Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kiwani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi jioni hii. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kupata nafasi ya kuweza kuchangia walau mawili matatu katika Wizara hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kwanza namshukuru na ninampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pia Mheshimiwa Dkt. Hussein Ally Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Mheshimiwa Spika, vilevile nampongeza Mheshimiwa Prof. Mkenda Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, hali kadhalika Waziri wetu wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mheshimiwa Leyla Mohamed Mussa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze kwenye udhamini wa masomo ya nje ambao umeasisiwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Udhamini huu unawafanya watoto wasiopungua 600 wa Kitanzania kusoma bila kukopa. Naomba nimwambie Mheshimiwa Profesa Mkenda kwamba, ni lazima vigezo na masharti ya kujiunga na ufadhili huo vizingatiwe.
Mheshimiwa Spika, vigezo ambavyo vinatumika ni vigumu sana kwa wale watoto wanyonge wanaoanza shule za Serikali, ninyi wenzetu huku mnaita Shule za Kata, ambao wanapambana mpaka wakafika kidato cha sita na kuweza kupata Division One za kuanzia point tano, sita na saba, wengi wanatemwa na mfumo huu kiasi kwamba, wanakosa hii fursa ambayo Mheshimiwa Rais kwa nia nzuri kaiandaa. Nakuomba sana Mheshimiwa Profesa Mkenda vigezo hivi tuvibadilishe.
Mheshimiwa Spika, sisi kwa upande wa Zanzibar tuna shule mbili, ambapo kwa upande wa Unguja kuna Sekondari ya Lumumba na Pemba kuna Sekondari ya Fidel Castro. Hizi shule ndizo shule ambazo zinafanya vizuri sana kwenye mitihani yao. Hata mitihani iliyopita ya mwaka 2023 Shule ya Sekondari ya Fidel Castro ilikuwa na wanafunzi 48 waliopata division one, wakiwemo walio na point tano, sita na saba. Pia, Shule ya Sekondari ya Lumumba kwa upande wa Unguja, nayo ilikuwa na wanafunzi 67 ambao walipata Division One, wakiwemo wenye point tatu, nne, tano, sita na kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, cha kushangaza, huu mfumo ambao mmeuweka, sijui ni kwa sababu gani unawatema na wanashindwa kupata fursa hii na matokeo yake wanajiunga kwenye vyuo vikuu kwa kupitia njia ya mkopo kama wanafunzi wengine ambao wamepata daraja la pili.
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni kwamba huu mfumo kaeni nao vizuri, hivi vigezo na masharti aidha vipunguzwe au mfumo uwekwe vizuri ili Watanzania walio wanyonge na yatima waweze kufaidika na hii fursa ambayo kwa nia safi Mheshimiwa Rais kaitoa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi kwa upande wa Pemba niseme kuna mwanafunzi anasoma katika...
SPIKA: Mheshimiwa Mbunge, mtu anayechangia yuko upande wako huku. Sijui kama ulimwona, umekatiza katikati yake. Mheshimiwa Rashid, endelea.
MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa upande wa Pemba tunao wanafunzi waliopata point tano, sita, na saba lakini mfumo haukuweza kuwachukua wakaweza kupata fursa hii. Kadhalika Lumumba wako wanafunzi walio na point nne, tano na sita nao wamekosa hii fursa.
Mheshimiwa Spika, sasa namwomba Profesa na wataalamu wake, najua anao na wanasikiliza, hii fursa ni ya Watanzania Watanzania wote wanyonge na maskini, lakini kwa hivi ambavyo tunakwenda, Profesa lazima ufahamu kwamba fursa hii itatumiwa na wale wazazi ambao wana uwezo, waliosomesha watoto wao kwenye shule za english medium mpaka wakafika kidato cha sita ambapo naamini wewe mwenyewe Profesa unafahamu kwamba shule hizi mwanafunzi haingii kidato cha sita ikiwa ana wastani wa average ‘A’ ya kuanzia point sita.
Mheshimiwa Spika, ni kwamba, una division one ya point saba, lakini huingii kidato cha sita. Sasa hapa ndipo pale ambapo fursa hii inatumiwa na wale walio wengi. Wale wanyonge ambao wanasomeshwa na Serikali zetu hizi mbili bila malipo, wanaweza kukosa fursa hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikija kwenye Baraza la Mitihani, nilipongeze, wanafanya kazi nzuri, nasi sote ni mashahidi, tunashuhudia kila mwaka ufaulu ukiongezeka lakini kuongezeka huku kwa ufaulu pia ni chachu ya mtendaji huyu na wenzake waliopita ambao wanafanya kazi vizuri katika kulisimamia hili Baraza pamoja na mitihani kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, sisi Zanzibar kwa maana ya Kisiwa cha Unguja, tunashukuru kwamba sasa Baraza la Mitihani wamejenga ofisi nzuri ya kisasa ambapo waratibu wale wa mikoa na wilaya sasa wamepunguziwa gharama zile za kuja kufuata shughuli za mitihani huku Tanzania Bara. Wana ofisi nzuri na ya kisasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, tunapozungumzia Zanzibar, ni Unguja na Pemba. Mara nyingi ukisema Zanzibar watu wanahisi ni Zanzibar tu, lakini Zanzibar ni Unguja na Pemba. Kwa hiyo, nasi kule Pemba tunahitaji uwepo wa ofisi ambayo itaenda sambamba na hii namna ya ufaulu ambao unaongezeka siku hadi siku.
Mheshimiwa Spika, kingine naomba nimwulize Mheshimiwa Prof. Mkenda, katika kuchangia kwangu aweze kuja kunijibu hapo. Januari, 2020 katika jimbo langu kulifunguliwa skuli moja kubwa ya sekondari ambapo Mgeni Rasmi alikuwa ni Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein na Skuli ile ikaitwa jina la Samia Suluhu Hassan. Hadi nazungumza hapa na hadi matokeo ya kidato cha nne yaliyotoka 2023, bado jina la skuli lililotolewa na Mheshimiwa Rais halijatumika. Ukiangalia kwenye records zao wataikuta inaitwa Skuli ya Sekondari ya Muambe. Hivi Mheshimiwa Prof. Mkenda kubadilisha jina nako kunahitaji upewe bajeti na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu?
Mheshimiwa Spika, kubadilisha jina tu la shule kutoka Muambe Secondary School ukaipeleka kuwa Dr. Samia Suluhu Hassan Secondary School, kunahitaji bajeti? Hivi hapa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu akupatie fedha za kubadilisha jina? Mwaka huu ni wa nne, naomba sana kwenye mitihani ya mwka 2024, skuli hii yenye jina la kiongozi wetu wa nchi liweze kusomeka katika majina ya orodha ya skuli ambazo wanazo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia tuwapongeze Wizara ya Elimu. Tulisema sana na tukaomba sana hapa namna ya kujengwa Chuo Kikuu Huria kule Pemba, tayari tunashukuru, ndani ya wiki hii mkandarasi anakwenda Pemba kukabidhiwa site. Tunashukuru sana kwa kazi kubwa ambayo wameifanya. Pia kuna Chuo cha Mwalimu Nyerere, chuo cha kisasa kimeshajengwa kule na ombi langu hapa, hiki chuo kimekamilika, kinachohitajika hapa, kipatiwe samani kwa maana ya furniture.
Mheshimiwa Spika, pia pale mahali chuo kilipo, lazima hapa Mheshimiwa Prof. Mkenda atenge bajeti ya kupata usafiri kwa ajili ya wanachuo. Hii itawasaidia sana wanafunzi kwa ajili ya dharura ambazo zitatokea, kadhalika na mahitaji madogo madogo yanayohitaji kutumia usafiri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakuheshimu sana na ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii na wala sisubiri kengele. Naunga mkono hoja. (Makofi)