Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata nafasi hii ya kuchangia hoja hii muhimu kwa ajili ya maslahi mapana ya Watanzania.
Mheshimiwa Spika, pili, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mageuzi makubwa aliyoyafanya katika sekta ya elimu kwa ujenzi wa madarasa ya kisasa, ujenzi wa vyuo vya VETA 29 ambavyo vimekamilika na vingine vinaendelea kujengwa, na utoaji wa vishikwambi kwa walimu ambacho ni kielelezo tosha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kufanya maboresho makubwa katika elimu. Nampongeza sana.
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Prof. Adolf Mkenda, yeye na timu yake kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya na timu yake. Nawapongeza sana.
Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia maboresho ya mtaala mpya uliofanyiwa marekebisho mwaka 2023. Mtaala huu ni mzuri kwa kuwa unalenga kuwafanya watoto wetu watoke na ujuzi na endapo utatekelezwa ipasavyo, utasaidia vijana wengi kujiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa, lakini changamoto ninayoiona hapa ni namna ya utekelezaji wake.
Mheshimiwa Spika, kama kweli tunataka ukombozi wa Taifa hili na tunataka maendeleo endelevu, ni lazima tuwekeze kwenye elimu. Mataifa kama China na Marekani yamefanikiwa katika uchumi kwa sababu ya elimu. Serikali iangalie na ijue nini kifanyike ili maboresho ya mtaala huu yaweze kuwa na tija.
Mheshimiwa Spika, nashauri kwamba, kwanza Serikali itenge fedha za kutosha kwa ajili ya kujenga karakana na maabara za kisasa zinazoendana na wakati huu wa sayansi na teknolojia. Pia walimu wapya na wa zamani wajengewe uwezo kwa kuwapa mafunzo ya mara kwa mara yanayoendana na nyakati za sasa. Aidha, Serikali itenge fedha za kutosha za kununua vitendea kazi kwa ajili ya mafunzo ya ufundi stadi na kuwepo na TV screen angalau moja katika vyuo vyetu vya ufundi ili wakati mwingine wanafunzi waweze kujifunza kwa njia ya video.
Mheshimiwa Spika, mwanafalsafa mmoja wa Marekani, John Dewey's amewahi kusema, elimu ni maisha na elimu ni kila kitu kwa mwanadamu. Kwa maboresho ya mtaala huu mpya ni kuwapa maisha vijana wetu endapo tu Serikali itajikita kwa nguvu zake zote kuutekeleza mtaala huu ipasavyo.
Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi na naunga mkono hoja.