Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Anastazia James Wambura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kutoa mchango wangu. Kwanza namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa zawadi yake ya uhai, lakini vile vile kwa kutujalia sote afya njema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vile vile Mhehimiwa Dkt. Philip Isdori Mpango, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu wake, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Dotto Biteko, pamoja na Mawaziri na Naibu Mawaziri wote kwa kazi nzuri ya kuliletea Taifa letu maendeleo katika nyanja mbalimbali. Nadhani sote ni mashahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee pia nampongeza sana Mheshimiwa Prof. Adolf Mkenda ambaye ni Waziri wa Elimu, Naibu wake maarufu QS Mheshimiwa Omari Kipanga ambaye ni Naibu Waziri. Vilevile Katibu Mkuu Prof. Caroline Nombo, Manaibu Makatibu Wakuu; Dkt. Jasson na Prof. Mdoe, pamoja na timu nzima ya Wizara kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya hasa kwa upande wa kuboresha miundombinu ya elimu na kwa maboresho ya sera ambayo wasemaji wengi wanaizungumzia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sitakuwa na mengi sana ya kuzungumza kwa sababu, tumeyazungumza katika Kamati. Mimi ni mjumbe mmojawapo wa Kamati hii ya Elimu na tunaiamini Serikali kwa sababu Mheshimiwa Waziri ametueleza mipango mingi ya Wizara. Pia tuna imani kwa sababu ya kazi nzuri ambayo tayari imeshafanyika. Kwa hiyo, tunajua kazi inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili nitakalolizungumza ni kwa sababu ni suala ambalo ni mtambuka na Serikali nzima ipo hapa. Kwa hiyo, napenda nilizungumze na baadaye kama muda utaruhusu nitaongea masuala ambayo ni specific kwenye elimu.

Mheshimiwa Spika, naanza kwa tafsiri ya elimu. Elimu inatafsiriwa kama njia ya kutengeneza nguvukazi yenye ujuzi ambayo inasababisha ukuaji wa uchumi na uvumbuzi. Kwa maana hiyo, madhumuni ya elimu katika jamii ni kupata ufahamu na ujuzi ambao utawaandaa watu kuendesha maisha yenye tija na utoshelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wenzetu walitutengeneza. Miaka iliyopita walitutengeneza Watanzania au Waafrika tuwe ni watu wa kuzalisha malighafi na kuziuza kwa bei ya chini ambayo wenzetu hao wanaipanga wao wenyewe, lakini pia sisi tununue bidhaa ambazo zinatokana na hiyo malighafi kwa bei ya juu ambayo pia, wanaipanga wao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natamani sana tutoke hapa tulipo kwa kutumia elimu ambayo sasa hivi tunakwenda kuitekeleza, ambayo ni elimu ya amali. Ninaamini kabisa kila mmoja wetu hapa anatamani tutoke tulipo ingawa tumefungwa kwenye minyororo, lakini inabidi sisi Watanzania wenyewe tujitoe kwenye hiyo minyororo na hata ikibidi kushirikiana na wenzetu kutoka nje, ili kusudi tuweze kuimarisha uchumi wetu kutokana na hii elimu ambayo tunaipata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nishauri kitu. Kutokana na kwamba, tuna wabunifu wengi katika nchi yetu ambao wanaweza wakatusaidia kukuza uchumi wetu, lakini pia tuna elimu ya amali ambayo tumeanza kuitekeleza mwaka huu 2024.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa kwanza ni Serikali ikutane na wabunifu, iangalie changamoto walizonazo, ione mahitaji waliyonayo kwa kuelezwa na wabunifu wao wenyewe na kinachofuata iwawezeshe wabunifu kutekeleza au kubidhaisha bunifu zao. Ninalisema hili kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mara kadhaa tumeona, mwaka hadi mwaka tunapata wabunifu au wavumbuzi wanaobuni vitu vizuri sana. Kuna ambao wamebuni magari, kuna ambao wamebuni pikipiki za umeme, lakini hatujaona kama kuna maendeleo makubwa katika kubidhaisha huu ubunifu wao. Isitoshe wanapewa tuzo kila mwaka. Wengine wanavumbua mashine mbalimbali, lakini kinachotokea ukiwauliza, changamoto waliyonayo wanakwambia hatuna mitaji, hatuna fedha za kutatua baadhi ya changamoto ambazo zipo kwenye ubunifu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba sana Serikali iwawezeshe hawa wabunifu ili kusudi na sisi kama Taifa, tuweze kutengeneza bidhaa tuuze katika nchi yetu na pia tuweze kuuza nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili linatokana na kwamba, kuna nchi ambazo tulikuwa tunashindana nazo kiuchumi, tulikuwa tunalingana nazo miaka ya hamsini na sitini iliyopita, lakini sasa hivi tunanunua bidhaa nyingi sana kutoka kwao. Kwa mfano, bajaji tunanunua kwa nchi za wenzetu ambao tulikuwa nao sawa kiuchumi na wakati huo hawakuweza kutengeneza bajaji wala baiskeli, lakini sasa tunanunua bajaji, tunanunua baiskeli, magari na mashine mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wenzetu wao wamefanya nini? Wanawasaidia wabunifu na wavumbuzi wao na inafikia mahali ambapo wanadiriki hata kununua kama ni magari ama mashine zenye gharama kubwa na kuwaletea wale wabunifu wana-dismantle na kuweza kutengeneza. Ndiyo maana utakuta mashine ile ile utaipata nchi fulani, au nchi fulani. Ni kutokana na haya ambayo wanayafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana Serikali iwasaidie wabunifu wetu ili kusudi elimu hii iweze kutafsirika katika ukuaji wa uchumi wetu. Napenda Serikali iangalie inahitaji nini zaidi, kitu au bidhaa ambazo tunaziagiza sana kutoka nje na ambazo sisi kama Watanzania tunaweza kuzitengeneza, iwa-task hawa wenzetu, i-task hizi shule za amali, i-task vyuo, iwaambie inataka vitu gani ili kusudi waweze kuvitengeneza kwa kutoa vivutio. Ninaamini kabisa Watanzania tunaweza tukatengeneza bidhaa nyingi sana kwa kutumia malighafi zetu na tukaziuza nchi za nje.

Mheshimiwa Spika, nasema tu kwamba, itasaidia kuongeza ajira na kupunguza tatizo la ajira katika nchi yetu, hususan kwa vijana na pia itainua per capita income. Samahani nimetumia neno hilo, yaani itainua kipato cha mtu mmoja mmoja. Pia, itaongeza fedha za kigeni na itapunguza sana ununuaji wa bidhaa za nje, na kwa maana hiyo, tutakuwa na akiba nyingi ya fedha za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi niseme tu kwamba, tukifanya hivi ina maana kweli mbili zitakuwa hazipingani, nikiwa na maana kwamba, tafsiri halisi ya elimu pamoja na elimu ambayo tunai-practice au tunaitekeleza zitakuwa zinaenda sambamba. Hii ni kutokana na alivyosema mtaalamu mmoja, Galileo Galilei, Muitaliano, yeye alisema, “two truths cannot contradict one another.” Kwa hiyo, hizi ni kweli mbili ambazo tukizitekeleza kulingana na tafsiri ya elimu ninaamini kabisa tutakwenda vizuri na tutainua uchumi wa nchi yetu kutokana na elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana suala la upungufu wa walimu, nimelisema hapa mara kadhaa kwamba Mkoa wetu wa Mtwara una upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi zaidi ya 60%. Naomba tupelekewe walimu katika mgao wa walimu maana tulishaahidiwa kwenye Kamati kwamba kuna ajira za walimu, Mheshimiwa Waziri asitusahau.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kuhusiana na mikopo ya vyuo vikuu. Kamati imetoa ushauri kwamba, tuwe na revolving fund, maana naona Waheshimiwa Wabunge wengi waliosimama hapa wamelizungumzia hili suala. Watoto wetu wanateseka sana kiasi kwamba wanafikia mahali wanatamani waache vipindi waende kufanya kazi mitaani ili waweze kupata fedha, hususan wale madaktari wa mwaka wa tatu ambao wanalazimika kufanya field practical, hawa wanataka kazi angalau wapate zile fedha za kwenda kufanya field practical katika maeneo ya nje ya chuo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana Serikali iliangalie hili. Hawa ni watoto wetu, wanateseka, wakiwemo wasichana na wavulana. Kwa kweli, ni hali ambayo inahuzunisha sana. Kwa hiyo, naomba sana revolving fund, fedha zinazorejeshwa ziwekewe uzio zisitoke, na tunaambiwa zipo zaidi ya shilingi trilioni moja ambazo zimeshawahi kurejeshwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hizi tungekuwa tumezitunza ina maana tusingekuwa tunalazimika kuiomba Serikali kila mwaka itoe fedha, zingekuwa zinazunguka hizi hizi, hata kama Serikali inaongeza, basi ingekuwa ni kiasi kidogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho ni malalamiko ya walimu wanapostaafu, wanapata shida sana. Hawapewi fedha za kuhamisha mizigo yao kutoka nyumbani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namalizia kwa kukupongeza wewe, Naibu Spika na Wenyeviti kwa kuliongoza Bunge vizuri.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)