Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kuchukua fursa hii adhimu na adimu kumshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyenipa kibali cha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu na kuniwezesha kuchangia hoja iliyoko mbele yetu.
Mheshimiwa Spika, kipekee naomba kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini ili kuweza kumsaidia katika Wizara yetu ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, mimi pamoja na Waziri wangu, Mheshimiwa Profesa Adolf Mkenda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, napenda kukushukuru wewe binafsi, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson Mwansasu, Spika wetu, lakini vilevile Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge kwa umahiri wenu kuweza kusimamia na kutuongoza katika mjadala wa hoja hii muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee namshukuru sana Mwenyekiti wetu wa Kamati, Mheshimiwa Husna Sekiboko pamoja na Wajumbe wote wa Kamati hii ya Elimu, Utamaduni na Michezo, kwanza kwa kuweza kuchambua shauri letu hili.
Mheshimiwa Spika, Wajumbe wote walishiriki kuchambua na kushauri Wizara kikamilifu. Kipekee nichukue fursa hii kuwashukuru kwa kupitia taarifa yetu na vilevile kuchangia katika makadirio haya ya mapato na matumizi ya mwaka 2024/2025. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipekee naomba kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wametoa michango yao hapa, wametoa pongezi, ushauri na maoni yaliyolenga kuboresha Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na ubunifu. Ndugu zangu, kipekee tunaomba tuwashukuru, na tumepokea pongezi zenu, maoni yenu pamoja na ushauri mlioutoa kwa lengo la kwenda kuboresha utendaji kazi katika Wizara yetu. Ahsanteni sana Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipekee naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa uongozi wake na ushauri. Mheshimiwa Waziri huyu siyo tu ni kiongozi, lakini ni mwalimu. Kwangu mimi ni rafiki wa karibu sana. Mheshimiwa Waziri, nakushukuru sana kwa uongozi pamoja na ushauri wako katika uendeshaji wa Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipekee, namshukuru sana Prof. Nombo, Katibu Mkuu wetu; Naibu Makatibu Wakuu, Prof. Mdoe pamoja na Dkt. Franklin, Menejimenti ya Wizara na watumishi wenzangu wote, kwa ushirikiano mnaotupa katika kuendesha Wizara hii muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nichukue fursa hii kuwashukuru sana wananchi wangu au wananchi wenzangu wa Mafia kwa kuendelea kuniamini na vilevile kunipa ushirikiano na kunivumilia katika kipindi chote ambacho natekeleza majukumu ya Serikali ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, siku ya tarehe 03, 04 na 05, kumetokea dhoruba kubwa kule Mafia, Kimbunga Hidaya, kimeweza kuvamia eneo lile lote la ukanda wa Pwani. Athari zimekuwa ni kubwa na matatizo makubwa yametokea na uharibifu mkubwa wa mali umetokea. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kuwapa pole wananchi wenzangu katika madhara na madhila haya yaliyotukumba.
Mheshimiwa Spika, natoa wito kwamba tuendelee kuwa wavumilivu na tuendelee kufanya subira katika kipindi hiki wakati Serikali inalishughulikia jambo hili. Sambamba na Mafia, nafahamu vilevile janga hili liliweza kufika maeneo ya Kilwa, Lindi pamoja na Mtwara na maeneo yote ya Ukanda wa Pwani. Basi nichukue fursa hii kuwapa pole wananchi wote waliokumbwa na madhila haya ya Kimbunga Hidaya.
Mheshimiwa Spika, kipekee naishukuru familia yangu kwa ujumla, watoto pamoja na wake zangu kwa kuendelea kunivumilia, kuniombea dua pamoja na kunipa ushirikiano katika kipindi hiki chote cha kutekeleza majukumu yangu.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naomba nami nichukue fursa hii kutoa ufafanuzi na kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la kwanza, ambalo ningependa kuchangia ni mafunzo ya walimu kwa ajili ya utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa. Nafahamu Wabunge wengi wamechangia kwenye eneo hili na kuonesha wasiwasi wao na kutaka kujua namna gani Serikali itafanya.
Mheshimiwa Spika, naomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu kwanza kwenye eneo la mafunzo ya walimu, Serikali yenu kupitia Wizara ya Elimu, tumeweza kutekeleza au kutoa mafunzo kwa walimu wote ambao tunatarajia watakwenda kufundisha katika mtaala huu ulioboreshwa. Kwa ujumla Serikali imetoa mafunzo kwa walimu wanaopaswa kufundisha zaidi ya 181,777 wa elimu ya awali mpaka wale wa darasa la saba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imeweka mpango endelevu kwa sababu mafunzo haya siyo kwamba yatatolewa tu katika kipindi hiki ambacho tumeanza kutekeleza mtaala, lakini yatakuwa ni mafunzo endelevu katika maeneo yote ya nchi yetu ili kuhakikisha kwamba tunatengeneza umahiri kwa walimu wetu pindi watakapokuwa wanakwenda kuwafundisha vijana wetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuna yale maeneo ya the Teachers’ Resource Centres, zitaendelea kutumika na hivi sasa tumeendelea kuziboresha kwa maana ya kuzifanyia ukarabati na vilevile kuongeza vifaa mbalimbali vya kujifunzia na kufundishia kwenye zile cluster zetu mbalimbali. Katika ngazi ya cluster vilevile mafunzo haya yatakuwa yanaendelea kutolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile Waheshimiwa Wabunge wameonesha wasiwasi mkubwa kwenye eneo la elimu ya amali, ambapo tumeanza kutekeleza kwa upande wa sekondari, elimu ya amali kwa kidato cha kwanza. Kitu gani ambacho tumefanya mpaka hivi sasa? Serikali kwa kushirikiana na taasisi zilizopo chini ya Wizara, imefanya maandalizi ya walimu kwa ajili ya utekelezaji wa mitaala mipya.
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, hapa kilichofanyika ni kuanza kutoa mafunzo kwa walimu watakaokwenda kufundisha katika elimu hii ya amali. Walimu 552 wa shule za sekondari zinazofundisha masomo ya amali wameweza kupata mafunzo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile mafunzo yametolewa kwa walimu 346 wa sekondari wanaofundisha masomo ya jumla. Tunajua kwamba katika utaratibu au mfumo huu, sasa hivi kutakuwa na michepuo miwili. Kutakuwa na yale masomo ya kawaida na vilevile kutakuwa na yale masomo ya amali. Kwa hiyo, tumetoa mafunzo kwa walimu wale ambao watafundisha masomo ya amali.
Mheshimiwa Spika, vilevile kutakuwa na masomo ya kawaida ambayo nayo tumeweza kuwapa mafunzo walimu 346 kwenye masomo haya ya jumla katika mkondo wa amali wa kidato cha kwanza ambapo walimu wa shule za Serikali walikuwa ni 147, na kwa shule zile za binafsi walikuwa ni walimu 199. Tunafahamu kwamba tuna shule 98 ambazo zimeanza kutoa elimu hii ya amali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jitihada za upatikanaji wa walimu wa kutosha kwa upande wa elimu ya amali zinaendelea kupitia mafunzo ya wenzetu wa VETA, ambapo walimu wa mafunzo ya amali zaidi ya 68 wameweza kupata mafunzo. Vilevile kupitia taasisi yetu ya Mamlaka ya Baraza la Elimu ya Ufundi, imeweza kuwafundisha walimu 843, wamepata mafunzo haya ya elimu hii ya amali kwenye shule zetu hizi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, juhudi hizi zinaendelea na niwaondoe hofu na sisi tutazisimamia kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha kwamba ule umahiri unakwenda kutengenezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la pili au hoja ya pili ilikuwa ni ya uhaba wa walimu kwa ujumla. Nini Serikali imefanya kwenye eneo hili? Katika kukabiliana na uhaba wa walimu, pamoja na jitihada zilizofanywa za kuongeza ajira za walimu, tunafahamu Serikali yetu kwamba imekuwa ikiajiri walimu kila mwaka. Sambamba na hilo, Serikali imeendelea na mikakati mingine endelevu kuhakikisha tunapunguza uhaba wa walimu kwa kuwawezesha walimu. Kwa hiyo, sasa tutakuwa na mfumo wa kuwawezesha walimu kuwa na mfumo wa kupata internship. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, walimu wote sasa watakaokuwa wanamaliza course zao za ualimu kabla ya kwenda kazini tutakuwa na mfumo wa kupata internship ya mwaka mmoja ili baadaye waje kupata leseni. Katika mfumo huu tutakwenda kupunguza tatizo la upungufu wa walimu zaidi ya 12,988 kila mwaka. Kwa hiyo, ni lazima mwaka mzima hawa waweze kukaa shuleni kwa ajili ya kujifunza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika kupeleka walimu wetu internship, tutakuwa na faida zifuatazo: -
(i) Tutawa-expose walimu wetu kwenye uzoefu halisi kuhusu fani ya ualimu katika mazingira halisi ya shule;
(ii) Watapata uzoefu wa namna ya kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wa ufundishaji na ujifunzaji; na
(iii) Tutawapa nafasi walimu wetu (wahitimu) katika ualimu kwa kushirikiana na walimu wazoefu katika eneo la kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, mkakati mwingine wa Serikali ni kuendelea kutumia fursa za walimu wa kujitolea na tumeshatoa miongozo mbalimbali ya namna gani ya kupata hao walimu wa kujitolea kabla hawajapata ajira zao. Kwa hiyo, mkakati huu nao vilevile utaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine kwenye upungufu katika eneo la elimu ya amali, nimezungumza kule nyuma, lakini sasa tuna mkakati kwa upande wa elimu ya amali ambapo tumedhamiria kuchukua hatua kadhaa. Eneo la kwanza ni kuhakikisha tunakabiliana na upungufu wa walimu wa mafunzo ya amali.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuwatambua walimu wa mkondo wa amali waliopo kwenye shule zisizokuwa na mikondo ya amali. Kwa hiyo, tumetambua zaidi ya walimu 18 na tumeweza kuwahamisha kutoka kwenye shule zile ambazo zilikuwa hazifundishi masomo hayo na kuwapeleka sasa kwenye shule ambazo zinafundisha mikondo ya amali na walimu hawa wamepelekwa takribani katika shule tisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la pili, Serikali itaendelea na uzalishaji wa walimu wa mafunzo ya amali katika ngazi za vyuo vikuu ambapo sasa kuna vyuo vikuu ambavyo tunakwenda kuvibadilisha ili viweze kutoa elimu ya amali.
Mheshimiwa Spika, naomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu kwamba Chuo chetu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya tunakwenda kuki-convert na kutengeneza campus katika Mkoa wa Mtwara, kwa vile vyuo viwili, Mtwara Kawaida na Mtwara Ufundi ambapo sasa zile zitakuwa ni campus maalum kabisa kwa ajili ya kuzalisha walimu wa amali.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Chikota, wakati anazungumza hapa kwamba, lini Mtwara itapata chuo kikuu? Sasa tunakwenda na mpango huu ambapo vyuo vile viwili tunakwenda kuvifanya viwe campus ya Chuo Kikuu cha Mbeya na specifically vitakuwa ni kwa ajili ya kuzalisha walimu hawa wa amali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mkakati wa tatu, kwenye mitaala yetu ya vyuo vikuu, tunajua kwamba katika mkondo huu wa elimu ya amali utakuwa unaanzia kidato cha kwanza huko, lakini dhamira ni kufika mpaka chuo kikuu. Kwa hiyo, vyuo vikuu sasa kupitia mradi wetu wa HEET, vinafanya mapitio ya mitaala ile ili kuhakikisha kwamba tunazalisha walimu ambao vilevile watakuja kufundisha mkondo wa amali kuanzia ngazi ya sekondari mpaka vyuo vikuu kwa wale wanafunzi watakaofika mpaka vyuo vikuu.
Mheshimiwa Spika, mkakati wetu wa nne pamoja na jitihada hizo za Serikali katika kupata walimu wa mafunzo ya amali, Wizara ya Elimu, Utumishi pamoja na TAMISEMI tutaendelea kuajiri walimu katika kada hii ya elimu ya amali.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine iliyofikishwa mbele hapa ni usambazaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia hasa kwenye shule hizi ambazo zimeanza mkondo wa amali. Naomba niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari alishatoa fedha kwenye shule zile 28 za Serikali, jumla ya shilingi bilioni nne kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunanunua vifaa vya kujifunzia na kufundishia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Taasisi yetu ya Elimu tayari ilishachapisha nakala 4,500 za masomo manne ya Historia ya Tanzania ambayo wataanza Kidato cha Kwanza; Mathematics for Ordinary Education, Form One; Business Education for Lower Secondary Education, Form One, pamoja na English Low Level Secondary Education ya Form One. Vitabu hivi nakala 4,500 tayari vilishachapishwa na kupelekwa kwenye shule hizi zote za amali, zile za Serikali, na zile shule 68 za binafsi katika uwiano wa mwanafunzi mmoja kwa kitabu kimoja.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kuna yale masomo ya jumla, tayari taasisi yetu ya TET imechapisha jumla ya nakala 104,956 ya vitabu tu vya kiada ambavyo tutakwenda ku-compliment kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la Shule za Msingi, hapa vilevile Waheshimiwa Wabunge walionesha wasiwasi kwenye eneo hilo.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Dakika moja malizia Mheshimiwa.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hilo kuhusu usambazaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia kwenye shule zetu za msingi, madarasa yaliyoanza kutekeleza mtaala huu ulioboreshwa ni darasa lile la awali, darasa la kwanza na darasa la tatu. Niwaondoe hofu Waheshimiwa Wabunge kwamba tayari nakala ngumu 9,825,601 zilichapishwa na zimesambazwa. Kuna upungufu kwenye baadhi ya mikoa ambayo hatujaweza kuifikia yote kwa ukamilifu, lakini kwa mikoa ambayo tayari vitabu hivi vimeshapelekwa kwa uwiano wa 1:2 mpaka 1:4 kwa mwanafunzi kwenye mikoa mingi sana, imeshapelekwa isipokuwa kwenye mikoa 10 vitabu hivi havijapelekwa kwa ujumla wake, tumepeleka kiasi fulani, lakini bado havijakamilika.
Mheshimiwa Spika, mikoa hiyo 10 ni pamoja na Mkoa wa Iringa, Katavi, Mara, Mbeya, Mtwara, Mwanza, Rukwa, Shinyanga, Simiyu, Songwe na Tabora. Kwa hiyo, kazi ya usambazaji wa vitabu hivi unaendelea, tumefikia 91% na baada ya muda siyo mrefu tutakuwa tumekamilisha. Hii ni kutokana tu na hali ya hewa ambayo imejitokeza.
Mheshimiwa Spika, maelezo ni mengi, lakini kutokana na muda, naomba kuunga mkono hoja. Nadhani hoja zilizobaki Mheshimiwa Waziri atakuja kuzimalizia.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. (Makofi)