Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hii niweze kuchangia Wizara hii ya Elimu. Wizara hii ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba kumpongeza Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyopeleka fedha nyingi kwenye miradi ya elimu nchini.
Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Wizara kwa ujumla kwa kuweza kuanza mtaala mpya ndani ya shule zetu. Kwanza nianze na changamoto, kwani ndiyo zitajitokeza ili mweze kuzifanyia kazi. Hongera sana Mheshimiwa Waziri na Wizara kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, naomba kujikita mchango wangu kwenye maeneo yafuatayo: nikianza na ujenzi wa vyuo vya VETA vya Wilaya katika ukurasa wa 30, ni jambo zuri sana kujenga VETA kila Wilaya, na kwa hili naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa namna ilivyolisimamia hili kwa nguvu zote kwa kuhakikisha kuwa kila Wilaya inakuwa na VETA.
Mheshimiwa Spika, pamoja na nia hii nzuri, bado nina swali kwa Wizara kuhusu namna gani wamejipanga kuwa na walimu, vifaa na vitendea kazi katika kuwezesha vyuo hivi kufanya kazi vizuri na kwa ufanisi kama inavyotarajiwa na Watanzania.
Mheshimiwa Spika, kuhusu uwiano mkubwa wa wanafunzi kwa darasa (msongamano wa wanafunzi darasani), pamoja na kazi kubwa iliyofanyika kwenye elimu nchini, bado kuna changamoto kubwa ya wanafunzi kusongamana madarasani. Hali hii inachangiwa na uhaba wa madarasa kwa baadhi ya maeneo, pia uchache wa walimu. Tatizo hili linaathiri sana ubora wa elimu kwa shule za umma. Ipo haja sasa ya Wizara kuangalia namna ya kutatua tatizo hili.
Mheshimiwa Spika, naiomba Wizara ya Elimu iangalie eneo hili. Shule na madarasa yameendelea kujengwa kwa fedha za miradi kama vile SEQUIP, BOOST, GPE – na HEET lakini tatizo bado linaendelea. Nataka kujua nini mkakati wa Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Elimu kumaliza tatizo hili la msongamano wa wanafunzi darasani?
Mheshimiwa Spika, miundombinu ya sekta ya elimu nchini inahudumiwa na kujengwa kwa kutumia fedha za wahisani kupitia Benki ya Dunia na washirika wa maendeleo. Je, ni upi mkakati wa Serikali ili tusiendelee kutegemea hizi projects kwa kiwango hiki kikubwa? Je, siku ikitokea hatuna miradi ya wafadhili, madarasa yatakuwa hajengwi? Wizara ije na mkakati mahsusi wa namna ya kumaliza changamoto ya vyumba vya madarasa kulingana na projections ya population growth na enrolment rates katika taasisi zetu za elimu.
Mheshimiwa Spika, hivi sasa Serikali imekuwa na utaratibu wa kutoa maelekezo ya kila mwaka kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya na Halmashauri kuhusu ujenzi wa madarasa bila kuangalia uwezo na vyanzo vya fedha kwa ajili ya kutekeleza maagizo hayo. Utaratibu huu siyo endelevu na wakati mwingine wanatumia mwanya huo kuchepusha fedha wakisingizia kutekeleza maelekezo ya Wizara.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.