Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Amb. Liberata Rutageruka Mulamula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. BALOZI LIBERATA R. MULAMULA: Mheshimiwa Spika, ukiongea karibu na mwishoni unakuta mengi yamesemwa, lakini naomba niruhusu niseme yale ambayo hayakusemwa. Naomba nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Prof. Adolf Mkenda, kwa hotuba nzuri na iliyosheheni matokeo chanya ya utekelezaji wa sera na mikakati ya kuboresha elimu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nampongeza Naibu Waziri, Mheshimiwa Omari Kipanga ambaye wakiwa wamekaa pamoja na Mheshimiwa Profesa Adolf Mkenda, wanaonekana kama Mapadri ambao wanatoa amani ya roho, I mean amani ya moyo. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, aidha, ninaipongeza Wizara na Serikali kwa mambo mawili makubwa ya kimapinduzi yaliyofanywa kwenye Sekta ya Elimu katika kipindi hiki cha Awamu ya Sita, chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwanza, ninapongeza jinsi Wizara na Taasisi zake zilivyosimamia na kuongoza mchakato mgumu wa kubadili mitaala ya elimu. Huu ni mchakato mgumu wenye siasa kali katika nchi yoyote. Nampongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kushirikisha makundi mengi iwezekanavyo na maoni mengi na kupata maoni mengi iwezekanavyo. Kwa kweli niseme hakuna anayeweza kusema hakupata nafasi ya kusema, ya kushauri au hata wale wa kubeza. Kwa hiyo, tunaweza kusema sasa tuna mtaala mzuri kuliko tulionao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kulichukulia kwa umuhimu mkubwa suala la tafiti na machapisho katika Chuo vyetu Vikuu. Utafiti na machapisho ndiyo uhai na sifa ya Chuo Kikuu chochote. Nampongeza kwa kutenga fedha za kuwafadhili wanataaluma wetu waweze kufanya tafiti na kutoa machapisho. Hii naona imeanza kuchochea utamaduni wa kutafiti na kuchapisha. Of course, ninajua fedha haitoshi, lakini nilisemea sana hili kuhusu kuwekeza katika research and development. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo, napenda kuchangia masuala mawili; moja, limeongelewa nami nimesifia kuhusu kuwa na mitaala mipya katika matokeo ya watoto wetu (education outcomes). Maana mitaala ni mizuri kama wengi walionitangulia walivyosema. Mitaala ikiwa peke yake haiwezi kuleta matokeo chanya au mapinduzi tunayotarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, napenda kuongelea kuhusu kuhuisha Vyuo vyetu Vikuu na kuvifanya viwe shindani Kimataifa. Naomba nianze na la kwanza; kwa sisi tuliozaliwa vijijini, shule na jengo la shule zuri ndiyo ilikuwa alama ya mafanikio, ustaarabu na utaifa. Pengine shule ilikuwa na majengo mazuri kuliko hata nyumba zetu. Kwa hiyo, ukienda shule ndiyo unayajua mengi, unayajua ya nchi nzima na kuanzia Middle School na Sekondari, kwa sisi wa zamani ilikuwa inatukutanisha na makabila mbalimbali na wanafunzi kutoka mikoa mbalimbali. Kwa hiyo, shule iliakisi Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii katika hizi zama za teknolojia, habari na mawasiliano vimeifanya shule kuwa ni dunia ndani ya shule. As they say, world in a classroom, you bring the world in a classroom through the use of technology. Kwa hiyo, hii mitaala mipya inayochochea kujifunza, ubunifu na kujiajiri, itafanikiwa tu endapo tutafungamanisha (integrate) mabadiliko haya ya mitaala na uwekezaji mkubwa ambao Serikali imeufanya kwa kusambaza umeme vijijini, kusambaza mkongo wa Taifa na kusambaza minara ya mawasiliano. Kwa hiyo, mifumo hii lazima isomane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miundombinu hii na uwekezaji huu utatusaidia sasa kuwezesha mtoto aliyepo Kagera afundishwe na mwalimu aliyepo Katavi au aliyepo Marekani kwa njia ya mtandao wa E-education. Kwa hiyo, tunavyowekeza lazima tuangalie hii inachangia vipi katika elimu? Maana yake inakuwa kama wakati mwingine tunafanya mambo kwenye in silos.

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo, kama tunavyoona katika sekta ya afya, matumizi ya mobile clinics (E-health) au wanaita M-health; Daktari yupo India, lakini anafanya opereshini hapa Dar es Salaam. Kwa hiyo, hii itawafanya watoto wetu waanze kushuhudia dunia ndani ya darasa na huko ndiyo kujenga kizazi cha utandawazi na mapinduzi ya nne ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nimesema nitaongelea kuhusu jinsi ya Vyuo Vikuu vyetu vinavyopimwa kuangalia pamoja na mambo mengine kiasi gani Chuo kinaileta pamoja dunia (Internationalization). Jana tulimsikia Mheshimiwa Jesca Msambatavangu akijaribu kupata tasfiri halisi ya Internationalization, lakini muhimu ni kwamba, vyuo vyetu lazima virudishe ule utaratibu ambao ulikuwa unaruhusu hii wanaita multicultural exchanges ya faculties, siyo wanafunzi tu, lakini ya faculties. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nimepata bahati ya kualikwa kwenye Chuo cha George Washington University kama scholar, lakini practitioner in residence, na hii ilikuwa ni kutumia kuwapa uzoefu/ujuzi ulionao, na walifaidika sana. Maana yake ilikuwa niende miezi mitatu, nikakaa miaka minne kwa kuwa kulikuwa na demand kubwa. Kwa hiyo, mimi nataka tuwe hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, niseme kuhusu umuhimu wa kutumia wana-Diaspora. Tumekuwa tukiangalia Wanadaispora katika remittances, lakini tuangalie namna ya kuwatumia wana-Diaspora katika sekta ya elimu.

Mheshimiwa Spika, nashukuru nilimwona Mheshimiwa Waziri huko Mwanga akizindua maktaba ya mwanafunzi wa kidato cha pili ambaye yupo Rwanda, lakini ameanzisha maktaba ya jamii. Huyo ni mwana-Diaspora na ndiyo tunataka ushiriki wa Diaspora wa namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hiyo ninaomba watumie pia Balozi zetu kwa kuanzisha vitengo vya International Cooperation (Mahusiano ya Kimataifa). Najua ndani ya Chuo Kikuu kitengo hicho kipo, lakini kipo kwa jina, hawatuchokozi mpaka mabalozi. Mimi nilivyokuwa ninawasiliana nao, nauliza vipi wangetaka ushirikiano upi?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba watumie sana hiyo programu ya ushirikiano wa Kimatifa kuweza kuleta hizo exchange programs, lakini kwa walimu wanajua capstone courses, wanafunzi wanakuwa na kiu huko nje kuja kufanyia hizo capstone courses hapa. Kwa hiyo, tuwawekee mazingira wezeshi, siyo vikwazo kupata vibali vya kazi, vya makazi na wakati wa summer wengi hupenda kuja kwenye nchi hii na kukaa kwenye vyuo na wengine ambao wapo Sabbatical Leave. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba tuwawezeshe ili vyuo vyetu viwe Internationalized, maana yake mtu ambaye hatoki, kama tunavyosema kwetu, mtoto ambaye hatoki anasema mama yake tu ndio anajua kupika, mpaka anapotoka. Pia tukitumia mbinu hii tutavipa vyuo vyetu...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. BALOZI LIBERATA R. MULAMULA: Mheshimiwa Spika, naomba dakika moja…

SPIKA: Sekunde 30.

MHE. BALOZI LIBERATA R. MULAMULA: Sawa.

Mheshimiwa Spika, tukitumia mbinu hii, tutavipa vyuo vyetu uhai mpya na kuvijengea ushindani katika Bara la Afrika na ushindani wa Kimataifa.

Mheshimiwa Spika, mwisho katika hizo sekunde 30, ni kuhusu ushiriki wa sekta binafsi kwenye kuboresha na kukuza viwango vyetu vya elimu, siyo kuanzisha shule na kuendesha shule, lakini kuanzisha. Mheshimiwa Waziri naomba unisikilize, suala la endowment fund, kwa kweli na hiyo anayosema tafiti na machapisho na kuweza kuwa na elimu bora bila endowment fund itakuwa ngumu na ushiriki wa sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)