Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BALOZI DKT. BASHIRU A. KAKURWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Nitakuwa na maneno machache ya utangulizi mafupi tu. La kwanza, mjadala wa tangu jana tunaouhitimisha sasa, umekuwa wa kusisimua. Nimepata wakati mgumu sana kujiandaa kuchangia. Mheshimiwa Prof. Mkenda, aliponikuta hapa akawa anasema, wewe unaandika thesis ya Ph.D! Maana yake tangu asubuhi aliona ninajiandaa ninaandika. Nilikuwa ninaandika ninafuta kadri wachangiaji wanavyoendelea kuchangia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii ni kiashiria cha nini? Ni kiashiria cha kwamba Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imethubutu kufanya mabadiliko ambayo sasa katika mjadala wetu baadhi yetu tumepata hofu, baadhi yetu tuna matarajio makubwa, baadhi yetu tuna wasiwasi na baadhi yetu tuna matumaini makubwa kwamba nchi yetu sasa inaelekea pazuri. Hiyo ndio hoja yangu ya kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ya pili, nitumie muda mfupi kuwakumbuka na kuwaenzi viongozi wetu wawili, Hayati Mwalimu, Julius Kambarage Nyerere na Hayati Ali Hassan Mwinyi, kwa kuweka msingi mzuri sana na imara wa elimu hii tunayotaka kuiboresha. Sitaki kurejea mchango wa Mheshimiwa Prof. Kabudi na Mheshimiwa Prof. Muhongo, mimi ni Mwanataaluma na taaluma ni kama jeshi; Profesa ni kama General, kwa hiyo, unatii tu, lakini unatakiwa kudadisi pia na kukosoa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, imewekea hoja mezani hapa kwamba, tumetoka mbali na tumepata mafanikio makubwa, lakini hapa tulipo haparidhishi, lakini siyo pabaya na kwamba, tunapoelekea ni parefu zaidi, pengine ni pagumu zaidi. Kwa hiyo, Serikali isichoke kusikiliza maoni na michango ya Watanzania wakiwemo Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Baba wa Taifa alitangaza vita na akasema maadui tunaopambana nao ni watatu; ujinga, maradhi na umaskini, na akaongeza kwamba, nchi yetu bado watu wake ni maskini na ili kuwakomboa watu hao maskini ni muhimu kuwapa watoto wao elimu kama nyenzo ya ukombozi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Hayati Ali Hassan Mwinyi, Mungu amrehemu akasema maneno haya haya, lakini kwa namna tofauti, ninamnukuu, alisema hivi: “Umaskini na uchafuzi wa mazingira ni watoto mapacha na mama yao ni ujinga.” Kwa hiyo, sasa hivi tunajadili namna ya kutokomeza ujinga unaozaa umaskini na pia unaosababisha matatizo mengi sana kama maradhi na uchafuzi wa mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimejaribu kutumia maneno haya ya utangulizi kwa kirefu kidogo, kwa sababu wachangiaji wa tangu jana na leo kwa kweli ni kama wamenifilisi. Hata hivyo, naomba nichangie maeneo mawili. Jana ulituongoza hapa kwamba, kwa sababu hii ni Wizara ya Elimu na tunatumia Kiswahili, basi tutumie Kiswahili fasaha. Nitakuomba uniuwie radhi nikichemka, lakini nitajitahidi.
Mheshimiwa Spika, jirani yangu hayupo hapa, lakini jana alizua mjadala mzuri sana kuhusu Internationalization na akaitafsiri kwamba ni umataifishaji wa elimu yetu. Mheshimiwa Prof. Kabudi, akaongeza akasema, umataifashaji wa elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nilikuwa Mkurugenzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tulikuwa tunatumia umataifishaji na katika lugha neno likitumika mara nyingi hata kama lina ukakasi linakubalika. Tumetumia neno makinikia, limepita tu, kwa sababu ya namna lilivyotumika kuchakachua na mambo mengine kama hayo. Sasa hoja ni hii, tunataka vyuo vyetu vikuu viwe na hadhi ya kimataifa, vitambuliwe kimataifa Mtaala mpya ni moja ya nyenzo ya kuelekea huko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninashauri kwamba ili tuelekee huko itabidi Bunge hili liishauri Serikali ilete marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma, hasa maeneo ya usimamizi wa rasilimali katika taasisi nyeti na za kimkakati kama Vyuo Vikuu vya Umma. Sheria hiyo ikibadilishwa itavipa uwezo na mamlaka chini ya uongozi wa Serikali kuajiri, kufanya tathmini ya utendaji wa Watumishi wake na hasa Wahadhiri kupandisha vyeo, kusimamia nidhamu pamoja na kupima utendaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hali ilivyo sasa hivi, kwa sheria tuliyonayo na utaratibu tulionao, vyuo vyetu ni kama Idara za Serikali. Siyo taasisi nyeti na za kimkakati zenye mazingira maalum na mahitaji maalum na nitatoa mfano. Nilipotoka Chuo Kikuu mwaka 2018, nilimwacha mwenzangu amepandishwa cheo kutoka Mhadhiri kuwa Mhadhiri Mwandamizi, nilitoka akiwa amepewa barua na chuo kilichomtambua, kwa sababu unapanda cheo kama Mhadhiri kwa kigezo cha machapisho pamoja na uzoefu wa miaka mitatu. Alikidhi hicho kigezo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Chuo Kikuu kikampa barua ya kutambua cheo chake, kikapeleka Utumishi kwa ajili ya kibali. Kibali chake kilitoka mwaka 2021 baada ya miaka mitatu. Baada ya miaka mitatu! Huku kakaa miaka mitatu kupata cheo hicho kwa vigezo na mwongozo wa chuo, lakini kibali cha kutambua cheo hicho kikatoka baada ya miaka mitatu. Kwa hiyo, akapata mshahara wa cheo alichokipata baada ya miaka mitatu na akakaa miaka mitatu analipwa mshahara wa cheo cha zamani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati utumishi wanatoa kibali mwaka 2021, alikuwa pia ametimiza vigezo kupanda nafasi ya kuwa Profesa Mshiriki. Kwa hiyo, kibali kinakuja wakati yeye amepanda vyeo hivi viwili, na ndipo alipoanza kupata mshahara huo. Tangu 2021, mpaka leo ninapozungumza, kibali cha kutambua Uprofesa wake Mshiriki, hakijatoka. Hii maana yake nini? Tunataka vyuo vyetu viwe vya kimataifa kweli? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, takwimu hapo zinatueleza kwamba tuna uhaba wa Maprofesa na Maprofesa Washiriki. Ukienda kwenye mfumo wa utumishi, huyu Profesa Mshiriki anatambuliwa kama Mhadhiri Mwandamizi. Kwa hiyo, data ya Mheshimiwa Prof. Ndakidemi sijui ulikuwa unasoma ya utumishi au ya vyuoni? Alikuwa anasoma ya vyuoni, hili ni tatizo kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza inavunja moyo kwa sababu, kuchapisha ni kazi ngumu sana, ni ghali, na wakati mwingine gharama hizo zinatoka mfukoni mwa anayechapisha kwa sababu ya uhaba wa rasilimali, lakini sherehe kubwa katika vyuo vikuu ni mtu anapopanda nafasi baada ya kuchapisha. Kimataifa tunatambuliwa kwa kuwa na machapisho yenye hadhi. Hii inatakiwa ibadilishwe, kama kweli shinikizo lililopo la kuvifanya vyuo vyetu viwe vya kimataifa litashughulikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, yapo matatizo ndani ya vyuo, lakini hata wakiyarekebisha, vipo vikwazo ndani ya utumishi. Mimi nina taarifa (nina wasiwasi na muda) kwamba, Msajili wa Hazina ameshatoa Waraka Namba Moja tangu mwaka jana 2023 Mwezi wa Nane, akijaribu kuainisha alichokiita mashirika na taasisi nyeti zinazohitaji uhuru wa kuendesha na kujiendesha na hasa uhuru wa kusimamia rasilimali watu. Huu waraka hautekelezeki mpaka Sheria ya Utumishi wa Umma ibadilishwe. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. BALOZI DKT. BASHIRU A. KAKURWA: Mheshimiwa Spika, nakuomba sekunde chache.
Mheshimiwa Spika, suala la mwisho nataka kukizungumzia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Chuo hiki kwa kweli naweza kukiita ni fahari ya Tanzania. Pamoja na matatizo mengi, Mheshimiwa Spika huruhusiwi kupiga makofi, lakini naona tabasamu linaashiria hivyo. Hapo ninajaribu kukuhonga uniongezee muda kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ndiyo kimezaa Chuo Kikuu cha Sokoine, kimezaa Chuo Kikuu cha Ardhi, kimezaa Chuo Kikuu cha Muhimbili, kinavilea Vyuo Vikuu Vishiriki vya DUCE na MUCE, lakini ndiyo roho ya vyuo vikuu vyote vya binafsi. Chuo hiki pia kimesaidia kuanzishwa kwa Chuo Kikuu kikubwa sana hapa nchini, cha Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hiki chuo kwa sasa ninavyoongea kina Shahada za Uzamivu (Ph.D) 1,000 na ukishafikia idadi hii kimataifa wewe unapewa hadhi ya Chuo cha Kitafiti (Research University). Pia, kwa mwaka chuo hiki kinazalisha Shahada za Uzamivu 100 kwa wastani. Sasa sitaki kuzungumza juu ya mazao ya chuo hiki kwa sababu, nitaonekana pengine ninatia chumvi, lakini aliyekalia kiti anatambuliwa kimataifa na ni zao la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. (Makofi)
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, sasa alikuwa ameomba dakika moja.
MHE. BALOZI. DKT. BASHIRU A. KAKURWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, ukimtaja Mheshimiwa Prof. Muhongo hapa tunamtambua kama Mbunge, lakini ni mtafiti, ni Profesa mwenye heshima kimataifa. Mheshimiwa Rais Yoweri Museveni wa Uganda ni zao la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hayati, John Garang wa Sudani ni zao la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Hayati Rais Magufuli ni zao la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Hayati Maalim Seif ni zao la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na ni mmoja wa wanafunzi kutoka Idara niliyokuwa mimi ya siasa aliyefanya vizuri na rekodi yake iko hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nadhani nitakuwa nakuvunjia heshima ulivyonivumilia. Nakushukuru na ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)