Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AMINA BAKAR YUSSUF: Mheshimiwa Spika, naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya hasa katika Wizara hii ya Elimu kwa Watanzania.
Mheshimiwa Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Naibu Waziri pamoja na wasaidizi/watendaji wake wote wa Wizara hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kazi kubwa wanayoifanya ndani ya Wizara hii.
Mheshimiwa Spika, nianze mchango wangu kuhusu mfumo wetu wa elimu nchini ambao haumwandai mwanafunzi kuweza kujitegemea mara baada ya kumaliza masomo yake. Hivyo basi, kuna haja ya kuboresha mfumo wetu wa elimu nchini ili mfumo wa elimu uweze kumwandaa mwanafunzi kuweza kujitegemea mara baada ya kumaliza masomo yake bila ya kusubiri kuajiriwa.
Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali kupitia Wizara kupeleka vifaa vya kisasa vya kufundishia kwa walimu na wanafunzi kwa wakati shule zote nchini, pia Wizara iboreshe mazingira wezeshi kwa walimu kutokana na mazingira yaliyopo maeneo yao hasa vijijini.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kuna changamoto ya ukosefu wa ajira nchini, naishauri Serikali kupitia Wizara hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iboreshe na iongeze kujenga Vyuo vya Elimu Amali/Vyuo vya Kati kote nchini, pamoja na kupeleka vifaa vya kisasa vya kufundishia ili kuzalisha wataalam wengi wa fani mbalimbali bobezi. Hii itasaidia jamii kuthamini vyuo hivyo vya kati na vijana wengi kujiunga na kunufaika kwa wingi zaidi na itasaidia sana kupunguza wimbi kubwa la vijana wasio na ajira, vijana wazururaji pamoja na vijana wanaosubiri ajira Serikalini, na pia itapunguza mzigo mkubwa kwa Serikali.
Mheshimiwa Spika, licha ya maboresho mengi ya mitaala na Sera ya Elimu kufanyika, ni vyema Wizara ikawawekea wanafunzi somo maalum la stadi za maisha, stadi za kazi, pamoja na somo la uzalendo ili kuwajenga watoto kuitambua nchi yao kiundani pamoja na kujitambua wao wenyewe ili wawe raia wema na kuwa wazalendo wa nchi yao, kwa sababu vijana wengi waliosoma, wakirudi mitaani wanafanya matukio ya ajabu ajabu yakiwemo wizi na mauaji. Hii yote inasababishwa na kukosa uzalendo na kutokujitambua.
Mheshimiwa Spika, pia kuna haja ya kuwapunguzia mzigo mkubwa wa idadi ya masomo watoto ili kuwapa wepesi katika ufahamu wa masomo yao na wanachokisoma.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.