ni watu wa nadharia nyingi sana kuliko vitendo, lakini mtaala huu unatengeneza watoto ambao watakuwa suluhisho la matatizo ya Taifa letu. Nakupongeza Mheshimiwa Prof. Mkenda na timu nzima ya wataalam walioandaa. Hiyo ni C. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, H - happy motivated teachers. Tunahitaji walimu waliokuwa motivated, walimu ambao hawana hofu ya kesho. Hata kama una mtaala bora kiasi gani, bila walimu bora hakuna utakachofanikiwa. Walimu wetu mazingira yao ni magumu, kwa hiyo, natamani walimu walipwe vizuri, natamani walimu waishi mahali pazuri ili watamani kufundisha watoto wetu. Mwalimu ambaye anaendesha bodaboda hawezi kufundisha mtoto wangu. Maisha yao ni duni, hivyo tuboreshe maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, A – availability ya educational infrastructure. Naipongeza sana Serikali yangu kwa madarasa mengi yaliyojengwa, lakini madarasa bila walimu haitasaidia chochote. Kwa hiyo, naomba tuendelee kuboresha miundombinu ya elimu katika nchi yetu ili mwisho wa siku watoto wetu wasikae chini, wasome kwenye madarasa mazuri na hivyo waweze kuwaelewa walimu wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, N – navigating from using Kiswahili kama medium of instruction. Siku zote nimesema, mimi sikubaliani sana na kufundisha kwa Kiswahili na ninarudia leo tena hapa ndani, nikizungumza huwa nabishiwa, naomba tuwafundishe watoto wetu kwa lugha ambayo imeficha maarifa ya dunia. Maarifa mengi yamefichwa kwenye Kiingereza, tuwafundisheni watoto wetu kwa English. Wazazi wengi hapa tunawafundisha watoto wetu international schools. Naomba sana tulifikirie suala hili, tuwafundishe kwa Kiingereza, wazungumze Kiswahili nyumbani na popote walipokuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nipe nafasi nimalizie. Nimemaliza ‘N’ na sasa nakuja G – go do research. Naomba tuwekeze sana fedha nyingi kwenye ufanyaji utafiti. Nchi hii haifanyi utafiti wa kutosha, kwa hiyo, tuweke fedha nyingi kwenye utafiti. World Bank imesema bajeti ya utafiti inatakiwa 2.7 percent ya GDP, lakini kwetu sisi ni 0.5 percent ya GDP. Ni fedha kidogo mno kufanyia utafiti. Kwa hiyo, tuwekeze kwenye utafiti wa elimu ili tujue matatizo yetu na jinsi ya kuyatatua na ili tuweze kuiona kesho itakuwaje kwa watafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utafiti usifanyike tu kwa ajili ya kutimiza masharti ya kupata degree shuleni, hapana. Utafiti ufanyike kila siku, fedha zitumike kwenye utafiti ili kuwawezesha wataalamu wetu kugundua matatizo yetu na jinsi ya kuyatatua.

Mheshimiwa Spika, la mwisho ni E - engage parents. Tusiwaache wazazi pembeni. Wazazi watimize wajibu wao. Wazazi tusiwaachie walimu watoto wetu, wazazi wa nchi hii tumekuwa wavivu, hatusimamii watoto. Mzazi zima TV nyumbani mpe mtoto kitabu asome. Mtoto akilia kidogo anapewa simu acheze game ili asipige kelele. Nawaomba wazazi washiriki kutimiza wajibu wao kushirikiana na Serikali ili tuweze kutengeneza watoto bora. Kama wazazi tukikaa pembeni hata siku moja hatutafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, nikielekea mwisho ni bajeti, UNESCO. Wamesema bajeti ya elimu katika nchi yoyote haitakiwi kupungua twenty percent ya bajeti nzima. Bajeti hii ambayo Mheshimiwa Prof. Mkenda anataka kupitisha ni shilingi trilioni 1.9 ambayo ikizidi sana, haiwezi kuzidi three percent ya bajeti yetu ya mwaka mzima ya forty-nine trillion. Hiyo haitoshi.

Mheshimiwa Spika, tuwekeze kwenye elimu. Tukubali ku-invest kwenye education kwa sababu bila kuwekeza kwenye elimu hatuwezi kupata mafanikio. Naomba kuunga mkono hoja, ahsante kwa kunisikiliza. (Makofi)